Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Afungua Maonesho ya Kilimo ya NaneNane Dole Zanzibar.




Na.Othman Khamis.OMPR. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa wito kwa Wananchi wote kuendelea kuzingatia njia za uzazi wa mpango uliokubalika katika Mila na desturi zao ili kukabiliana na tishio la uvamizi wa maeneo ya Kilimo yanayotumiwa hivi sasa kwa shughuli za Makaazi linalosababishwa na chanzo cha ongezeko kubwa la Idadi ya Watu.
Alisema ongezeko la Watu takriban la asilimia 3% kwa mwaka linachangia kwa kiasi kikubwa maeneo hayo ya Kilimo na hifadhi za misitu kutumika bila ya mpangilio kasi ambayo kama haikudhibitiwa sasa inaweza kuleta janga kubwa la Kimazingira na uhaba wa chakula hapa Nchini.
Akiyafungua Maonyesho  ya Siku ya Wakulima, Nane - Nane 2018 yanayofanyika Kizimbani Wilaya ya Magharibi  “A” Balozi Seif Ali Iddi alisema Visiwa vya Zanzibar hivi sasa vimekumbwa na tishio la uvamizi wa maeneo ya kilimo jambo ambalo ni hatari kwa kizazi cha sasa na kile cha baadae.
Alisema Ardhi ya Visiwa vya Zanzibar  haiongezeki na wakati mwengine hukumbwa na mmong;onyoko unaosababishwa na maji ya Bahari , hivyo ni jukumu la Wataalamu wa Kilimo kuendelea kutoa Elimu juu ya matumizi sahihi ya ardhi yatakayozingatia uzalishaji wa mazao mengi kwa kutumia ardhi ndogo.
Balozi Seif alieleza kwamba Taalum hiyo vi vyema pia ikawahusisha Wananchi wanaisho maeneo ya Mijini ili wajenge tabia ya kupenda kulima katika sehemu wanazoishi kijuilikanacho kwa umaarufu wa Kilimo cha Mjini kilichojipatia umaarufu mkubwa Duniani.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatekeleza  mkakati wa kuleta Mapinduzi ya Kilimo Nchini kwa kukifanya Kilimo kuwa cha kisasa, cha kitaalamu na Kibiashara.
Balozi Seif alifahamisha kwamba juhudi hizo zimesaidia kuongeza uzalishaji wa matunda na mazao ya chakula kwa kufikia Tani  Laki 357,932 kwa Mwaka 2017 ikiwa ni ongezeko la Asilimia 32.1 ikilinganishwa na uzalisihaji wa Tani  Laki 111,882 kwa Mwaka 2016.
Alisema mafanikio hayo yanaonyesha wazi kuwamba Taifa kwa kushirikiana na Wananchi likiwekeza kwa wingi kwenye sekta ya kilimo maendeleo ya Viwanda kama Kauli mbiu ya mwaka huu inayoeleza wekeza katika kilimo, mifugo na uvuvi kwa maendeleo ya Viwanda yatapatikana.
Akizungumzia ushiriki wa Vijana katika Sekta ya Kilimo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif Ali Iddi alisema upo umuhimu mkubwa wa kuongeza uzalishaji ndani ya Sekta hiyo kwa kuwashajiisha Vijana kujishughulisha na Kilimo.
Alisema ni ukweli usiopingika kwamba Kilimo Nchini bado kinaendeshwa kwa asilimia kubwa na Wazee hali inayopaswa kurekebishwa  na Vijana wenye dhana potovu ya kufikiria kazi inayowahusu  wao ni ile ya ajira kutoka vikosi vya ulinzi pekee.
Balozi Seif  alisema Jamii haina budi kuwavuta Vijana kwenye Kilimo, Uvuvi na Ufugaji wakiwa bado wadogo mvuto unaopaswa kwenda sambamba na fikra za kubadilisha Mitaala Maskulini kwa kuongeza somo la Kilimo ili Mwanafunzi ajifunze Kilimo bado akiwa Skulini.
Alitoa ombi kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuzitaka Skuli za Sekondari za Serikali na zile Binafsi kuandaa safari za masomo kwa Wanafunzi wake za kwenda kutembelea maonyesho hayo ya Wakulima ya Nane nane ili kujifunza kwa vitendo.
Alisema safari hizo ni vyema zikawa za kudumu kwa kila Skuli kutokana na Maonyesho hayo kufanyika kila Mwaka ambapo yapo mambo mengi ambayo Wanafunzi hao wanaweza kujifunza ikiwemo fani ya Kemia, Biolojia pamoja na mazingira.
“ Ombi hili pia nalitoa kwa Mabaraza ya Vijana, Vikundi vya Mazoezi, Saccos na vile vya Ushirika kuandaa safari za kujifunza kwa Wanachama wao mbinu mbali mbali za ukulima, ufugaji na uvuvi”. Alisema Balozi Seif.
