Habari za Punde

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


NAMUNGO FC KUPAMBANA NA SIMBA YA JIJINI DSM
*Ni katika uzinduzi wa uwanja wa Halmashauri ya Ruangwa

HALMASHAURI ya Wilaya ya Ruangwa kesho (Jumamosi, Agosti, 11, 2018) inatarajia kuzindua uwanja wake wa michezo, ambapo timu ya wilaya hiyo Namungo FC inayoshiriki ligi daraja la kwanza itapambana na bingwa wa ligi kuu 2018/2019 Simba SC ya jiji Dar es Salaam.

Timu hiyo ya Namungo FC ambayo inamilikiwa na wachimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la Namungo wilayani Ruangwa ilianza 2009 kamasehemu ya mazoezi kwa wachimbaji hao mara wanapotoka kazini, imeupa heshima mkoa wa Lindi kwa kuwa ndiyo pekee inayoshiriki ligi daraja la kwanza. 
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa uwanja huo leo (Ijumaa, Agosti, 10, 2018) Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mbali na timu ya Simba pia timu hiyo inatarajia kucheza na timu za Yanga , Azam za jijini Dar es Salaam na Dodoma FC ya jijini Dodoma.
Uwanja wa mpira wa miguu wa wilaya Ruangwa unaoitwa Majaliwa Stadium umejengwa katika kitongoji cha Mtichi kata ya Nachingwea na ndio utakaokuwa unatumiwa na timu ya Namungo FC kuchezea mechi za nyumbani.  
 “Lazima tuisapoti timu yetu ya Namungo FC icheze daraja la kwanza kwa mafanikio makubwa, hivyo ni vema tukashirikiana kuhakikisha timu hiyo inafanikiwa ili ndoto ya kucheza ligi kuu itimie.”
Kadhalika Waziri Mkuu amesema ni muhimu kwa timu ya Namungo FC kucheza na timu kama za Simba, Yanga, Azam na Dodoma FC kwa sababu zinasaidia katika kuimarisha viwango vya wachezaji na kuwaondolea uoga wa kupambana na timu nyingine.
Kiingilio katika mechi ya Namungo FC na Simba SC ni sh. 3000. Tayari timu ya Simba imeshawasili wilayani Ruangwa leo (Ijumaa, Agosti, 10, 2018), saa 11.01 jioni kwa ajili ya mechi yake na timu ya Namungo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, AGOSTI 9, 2018.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.