NA ABDI SHAMNAH
Jamii yakumbushwa
umuhimu wa kusoma vitabu
L Huduma za maktaba zina mchango mkubwa
kitaaluma
ILIKUWA ni asubuhi
tulivu, jua likiwaka bila kuathiri shughuli za kibinadamu, huku pepo mwanana za
bahari zikivuma na kupunguza makali ya
joto, ambalo yumkini tayari limeanza kuvinyemelea visiwa vya Zanzibar.
Shamra shamra, chereko chereko, nderemo na hoi hoi
zilihanikiza katika viunga vya Ofisi za Shirika la Hudma Maktaba, ziliopo
Maisara, kuashiria kuna jambo kubwa linalojiri.
Hakika ilikuwa ni tukio la kihistoria, ni muendelezo wa
matukio yanayojiri takriban kila mwaka, kwani kilichofanyika viwanjani hapo
kililenga kumuelekeza, kumfahamisha na kumtanabahisha Mzanzibari, juu ya umuhimu
wa kutumia huduma za maktaba.
KUANZISHWA HUDUMA ZA
MAKTABA ZANZIBAR
Mnamo miaka ya 1980, Huduma za Maktaba zilianzishwa rasmi
hapa Zanzibar, na ilipofika mwaka 1993 Baraza la Wawakilishi likapitisha Sheria
Nam.7 ya 1983 uanzishaji wa Bodi ya Huduma za Maktaba (ZLSB).
Aidha, mnamo mwaka 2009, huduma hizo ambapo kabla zilikuwa
katika Jengo Serena, Shangani mjini hapa,
zikahamishiwa katika jengo jipya na la kisasa Zaidi liliopo Maisara.
Lengo likiwa ni kuwa na taasisi inayotowa huduma bora za
kimaktaba mijini na vijijini , ili wanafunzi wa nagzi zote pamoja na jamii kwa
ujumla , ipate huduma hizo na kujifunza bila malipo, ili hatimae kuwa na kizazi kilichoelimika.
Katika makala hii, mwandishi anangalia vipi Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, kupitia Shirika la Huduma za Maktaba lilivyoungana na
jumuiya ya kimataifa, kuadhimisha siku hii
muhimu na adhimu kwa lengo la
kuhakikisha jamii ya Wazanzibari inahamasika katika matumizi bora ya huduma za
maktaba.
YALIYOJIRI KATIKA
MAADHIMISHO
Maadhimisho yam waka huu yalitanguliwa na maandamo
yaliyoongozwa na watoto wanaotumia huduma za maktaba, wakiwa na mabango yenye kaulimbiu
inayosomeka ‘kusoma na kuendeleza
ujuzi’.
Aidha, yalipambwa kwa aina tofauti za maonyesho,
ikiwemo yale ya vitabu , usomaji wa tenzi,
nyimbo na onyesho maalum la ‘English-Debate’,
ambapo kundi moja la wanafunzi kwa mtazamo wao wanahisi lililo bora kwao katika matumizi ya vita bu ni
kurudufu nakala za vitabu (kutowa kopi), huku kundi jingine likisisitiza
umuhimu wa kununua vitabu, kama njia sahihi ya kufikia azma ya kujifunza.
Hata hivyo, kupitia onyesho hilo lililoendeshwa kwa lugha ya
kiingereza, ufumbuzi sahihi ukafikiwa kuwa njia ilio bora ni ‘kwenda
maktaba pekee, mahala ambapo huduma za vitabu, majarida, magazeti na machapisho
mengine hupatikana na mtu kujisomea bila malipo’.
Suluhisho hilo likabainishwa kwa hoja, kuwa utaratibu wa kutowa kopi nakala za vitabu una changamoto
zake, ikiwemo Haki miliki ya muandishi, jambo ambalo lapaswa kufanyika kwa
ridhaa ya muandishi. Lakini pia hoja ya
kununua vitabu vipya, nayo ikabainishwa changamoto zake ikiwemo ya kuwa na
uwezo wa kutosha kwa maana ya fedha nyingi, kwa kuzingatiwa muhusika atakuwa na mahitaji ya vitabu zaidi
ya kimoja.
Kuambatana na onyesho hilo ufafanuzi ukatolewa kuwa Huduma za
Maktaba hutolewa bure kituo hapo, ambapo kimsingi kinachohitajika ni
kujisajili.
Imeelezwa kuwa kwa mwanafunzi wa skuli ya msingi itamlazimu
kulipia shilingi 1,000/-, mwanafunzi wa Sekondari shilingi 3,000/- na kwa wale
walioko Vyuo vikuu wanahitajika kulipia shilingi
5,000, ambapo fursa kubwa watakayoipata ni pamoja na kujisomea vitabu hivyo
nyumbani.
