Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akiwa katika mazungumzo na Mwenyeji wake Makamo wa Rais wa Indonesia Mohammed Jusuf Kalla (kushoto) leo Ofisini kwake katika Mji wa Jakarta nchini Indonesia katika ziara ya maalum ya mualiko wa siku saba,[Picha na Ikulu.] 01/08/2018.
Viongozi hao walifanya
mazungumzo katika Ofisi ya Makamo wa Rais wa Indonesia Muhammad Jusuf Kalla
iliyopo mjini Jakarta Indonesia, ambapo mkutano huo pia ulihudhuriwa na
Mawaziri wa pande zote mbili.
Katika mazungumzo hayo
Rais Dk. Shein alimpongeza Makamo wa Rais wa nchi hiyo kwa muwaliko wake huo
muhimu ambao unaimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya
Indonesia na Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa jumla na makhsusi kwa Zanzibar.
Dk. Shein alimueleza
Makamo huyo wa Rais wa Indonesia kuwa Tanzania inajivunia kwa kiasi kikubwa
uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo ambao
umeasisiwa na viongozi wakuu wa nchi hizo tokea miaka ya sitini na kuahidi kuwa
utaendelezwa.
Alieleza kuwa tangu
mwaka 1964 kulikuwa na uhusiano na ushirikiano mkubwa kati ya Zanzibar na
Indonesia hasa katika biashara ya karafuu
ambapo wakati huo zao hilo lilikuwa likizalishwa kwa wingi zaidi na bei yake
kuwa juu katika soko la dunia, Indonesia ikiwa moja ya wanunuzi wakubwa.
Aidha, Dk. Shein
alieleza kuwa Indonesia imekuwa ikiunga mkono juhudi za Zanzibar kwa kusaidia
maeneo mbali mbali yakiwemo ya kuwajengea uwezo wananchi hasa katika sekta ya
elimu na kilimo na kusisitiza haja ya kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano.
Kwa upande wa sekta ya
kilimo Rais Dk. Shein alieleza haja ya kuongeza uzalishaji wa mpunga sambamba
na kuangalia kilimo cha mwani na mazao yake.
Dk. Shein alieleza haja
ya kuirejesha biashara ya karafuu sambamba na kuwawezesha vijana kujiajiri
katika kilimo kwa kuwapatia taaluma ya teknolojia mpya kwenye kilimo cha
mikarafuu.
Kwa upande wa eneo la
uvuvi ambapo ni eneo jipya la ushirikiano, Rais Dk. Shein alieleza kuwa ni
vyema na eneo hilo likaangaliwa kwa upeo mkubwa zaidi hasa katika kuimarisha
uvuvi kwa kutumia teknolojia ya kisasa kwenye kuvua, hasa katika bahari kuu.
Akieleza kuhusu sekta ya
utalii, Rais Dk. Shein alisema kuwa juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa
na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi sasa katika kuhakikisha idadi ya
watalii inaongezeka hasa ikizingatiwa kwamba sekta hiyo inachangia asilimia 80
ya mapato ya serikali kwa fedha za kigeni sambamba na kuchangia kiasi kikubwa
katika pato la Taifa.
Aliongeza kuwa katika sekta
ya utalii katika kipengele cha ukarimu ni vyema yakaimarishwa mashirikiano kati
ya pande mbili hizo hasa ikizingatiwa kuwa Indonesia tayari imeshapata
mafanikio makubwa.
Dk. Shein alieleza kuwa
mbali na juhudi hizo pia, hatua za makusudi zimekuwa zikichukuliwa katika
kuhakikisha utalii wa Zanzibar unatangazwa na kusisitiza kuwa ili utalii uweze
kutangazwa vizuri ni vyema kukawa na njia nzuri za kuwasafirisha watalii.
