Habari za Punde

CHINA KUTOA DOLA BIL. 60 KWA MAENDELEO YA AFRIKA



RAIS wa China, Xi Jinpingamesema China itatoa jumla ya dola bilioni 60 za Marekani kwenye mpango wake wa miaka mitatu ya ushirikiano na Afrika katika shughuli za maendeleo.

Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Septemba 03 ,2018) wakati akifungua Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaofanyika jijini Beijing nchini China.

Rais Jinping ameahidi kuwa nchi yake itatoa ushirikiano ili kuhakikisha kwamba amani ya kudumu inapatikana Barani Afrika, hatua ambayo ni muhimu kwa ustawi wa nchi za Afrika.

Maeneo mengine ambayo Rais huyo ameahidi kuwa China italisaidia Bara la Afrika ni pamoja na ujenzi wa miundombinu, ushirikiano katika sekta ya biashara  na huduma za afya.

Kadhalika, Rais Jinping amesema China itatoa nafasi za mafunzo ya kilimo bora na mafunzo ya ufundi kwa watalaam kutoka nchi za  Afrika ili kuchangia katika maendeleo ya uchumi. 

Amesema hivi sasa anaamini kwamba China na nchi za Bara la Afrika wako karibu zaidi na wanashirikiana vizuri sana katika shughuli za kimaendeleo ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Mkutano huo  ulianza kwa sherehe ya ukaribisho na baadae viongozi  kutoka nchi mbalimbali barani Afrika na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antyonio Geterres walipata fursa ya kupiga picha ya pamoja na mwenyeji wao Rais wa China. 

Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa ambaye anamuwakilisha Rais Dkt. John Magufuli katika mkutano huo alisalimiana na Rais Jinping baada ya ufunguzi. Mkutano huo utaendelea kesho ambapo viongozi wengi kutoka Bara la Afrika watapata nafasi ya kuzungumza.


 (mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, SEPTEMBA 03, 2018.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.