NASAHA ZA WADAU
Sichana Haji Foum ni Mkurugenzi wa Shirika la Huduma za
Maktaba Zanzibar, anasema mkusanyiko huo unalenga kuwakutanisha wadau na
kuwahamasiha umuhimu wa kupenda kusoma na kuandika.
Anabainisha kuwa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja
wa Mataifa (UNESCO) mnamo mwaka 1965 lilibaini kuwepo kwa tatizo kubwa la watu kutokujua
kusoma na kuandika, hivyo mnamo mwaka 1966 maadhimisho hayo yalianza.
Anasema lengo ni kutathmini mafanikio na changamoto
zinazoikabili jamii katika kufanikisha dhana ya kujua kusoma na kuandika.
Aidha anasema kwa vile
Shirika la Huduma za Maktaba Zanzibar ni wadau, hivyo kuna kila sababu za kujumuika na kuadhimisha
siku hiyo.
Kwa mnasaba huo, analitolea pongezi Shirika la Book Aid
International kutoka nchini Uingereza kwa misaada mbali mbali inayotowa kwa
shirika hilo, ikiwemo uaptkanji wa vitabu, ambavyo hatimae husambazwa skuli
mbali mbali Unguja na Pemba, ambapo nao huanzisha maktaba zao.
“Sio rahisi kwa wazazi kuwa na uwezo wa fedha za kutosha
kununua vitabu kwa ajili ya wanafunzi, hivyo wenzetu hawa wamekuwa wakiondowa
hiyo ‘gape’ iliopo kati wenye nacho na wasio nacho”, anasema.
Aidha, anasema ni jambo gumu kwa mwanafunzi au jamii kwa
ujumla kujifunza iwapo haiwezi kusoma, na kubainisha kuwa wale wanaosoma
wanakuwa katika nafasi nzuri ya kuendeleza ujuzi walionao.
“Iwe mwanafunzi, iwe mwalimu, iwe mkulima au jamii kwa jumla,
shughuli zako utazifanya kwa ufanisi”, anaongeza.
Mkurugenzi Sichana akawakumbusha wadau, jinsi kitabu
kitakatifu cha Qoraan kilivyokuja na kuhimiza umuhimu wa suala la kusoma, ikiwa
ni njia ya kupanuwa wigo wa ufahamu kwa binadamu.
Akatowa wito kwa wadau wote kuishajiisha jamii kujenga
utamaduni wa kupenda kusoma na kuandika, sambamba na kuzitumia kikamilikfu
huduma za maktaba ili kujiongezea maarifa.
Nae, Mwalimu Ali mwalimu, Katibu wa Jumuiya ya Waandishi wa
Vitabu Zanzibar, akabainisha shughuli zinazofanywa na jumuiya hiyo, kuwa ni
pamoja na kuihamasisha jamii ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla, umuhimu
wa kusoma vitabu.
Anasema chanzo cha kuanzishwa Jumuiya hiyo kuliotokana na changamoto
iliyokuwepo ya wananchi kutokuwa na utamaduni wa kupenda kusoma vitabu, hivyo
kuundwa kwake kulilenga kumuamsha Mzanzibari
juu ya umuhimu wa jambo hilo.
Anasema, “kuanzia hapo tulianza kufanya juhudi za kuandika na
ndio leo hii unakuta kuna vitavu vingi vilivyoandikwa na Wazanzibari”.
“Hivi sasa kuna umuhimu kwa wadau kukaa na kutafakari, kwani
hali ya usomaji wa vitabu haiko vyema, hakuna utamaduni wa kusoma vitabu’,
anasema.
Amewataka wadau walioshiriki katika maadhimisho hayo
kutumia
fursa hiyo kuishajiisha jamii kujenga utamaduni wa kusoma vitabu, akibainisha
jinsi Jumuiya yake, ilivyojidhatiti katika jambo hilo, kwani ina kipindi maalum
kupitia Shirika la Utangazaji Zanzibar( ZBC TV).
Anaedelea kuitanabahisha jamii kuwa suala la matumizi yaa
huduma za mkataba, hayapo kwa ajili ya wanaafunzi pekee, bali ni kwa ajili ya
watu wote.
Aidha, anashauri kuziunga mkono na kuziimarisha maktaba za
skuli, kwa kigezo kuwa haziko vyema na zinakabiliwa na chanagmoto kadhaa,
ikiwemo ukosefu wa vitabu, sambamba na maktaba za Wilaya ambazo bado
hazijaanzishwa.
“Kuna maktaba za wananchi, ni mfano ule ule utakuta kwenye
majumba yetu, mtu kaweka ‘shockest’ lake ukumbini, kuna vitu kadhaa vya
thamani……..vikombe, visahani na vingine kadha wa kadha, lakini huwezi kukuta
vitabu………”, anaonyesha mshangao.