Rais Dk. Shein pia,
alitumia fursa hiyo kueleza haja ya kuwepo na kuimarisha ushirikiano katika
Nyanja ya utafiti na maendeleo ambalo ni eneo jengine la ushirikiano na
kupelekea taasisi za elimu kuhusishwa
ikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Taasisi ya Afya pamoja na
Taasisi ya Utafiti wa Mifugo.
Alieleza kuwa taasisi hizo
ni vyema zikashirikiana na zile za Indonesia, katika nyanja mbali mbali, ikiwa
ni pamoja na kubadilishaja taaluma na uzoefu chini ya Mpango wa ushirikiano wa Nchi
za Kusini mwa Dunia hasa katika sekta ya utalii,kilimo, afya na elimu.
Dk. Shein alieleza kuwa
tayari Zanzibar ina Vyuo vitatu vya Amali kwa ajili ya kuwajengea uwezo vijana
wa kujiajiri, hivyo aliona haja kwa Mawaziri husika kukutana pamoja kujadili
namna bora ya kushirikiana katika nyanja hiyo.
Akieleza kuhusu suala
zima la uchumi wa kisasa, Rais Dk. Shein alieleza umuhimu wa kuwepo kwa mashirikiano
katika kuimarisha uchumi wa kisasa kwa kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika miradi ya miundombinu, kwa njia ya mashikiano
na sekta binafsi.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alimualika Makamo huyo wa Rais wa Indonesia kuhudhuria katika sherehe
za maadhimisho ya miaka 55 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar hapo Januari
mwakani ambapo kiongozi huyo alikubali mwaliko huo.
Nae Makamo wa Rais wa
Indonesia Muhammad Jussuf Kalla kwa upande wake alimpongeza Rais Dk. Shein kwa
kukubali mwaliko wake huo na kumueleza kuwa Indonesia itaendeleza uhusiano na
ushirikiano uliopo ambao umewekwa na waasisi wa Mataifa hayo.
Makamo wa Rais huyo alieleza kuwa uhusiano huo ulianza
kutoka kwa Baba wa Taif Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Baba wa Taifa hilo
Soekarno Hatta.
Katika maelezo yake,
kiongozi huyo alieleza kuwa kuna haja ya kuongeza mashirikiano hasa katika
sekta ya biashara kati ya pande mbili hizo hasa kutokana na soko kubwa la
biadhaa za nchi hio kwa Afrika.
Akieleza katika sekta ya
utalii, Makamo huyo wa Rais ameleza kuwa kuwepo kwa mashirikiano kati ya pande
mbili hizo kutasaidia kuimarisha sekta hiyo hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar ina
vivutio vingi vya kitalii zikiwemo fukwe nzuri.
Alieleza kuwa kutokana
na Indonesia kuwa na Chuo Maalum cha Kitalii wanaona haja ya kushirikiana na
Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo ya utalii katika Nyanja ya mafunzo.
Kiongozi huyo pia, aliahidi
kuunga mkono katika kuimarisha sekta ya kilimo kwa kutoa mafunzo hasa katika
kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga na kueleza haja ya vijana wa Kizanzibari
kwenda kujifunza nchini humo kutokana na nafasi maalum watakazozitoa.
Makamo wa Rais, alieleza
kuwa mmano Agosti 26 mwaka huu Indonesia itafanya mkutano wa Kimataifa wa
Kilimo ambao utagusia kilimo cha mpunga na kutafuta njia za kuwasaidia vijana
katika kuhakikisha wanajihusisha na kilimo.
Aidha, alitilia mkazo
suala la kubadilishana uzoefu kwa vijana huku akieleza namna ya kuwasaidia
vijana kwa kuwapa ufadhili katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo utalii,
uvuvi, mifugo na kilimo.
Aliongeza kuwa nchi yake
imekuwa ikitoa mafunzo ya amali kwa vijana
na kueleza kuwa mbali ya mafunzo hayo pia, wako tayari kuengeza maeneo
mengine yakiwemo uvuvi, utalii, mifugo na kilimo kwa vijana wa Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment