Habari za Punde


RISALA YA MWENYEKITI WA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI MHE. JAJI (R) SEMISTOCLES S. KAIJAGE KUHUSU UPIGAJI KURA KATIKA UCHAGUZI MDOGO WA UBUNGE KATIKA JIMBO LA BUYUNGU NA UDIWANI KATIKA KATA THELATHINI NA SITA (36) TANZANIA BARA
TAREHE 12 AGOSTI, 2018

Ndugu Wananchi;
Awali ya yote, kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi nachukua fursa hii kuvipongeza Vyama vya Siasa vilivyojitokeza kushiriki uchaguzi huu mdogo kwa kuwadhamini Wagombea waliochukuwa fomu na hatimaye kuteuliwa kuwania nafasi hizo zilizo wazi za Ubunge na Udiwani.
Nitumie nafasi hii pia kuwapongeza wananchi wote katika Jimbo la Buyungu na Kata Thelathini na Sita (36) zinazohusika na uchaguzi huu, kwa utulivu mliouonyesha wakati wote wa kipindi cha Kampeni. 
Ndugu Wananchi;
Kesho Jumapili tarehe 12 Agosti, 2018, ni Siku ya kupiga kura katika Uchaguzi Mdogo wa Ubunge wa Jimbo la Buyungu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Mkoani Kigoma.  Vile vile, Uchaguzi mdogo wa Madiwani katika Kata Thelathini na Sita (36) zilizopo katika Halmashauri 29, za mikoa 19, ya Tanzania Bara. Uchaguzi huu Mdogo wa Ubunge na Udiwani Tanzania Bara, utahusisha jumla ya Wapiga Kura 485,203 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kutakuwa na Vituo vya Kupigia Kura 1,314.
Ndugu Wananchi;
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inapenda kutumia nafasi hii kuwakumbusha wapiga kura wa Jimbo la Buyungu na kata zote zitakazoshiriki Uchaguzi huu kuzingatia mambo muhimu yafuatayo:-
i)            Mosi, Upigaji kura utafanyika katika vituo vile vile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na vitafunguliwa saa moja kamili (1:00) asubuhi na kufungwa saa kumi kamili (10:00) jioni.  Iwapo, wakati wa kufunga kituo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao wamefika kabla ya saa kumi jioni na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura.  Mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya saa kumi kamili (10:00) jioni.
ii)         Pili, watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale tu ambao wamo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye Jimbo au Kata husika na wana kadi ya mpiga kura. Hata hivyo, Tume kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 61(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, pamoja na kifungu cha 62(1) cha Sheria  ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, imeruhusu wapiga kura ambao ama kwa bahati mbaya wamepoteza kadi zao za kupigia kura au zimeharibika au zimechakaa watumie mojawapo ya vitambulisho vifuatavyo; wanaweza kutumia Pasi ya Kusafiria, Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

iii)      Tatu, mpiga kura aliyepoteza kadi yake ya kupigia kura au kadi hiyo kuharibika au kuchakaa ataweza kuruhusiwa kutumia Vitambulisho hivyo mbadala, iwapo tu; atakuwa aliandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mwaka 2015, jina lake liwe katika orodha ya Wapiga Kura katika kituo anachokwenda kupiga Kura na majina yake yaliyopo katika Daftari la Mpiga Kura yafanane kwa herufi, maneno na tarakimu na majina yaliyopo katika kitambulisho mbadala.
iv)       Nne, katika zoezi la upigaji kura, na kwa kadri itakavyowezekana kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali, wanawake wajawazito au wenye watoto wachanga, na wazee.
v)          Tano, mpiga Kura mwenye ulemavu wa kutoona, ataruhusiwa kwenda kituoni na mtu atakayemchagua mwenyewe kwa ajili ya kumsaidia  kupiga kura yake.
vi)       Sita, ni wajibu wa Vyama vya Siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi kuweka Mawakala katika vituo vyote vya Kupigia na Kujumlishia Kura kwa utaratibu ambao tulikubaliana wakati wa Mkutano wa Tume na Vyama vya Siasa tarehe 10/07/2018 uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam, na nakala ya utaratibu huo kutumwa kwa Wasimamizi wa Uchaguzi.