Anasema kuna haja kwa skuli kuanzisha maktaba zao ili
wanafunzi watumie fursa ya kujifunza kikamilifu.
Nae, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Huduma za Maktaba
Fatma
Hassan Kingwaba, akaitanabahisha jamii juu ya thamani ya elimu na gharama
zinazowakabili wazazi katika kufanikisha azma ya kuwapatia elimu bora watoto
wao.
Anasema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kulifahamu hilo,
imelazimika kuanzisha miundombinu ya elimu, ikiwemo Shirika la Huduma za
Makatba, kwa lengo la kusaidia juhudi za wananchi/wazazi kuwapatia elimu
watoto.
“Ninaiomba jamii ithamini juhudi za Serikali za kuanzisha
huduma hizi za maktaba tofauti, ikiwemo za shule. Tujenge utamaduni wa kupenda
kusoma vitabu, kuna vitabu vimetungwa na watunzi wetu; vimezingatia lugha,
mila, silka na maadili yetu”, anafafanuwa.
Hudhaifa Haji ni Mkutubi katika Shirika la Huduma za Maktaba
Zanzibar, anasema huduma hizo zinapatika kwa watu wa aina zote, ikiwemo
wanafunzi wa skuli za msingi, sekondari, vyuo vikuu pamoja na wananchi
wengineo.
Anasema kuna utaratibu uliopangwa kwa watoto wanaosajiliwa
kujifunza katika siku za ijumaa, ambapo hupata fursa ya kufundishwa namna bora
ya kusoma, kuchora, kuimba pamoja na kushiriki michezo mbali mbali inayolenga kuimarisha
uwezo wao wa akili.
Anatowa wito kwa wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao
katika shirika hilo ili kupata mwanga na kuwa na msingi bora wa kielimu.
“Tunaiomba jamii ihamasike na kuwaleta watoto wao hapa,
angalau kwa siku ya Ijumaa, ili kuwafanya watoto wajenge utamaduni wa kupenda
kusoma na kuandika”, anasema
Hudhaifa.
Katibu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dk.
Muslih Hijja ambae alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo akimuwakilisha
Naibu Waziri wa Wizara hiyo. Anasema, kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la
UNESCO katika taarifa iliyotolewa mwaka 2016, inakadiriwa zaidi ya watu Milioni
775 hawajui kusoma wala kuandika Duniani kote.
Akinukuu takwimu za Shirika hilo anasema kila penye watu
wazima watano (5), basi kuna mtu mmoja ambae hajuwi kusoma na kuandika, ambapo
miongoni mwao, asilimia sitini na sita
(66%) ni wanawake.
“Hii inaonyesha kwa kiasi gani tatizo hilo lilivyo kubwa na
juhudi madhubuti zinazohitajika kuchukuliwa ili kupunguza au ikiwezekana kuliondosha
kabisa tatizo la kutojua kusoma na kuandika”, anasema.
Aidha, anasema maktaba
zina mchango mkubwa sana kwa jamii
katika kuhakikisha wananchi wanapata fursa za kusoma kupitia vitabu na
machapisho mengine kama vile magazeti, majarida na huduma za mitandao (internet).
Anasema kuna muhimu kwa Shirika hilo kuendelea kuihamasisha
jamii kuchangamkia fursa hizo, kwa kigezo kuwa kuna nafasi kubwa ya
kuwanyanyuwa kiuwezo katika nyanja za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni
na pia kwenda sambamba na maendeleo ya Ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia.
Anaeleza kuwa katika kuhakikisha wananchi wa Zanzibar
wanaweza kusoma na kuandika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafanyakazi kwa
karibu na wadau mbali mbali wa elimu ndani na nje ya nchi.
Akatumia fursa hiyo kulipongeza Shirika la ‘Book Aid International’
la Uingereza, kwa kuwa mstari wa mbele kusaidia juhudi za Zanzibar na Tanzania
kwa ujumla katika kupunguza tatizo la kutokujua kusoma na kuandika.
“Serikali yetu inapenda kulishukuru sana Shirikia hili kutokana
na jitihada zake ambazo leo hii sote ni mashahidi kwamba Shirika la Maktaba,
lililo chini ya Wizara Elimu na Mafunzo ya Amali limekuwa likipokea msaada wa
vitabu vipya na vizuri ambavyo husaidia kuendeleza maktaba za Jamii, skuli na
hata maktaba za Vyuo”, anasema.
Anasema hayo yanafanyika kwa lengo la kuyabadili maisha ya wananachi
, akiamini kuwa mtu asiyejuwa kusoma na kuandika ni sawa na yule anaeishi
gizani.
