Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Atembelea Karakana Kuu ya Serikali Chumbuni Zanzibar.

Kaimu Mkuu wa Karakana ya Serikali Ndugu Yussuf  Kulia Masururu akimkaguza sehemu mbali mbali balozi Seif kujionea hali halisi ya Mazingira ya Karakana hiyo.Wa kwanza kutoka Kushoto ni Naibu Waziri Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Mihayo Juma N’hunga.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kushoto akiangalia baadhi ya vitengo vya Karakana Kuu ya Serikali iliyopo Chumbuni alipofanya ziara ya ghafla kwenye Taasisi hiyo ya Uhandisi.Aliyepo Kulia ni Kaimu Mkuu wa Karakana ya Serikali Ndugu Yussuf  Masururu na nyuma ya Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Mh. Mohamed Ahmed Salum.
Kaimu Mkuu wa Karakana ya Serikali Ndugu Yussuf  Kulia Masururu akiendelea kutoa maelezo kwa Balozi Seif  kuhusu baadhi ya Mashine zinazofanya kazi kwenye Karakana hiyo.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameukumbusha Uongozi wa Karakana Kuu ya Serikali kuandaa mapendekezo yatakayotoa mwanga wa kuifufua Karakana hiyo ili itoe huduma imara zilizokusudiwa kutokana na uwepo wa azma ya kujengwa kwake.
Alisema mapendekezo hayo ambayo tayari alikwisha yaagiza kwa Uongozi huo kufuatia ziara yake aliyoifanya kwenye Karakana hiyo karibu Miaka Mitano iliyopita ni vyema yakaainisha vyema mpango Mkuu wa muda mfupi wa kati na mrefu.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kumbusho hilo wakati alipofanya ziara ya ghafla katika Karakana hiyo iliyopo Chumbuni kuangalia uhalisia  wa mazingira halisi ya uwajibikaji wa Watendaji wake na changamoto zinazowakabili katika utendaji wao wa kazi wa kila siku.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliamua kwa makusudi kuanzisha mradi huo wa Karakana ya Serikali ili kujaribu kusimamia huduma za matengenezo kwa Vyombo vya Moto kama Gari na Ringi Mbili vya Taasisi za Umma na hata zile binafsi.
Balozi Seif alieleza kwamba hatua hiyo ilikuwa na azma ya kuokoa fedha nyingi za Serikali zinazopotea kutokana na mfumo wa utengenezaji wa vyombo vyake kufanywa na Mkampuni au Watu Binafsi Mitaani.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  itafikiria kuchukua hatua stahiki za kuona Karaka hiyo inaendelea kutoa huduma kama kawaida baada ya kupata ufafanuzi wa kutosha wa ripoti au mapendekezo yatakayotolewa na Wahandisi hao.
“ Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliamua kuifufua Karakana  yake  ili Taasisi za Serikali ziache tabia ya vyombo vyao vya Moto kutengenezwa Vichochoroni mfumo unaoigharimu fedha nyingi Serikali Kuu”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wafanyakazi na Uongozi wa Karakana Kuu ya Serikali kwa jitihada zao za kufanya kazi katika mazingira magumu ya ukosefu wa baadhi ya zana muhimu za Kisasa za kutendea kazi.
Alisema Dunia ya sasa inaendelea kushuhudia Maendeleo makubwa ya Teknolojia Ulimwenguni yanayopaswa kwenda sambamba na uwajibikaji wa Watendaji wa Karakana hiyo.
Mapema  Balozi Seif  akikaguzwa sehemu mbali mbali za Karakana hiyo ambapo Kaimu Mkuu wa Karakana ya Serikali  Ndugu Yussuf  Masururu ameishauri Serikali wakati inapoagiza vyombo vya Moto kama Magari kuushauri Uongozi wa Karakana hiyo ili utoe baraka kwa vyombo vinavyostahiki kununuliwa kwa mujibu wa zana za matengenezo zilizopo.
Nd. Yussuf alisema zipo changamoto zinazowakuta Wahandisi wa Karakana hiyo hasa pale wanapopokea baadhi ya Magari ya Serikali ambayo vipuri vyake  kwa mujibu wa muundo wa Gari hizo huwa havipatikani Nchini jambo ambalo chombo hicho hubaki kuchakaa au matengenzo yake kuchuukuwa gharama kubwa endapo kifaa kinachohitajika italazimika kukiagiza nje ya nchi.
Kaimu Mkuu wa Karakana hiyo ya Serikali alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba utoaji wao wa huduma hivi sasa unategemea Wahandisi wa Karakana kuwasiliana na  muhusika wa Gari lililopelekekwa kufanyiwa matengenezo kulazimika kununua kwa Kampuni na Taasisi binafsi nje ya Karakana hiyo.
Hata hivyo ndugu Yussuf  alifahamisha kwamba zipo baadhi ya Mashine zinashindwa kufanya kazi kwa vile Wataalamu waliokuwa wakizihudumia kumaliza muda wao wa Utumishi nawengine  kufariki Dunia.
Akitoa shukrani zake Naibu Waziri Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Mh. Mohamed Ahmed Salum  alisema Wizara hiyo hivi sasa iko katika hatua za mwisho za kufanya upembuzi wa mapendekezo ya uimarishaji wa Karakana ya Serikali.
Mh. Mohamed alisema Wizara hiyo imekusudia kuweka mikakati itakayoweka misingi imara ya kuimarisha Karakana hiyo  ili gari zote za Serikali zirejee kupatiwa huduma za matengenezo kama kawaida.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.