Habari za Punde

SMZ Kujenga Jengo la Mahakama Kuu Lenye Ghorafa Tisa Zanzibar.


Na. Abdi Shamna.
WIZARA ya Nchi (OR), Katiba, Sheria na Utawala Bora, imesema imeanza mchakato wa ujenzi wa jengo la Mahakama kuu Zanzibar, unaotarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2020.
Ramani na michoro ya Ujenzi wa jengo hilo la Ghorofa tisa, utakaofanyika katika eneo la Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja, umeanza chini ya Kampuni ya Landmark Consultants Limited ya Zanzibar.
Akizungumza na vyombo vya habari, Waziri wa Wizara hiyo, Haroun Ali Suleiman (bila ya kutaja gharama halisi za ujenzi huo), alisema hatua hiyo ya Serikali inalenga kuleta ufanisi katika suala zima la upatikanaji wa haki, kuimarisha huduma za kisheria pamoja na kutoa fursa kwa vijana wengi zaidi.
Alisema katika hatau za awali, tayari Serikali imetenga kiais cha Shilingi Bilioni tano kwa ajili ya matayarisho ya ujenzi huo, ambapo miongoni mwa fedha hizo zitakazotumika kwa usafishaji wa eneo, michoro na mambo mengineyo.
Alisema Wizara yake itahakikisha inasimamia vyema agizo la Serikali la kufanikisha ujenzi huo, ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Aidha, Waziri Haroun alitowa wito kwa mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar kuwa program maalum ya kusomesha vijana wengi zaidi katika fani ya sheria ili waweze kwenda sambamba na mahitaji ya kuwepo kwa jengo hilo.
Mapema Mkurugenzi wa Landmark consultants Ltd ,Ali Mbarouk Juma alisema jengo hilo la kisasa litakalojengwa ndani ya eneo la hekta nne,  litakidhi mahitaji yote muhimu na kuendana na maadili ya kisheria.
Alisema katika eneo hilo pia kutakuwa na msikiti, Jengo la Jenereta, maegesho ya magari, sambamba na eneo lililotengwa kwa ajiili ya ujenzi wa “law school”.
Alisema eneo la chini ya jengo hilo limeandaliwa maalum kwa ajili ya maktaba na uhifadhi wa vielelezo, hususan vile ambavyo kesi zake zitachukuwa muda mrefu kumalizika.
Aidha, alisema ndani ya ene hilo zitapatikana huduma za kibenki, ili kuwawezesha  wenye mahitaji ya kulipia huduma za kisheria kuondokana na usumbufu wa kufuata huduma hiyo mjini au maneo mengine ya mbali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.