vii)    Saba, mawakala hao wanaruhusiwa kuwepo katika Vituo vya Kupigia Kura na wanatakiwa kufuata na kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu zinazoongoza Uchaguzi katika kipindi chote cha kupiga, kuhesabu na kujumlisha kura na kutangaza matokeo.
 Ndugu Wananchi;
Pamoja na kuwakumbusha mambo machache yanayopaswa kufanywa na kufuatwa siku ya Uchaguzi, Tume pia inapenda kusisitiza mambo yafuatayo:-
Kwanza, mwisho wa mikutano ya kampeni ni leo saa kumi na mbili kamili (12:00) jioni. Baada ya muda huo, Vyama, wagombea na mashabiki wasifanye kampeni za aina yoyote, kama vile kutumia alama za Vyama zinazoashiria kampeni, vipeperushi, bendera, mavazi n.k kwa kuwa kesho ni siku ya Uchaguzi.  Aidha, wananchi waheshimu Sheria za Nchi wakati wote wa upigaji, kuhesabu, kujumlisha kura na kutangaza matokeo.
Pili, pale panapokuwa na malalamiko yoyote ya ukiukwaji wa Sheria na Taratibu za Uchaguzi, malalamiko hayo yafikishwe kwenye mamlaka inayohusika kwa utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa Sheria. Vivyo hivyo, Viongozi wa Vyama vya Siasa, Wagombea au wafuasi wao na wananchi kwa ujumla wajiepushe na vitendo vinavyoweza kusababisha fujo au vurugu katika vituo vya Kupigia, Kuhesabia na Kujumlishia Kura.
Tatu, kwa kuzingatia tafsiri sahihi ya Kifungu cha 104 (1) kikisomwa pamoja na Kifungu cha 72(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania kwenye Shauri la Madai Anuai (Misc. Civil Cause No. 37 la mwaka 2015) mpiga kura anatakiwa kuondoka kituoni na kwenye maeneo ya kituo cha kupigia kura mara baada ya kupiga kura yake. Aidha, mbali ya wale ambao Sheria za Uchaguzi zinawaruhusu kuingia na kuwepo kwenye Vituo vya kupigia kura, wananchi wanatakiwa kujiepusha na mikusanyiko au mikutano katika maeneo ya Vituo vya kupigia kura. Vyama vya Siasa vimeweka mawakala vituoni ambao watalinda maslahi ya vyama husika na wagombea wao.
Nne, wanaoruhusiwa kuingia kwenye Vituo vya kupigia, kuhesabia na kujumlishia kura ni wale tu walioainishwa kwenye kifungu cha 72(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na kifungu cha 63(2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Tano, Vyama vya Siasa, Wagombea, Wananchi na Watendaji wa Uchaguzi kwa ujumla wanakumbushwa kuzingatia na kuheshimu matakwa na masharti ya Sheria za Uchaguzi, Sheria za Nchi na Maadili ya Uchaguzi wakati wa Upigaji Kura, Kuhesabu, Kujumlisha hesabu za Kura, na Kutangaza matokeo.
Ndugu Wananchi;
Kwa kumalizia, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inawasihi tena Wapiga Kura wote waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na wanaoishi kwenye maeneo yanayofanya Uchaguzi Mdogo, kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuwachagua Viongozi wanaowataka wawaongoze kwa kipindi cha takribani miaka miwili ijayo.  Wananchi wafanye na kutekeleza zoezi la kuwachagua wawakilishi wao bila hofu, woga, wasiwasi au ushawishi kwani chini ya Kanuni ya 3.1 (b) ya Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015, Serikali imepewa wajibu wa kuhakikisha kuwa kuna hali ya usalama, amani na utulivu katika kipindi chote cha Uchaguzi.
Ni matumaini ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa, hali ya Amani na Utulivu kwenye maeneo ya Uchaguzi ambayo imekuwepo hadi hivi sasa, itaendelea kudumishwa ili kuhakikisha Uchaguzi huu mdogo unafanyika na kumalizika salama kwa Ustawi wa Taifa letu.
Aidha, kila Mwananchi, Vyama vya Siasa na wadau wote wa uchaguzi tushirikiane, ili kuhakikisha kuwa viashiria vya kuvunjika kwa amani na utulivu vinaepukwa ili uchaguzi utakaofanyika uwe huru, wazi na wa haki.


KUMBUKA, KUPIGA KURA NI HAKI YAKO YA MSINGI
KWA MUSTAKABALI WAKO NA WA NCHI YAKO,
NENDA UKAPIGE KURA.
MUNGU IBARIKI TANZANIA.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.