Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Aondoka Nchini Leo Kuelekea Nchini China Kuhudhuria Maonesho ya 15 ya Biashara ya Kimataifa Katika Mji wa Guangxi Jimbo la Guangzhou.

 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Sief Ali Iddi akisalimiana na kuagana na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar , akielekea Nchini China kuhudhuria Maonesho ya Biashara ya 15 ya Kimataifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi wakiagana na Viongozi mbali mbali wa Serikali na Vyama vya Siasa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar akielekea China kuhudhuria Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara.Anayempa mkono niMwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini Ndugu Talib.
Balozi Seif ambae anatakiwa safari njema  na Naibu Waziri wake Mh. Mihayo Juma N’hunga  atapata wasaa wa kutoa salamu za Tanzania kwenye Maonyesho hayo akiwa kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania.Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimiwa Aayoub Mohamed Mahmoud akimtakiwa safari njema yenye mafanikio  Balozi Seif  hapo kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abaid Aman Karume.

Picha na –OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameondoka Zanzibar kupitia Mjini Dar es salaam kwa safari ya kikazi akiuongoza Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Maonyesho ya 15 ya Biashara ya Kimataifa yanayotarajiwa kufanyika katika Mji wa Guangxi Jimbo la Guangzhou Nchini China.
Maonyesho hayo ya China Asean Expo 2018 yakiwa miongoni mwa Maonyesho Makubwa Duniani kwa kuhudhuriwa na Washiriki wengi yanatarajiwa kuanza Tarehe 12 hadi 15 Septemba 2018 Tanzania ikipata fursa na kuwa Nchi pekee ya Afrika Mashariki kushiriki Maonyesho hayo.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyembatana na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi aliagwa na Viongozi mbali mbali wa Serikali, Vyama vya Kisiasa wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Majini Magharibi Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud.
Katika ziara hiyo ya kikazi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar anaambatana  na Waziri wa Fedha na Mipango Dr. Khalid Salum Mohamed, Waziri wa Biashara na Viwanda Balozi Amina Salum Ali na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed .
Viongozi wengine anaofuatanana nao ni Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar Nd. Juma Ali Juma, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale Bibi Khadija Bakar Juma, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambio ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Ramadhan Mwinyi Muombwa pamoja na Maafisa wengine Waandamizi wa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Tanzania imepata fursa na kuwa Nchi pekee ya Afrika Mashariki kualikwa rasmi kushiriki kikamilifu kwenye Maonyesho hayo ambayo tayari yameshafanyika kwa takriban Miaka 15 sasa tokea kuasisiwa kwake mnamo Mwezi Spetemba Mwaka 2003.
Tanzania kwa ujumla imepata fursa ya kutangaza sekta ya Utalii, Uchumi wa viumbe wa Baharini na Utamaduni wa Zanzibar ambayo itatoa nafasi kubwa ya kuvutia Wawekezaji wa Viwanda vya kuongeza thamani katika sekta ya viungo kama Karafuu, Mwani, Chumvi, Dagaa na kuendeleza Miundombinu ya Uchumi wa Zanzibar.
Wadau wa Maonyesho hayo watapata muda wa kushuhudia mambo ya Teknolojia, Mashine, Mitambo, Telnolojia ya Habari na Mawasiliano, Biashara za Viwanda na Teknolojia ya Kilimo na Viwanda yakiwa na fursa ya kutangaza Miradi ya Uwekezaji kwa lengo la kutafuta Wabia wa Kuwekeza.
Pamoja na Mambo mengine Washiriki wa Maonyesho hayo watajumuika pia katika Mikutano kwa Timu ya Tanzania kufanya mazungumzo ya kuvutia Wawekezaji, Kongamano la Biashara na Uwekezaji ili kutangaza fursa zilizopo Tanzania pamoja na kutangaza Miradi inayohitaji Wabia kuiendeleza.
Maonyesho hayo ya China Asean Expo 2018  yanaunganisha Mataifa ya Indonesia, Thailand, Vietnam, Singapore, Malaysia, Philippines, Myanmar, Cambodia, Laos, Brunei, na wenyeji China.
Zaidi ya Watu 800 kutoka Nchi  Mataifa  zaidi ya 50 Duniani hushiriki Maonyesho hayo ambapo pia hutembelewa na Wateja Wakubwa zaidi ya 300 na Wawekezaji wasiopungua 20,000.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.