Habari za Punde

Taasisi za fedha zatakiwa kutoa mikopo nafuu kwa vikundi vya wajasiriamali

Na Mwashungi Tahir       Maelezo 

WAZIRI  wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Dr Sira Ubwa Mamboya amezitaka taasisi za fedha kutoa mikopo nafuu kwa vikundi vya wajasiriamali nchini ili waweze kuwasaidia kujiinua kiuchumi  na kujipatia kipato.

Hayo aliyasema  huko kizimbani kwenye maonyesho ya sherehe za wakulima  nane nane wakati alipokuwa akifunga maonesho hayo  ambayo yalianza wiki moja nyuma na leo kufikia kilele chake kwa mwaka huu.

Alivitaka vikundi vya  wajasiriamali , vyama vya ushirika na wazalishaji kuzitumia fursa hizo kwa kujipatia mikopo  iliyokuwa nafuu ili waweze kujiendeleza katika vikundi vyao na kuweza kujikwamua kwenye umasikini kwa kuweka bidhaa zilizo bora.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeandaa  maonyesho haya kitaifa kwa lengo la kumkomboa mkulima kutoka kwenye kilimo kilichokuwa duni na kumsogeza kwenye kilimo cha kisasa na kuwa na kipato cha juu ili aweze kuondokana na umasikini.

Aidha alisema wajasiriamali waliopo nchini wanahitaji elimu ya kutosha ili waweze kukuza soko kwa bidhaa zao kuwa na ushindani mkubwa katika harakati za kilimo ukizingatia wajasiriamali wengi wako chini kielimu na kifedha.
“Elimu bado iko chini kwa wajasiriamali wengi hivyo amewaomba wapate elimu ya kutosha ili wapate kukuza soko lao kwani elimu haimtupi mtu  na elimu ndio inayomkomboa mtu kimaisha”. Alisema Waziri huyo.
Akitoa wito kwa vijana na kuwataka kuzitumia fursa walizozipata kwenye maonesho hayo ya wakulima kwa kuendeleza kilimo na kuweza kujiajiri wenyewe na kuacha kusubiri ajira Serikalini.

Nae Waziri wa kilimo , Maliasili, Mifugo na Uvuvi  Rashid Ali Juma alisema kupitia  maonesho  hayo wakulima waliweza kupata fursa za kushiriki na kutoa huduma  na mbinu bora za kukiendeleza kilimo cha biashara ambacho kitamsaidia mkulima katika kujiajiri na kujiongezea kipato.
Pia alisema kwa kiasi kikubwa maonyesho ya nane nane yaliweza kuleta mvuto kwa wakulima hasa ukizingatia hii ni mara ya kwanza kufanyika hapa Zanzibar na kauli mbiu ya mwaka huu wekeza kwenye kilimo mifugo uvuvi kwa maendeleo ya viwanda.
Aidha alisema maonesho hayo yameweza kuongeza ari kwa wakulima katika kukuza na kuendeleza shughuli za kilimo kwa faida yao na Taifa kwa ujumla , kupatikana fursa adhimu ya kukutana na kutoa huduma kwa wajasiriamali ambao ni muhimu katika kuendeleza kilimo hapa nchini.
Sambamba na hayo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo , Maliasili, Mifugo na Uvuvi Dr Islam Seif alisema asilimia kubwa wanategemea sekta ya kilimo  kwa kuwa ndio inayotoa fursa nyingi za ajira mjini na vijijini  na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na kuleta mabadiliko ya kiuchumi.
Hata hivyo wakulima waliweza kuona  na kujifunza mbinu na zana zilizotumika katika uzalishaji , uhifadhi  na udhibiti wa bidhaa kwa jumla .
Maonyesho hayo yamegharimu jumla ya mia moja na hamsini milioni  TSH 150,000,000 ambazo zimetumika katika ujenzi wa miundombinu , mabanda, maji , umeme, ulinzi na usalama na afya na wadau 83 wameshiriki kutoka Serikalini na binafsi.

IMETOLEWAM NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.