Dk. Muslih anasema kuna kila sababu ya Serikali kuwahimiza wananchi
wake kuongeza bidii katika kusoma pamoja na matumizi ya maktaba.
Akiziainisha sababu hizo, anasema ni pamoja na ukweli kuwa
kusoma ndio msingi mkuu katika mafanikio ya kielimu na katika maisha.
Anasema kusoma kunaongeza uwezo wa ubongo kufanya kazi, kama
ilivyo kwa wanaofanya mazoezi ambapo huongeza uwezo wao wa misuli.
Anasema pia kusoma kunaongeza ukwasi wa misamiati, “ kadri
unavyosoma vitabu vingi kutoka kwa waandishi mbali mbali, ndivyo unavyojitajirisha
katika suala la misamiati”.
Aidha, anasema hatua ya kuwa na misamiati mingi kunasaidia sana katika maisha
ya kila siku, kwani humfanya mtu kujiamini na kujenga uwezo mzuri wa kuzungumza
mbele ya hadhira.
“Kusoma kunaimarisha stadi za uandishi, waandishi mahiri ni
wale waliopata msukumo kutokana na usomaji wa kazi za waandishi wengine hususan
waliobobea”, anaeleza.
Katika hatua nyengine, anasema kusoma kunaongeza maarifa,
ambapo humpa mtu taarifa mpya, jambo linalomfanya mtu kuwa na utajiri wa
maarifa, ikiwa nyenzo muhimu katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza
maishani mwake.
Katibu Mkuu huyo, akatanabahinisha jinsi kusoma kunavyoweza
kuongeza uwezo wa kufikiria na kupambanuwa mambo, sambamba na kuleta burudani
isiyo na gharama.
“Ni kweli vitabu vingi vizuri huuzwa kwa bei ghali, lakini
usisahau kuwa unaweza kupata burudani ya karibu ya bure kupitia vitabu, kwa
kujenga mazoweya ya kutembelea maktaba katika eneo lako”, anabainisha.
Anaeleza kuwa Maktaba huwa na mchanganyiko wa vitabu vya kila
aina, kuanzia riwaya hadi taaluma mbali mbali.
Katika hatua nyengine Injinia huyo anatowa wito kwa wazazi,
walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha watoto wote waliofika umri wa kusoma
wanapatiwa fursa endelevu za kielimu ili kuondokana na tatizo sugu la kutojua
kusoma na kuandika kwa maslahi ya Taifa.
“Wazazi na walezi ni watu muhimu sana katika kuwasimamia
watoto kujua kusoma na kuandika, suala hili si la walimu peke yao, ila ni la
jamii nzima, tushirikiane pamoja ili tuweze kulipatia ufumbuzi wa kudumu”.
Dk. Muslih anabainisha njia za kufuatwa na wazazi pamoja na
walezi katika kumsaidia mtoto ili kumuwezesha kujua kusoma na kuandika, kuwa ni
pamoja na kusoma pamoja na watoto hao na kuwasikiliza wanaposoma, sambamba na kuweka
vitabu nyumbani.
Aidha, anawataka wazazi/walezi kufanya ushawishi kwa kuwapeleka watoto maktaba ili waweze
kusoma vitabu pamoja na kuchukuwa nyumbani kwa ajili ya kujisomea.
Anasema endapo kutakuwa aa usimamizi mzuri, bila shaka watoto
na jamii kwa ujumla itajenga utamaduni imara wa kupenda kusoma na kuongeza
ufaulu katika masomo yao, sambamba na kuwa na uwezo wa kuendeleza ujuzi katika
mambo mbali mbali.
Nidhahiri kuwa suala la kubadili mitizamo kwa wanafunzi na
jamii ya Wazanzibari kwa ujumla, hususan katika suala zima la kutumia huduma za
maktaba linahitajika.
Kuna ukweli kuwa bado jamii ya Wazanzibari haina utamaduni wa
kutumia huduma za maktaba, kwa kile kinachoonekana kutokuwepo utamaduni wa
kupenda kusoma na kuandika.
Hivyo ni wakati sasa kwa Wazanzibari kubadilika na kuhamishia
nguvu zao katika kujenga utamaduni wa kupenda
kusoma vitabu, ikizingatiwa kuna vipaji vingi vya waandishi mahiri wa vitabu,
hususan vya Kiswahili hapa nchini.
Wakati Wazanzibari wakiungana na Jumuiya za Kimataifa
kuadhimisha siku ya Kujua kusoma na kuandika, ni wakati pia wa kutafakari kwa
kiasi gani tunachukuwa hatua maridhawa katika kuwasaidia watoto na jamii kwa
ujumla kujua kusoma na kuandika.
No comments:
Post a Comment