Balozi Seif  alitoa nasaha kwamba ipo faida kubwa itakayopatikana  kwa jamii kutembelea Maonyesho hayo ya Kilimo hasa vijana kwa vile safari yao itawapa fursa ya kuanza kufikiria muelekeo wa kukabiliana na maisha yao ya baadae baada ya kumaliza masomo yao wakielewa kuwa nafasi za ajira ndani ya Serikali Kuu kwa wakati huu ni finyu.
Alisema ili Maonyesho hayo ya Wakulima Nane - Nane yaendelee kuwa kivutio kwa Vijana, waandaaji wanapaswa kufikiria kuwa na Vikombe vya Wakulima bora Vijana wa Kike na Kiume sambamba na uanzishwaji wa mashindano kilimo cha maua ili kuwashawishi Vijana kujiingiza kwenye Sekta hiyo Muhimu ambayo inaendelea kuwa Uti wa Mgongo wa Taifa.
“ Kilimo bado kinaendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa letu, na ndicho kinacho tuhakikishia uhakika wa chakula kwa kila mmoja wetu”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliiagiza Wizara ya Kilimo, Malisili, Mifugo na Uvuvi pamoja na Halmashauri za Wilaya na Manispaa kuongeza nguvu za kusimamia uzalishaji wa chakula Nchini kwa kuwa karibu zaidi na Wakulima, Wafugaji na Wavuvi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewapongeza Wananchi hasa Wakulima wa Mkoa wa Kusini Unguja kwa juhudi zao za kujifunza Taaluma ya Kilimo iliyopelekea kuwawezesha kuzalisha mazao mbali mbali na kujipatia mapato makubwa.
Balozi Seif alisema ukanda wa Kusini hasa Makunduchi ulizoeleka Wakaazi wake kushindwa  kuendeleza kilimo kutokana na  sababu mbali mbali ikiwemo mazingira ya Ukame wa Ardhi yake.
Alisema  hali iliwapelekea Wananchi hao kuagiza vyakula matika masoko ya mjini, lakini kutokana na jitihada hizo, ukanda huo umebadilika na hivi sasa Wananchi wake wamekuwa wazalishaji wakubwa wa mazao ya Ndizi na kupeleka Marikiti Kuu kwa mauzo.
Akielezea masikitiko yake kutokana na baadhi ya watu kuharibu mazingira kwa kukata miti ya Mikarafuu Kisiwani Pemba hivi karibuni, Balozi Seif aliliagiza Jeshi la Polisi Kisiwani humo kuendelea na uchunguzi wa wahusika hao na wale waliokwisha patikana ni vyema sheria ichukuwe mkondo wake.
Alisema hicho ni kitendo kisichokubalika kwa vile kinahatarisha Uhai wa Kisiwa  cha Pemba na dalili za uchafuzi huo umeanza kujitokeza kwa baadhi ya maeneo mengi ya Kisiwa hicho kutokana  na maji ya Bahari kuendelea kuvamia Makaazi ya Watu pamoja na maeneo ya Kilimo.
Akitoa Taarifa ya juu ya Maonyesho ya Siku ya Wakulima Nane – Nane, 2018 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar Ndugu Ahmad Kassim Haji alisema sekta ya Kilimo ina fursa nyingi za kutoa ajira endapo Wakulima watajielekeza katika uzalishaji wa kiwango kwa mujibu wa mfumo wa Kisasa.
Nd. Ahmad alisema Maonyesho ya Siku ya Nane Nane Zanzibar  ni agizo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika azma ya kuwapa fursa Wakulima Nchini kuonyesha Maendeleo yao pamoja na upatikanaji wa Taaluma kupitia Sekta hiyo muhimu.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar alifahamisha kwamba maonyesho hayo yaliyokisiwa kugharimu jumla ya shilingi Milioni 150 kwa ujenzi wa Miundombinu, Majengo pamoja na huduma za Maji yameshirikisha Taasisi 83 za Serikali na Jumuiya za Kiraia za Unguja na Pemba.
Akimkaribisha mgeni rasmi kuyafungua Maonyesho hayo Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar Mheshimiwa Rashid Ali Juma alisema  Maonyesho ya Kilimo Zanzibar hivi sasa yataendelea kuwa ya kudumu na  kifanyika ndani ya Wiki ya Nane Nane.
Mheshimiwa Rashid alisema Siku ya Nane - Nane  kwa sasa ni fursa nzuri kwa Wakulima pamoja na Wananchi kujifunza mbinu bora za Kilimo kupitia Maonyesho hayo ambapo kipindi kilichopita ilikuwa ni siku ya Mapumziko.
Waziri wa Kilimo alifahamisha kwamba maandalizi ya Maonyesho ya Nane Nane yalifanikiwa kwa ushirikiano mkubwa wa Watendaji wa Wizara ya Kilimo kwa kupata msukumo kutoka kwa wadau wa Sekta hiyo kutoka Taasisi za Umma pamoja na Jumuiya za Kiraia.
Ujumbe wa Siku ya Wakulima Nane Nane Mwaka huu unaeleza kwamba “ Wekeza katika Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa Maendeleo ya Viwanda”.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.