Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) alipokuwa akizungumza na Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini Mhe.Jaji Frances Mutungi (katikati) alipofika kujitambulisha katika hafla iliyofanyika leo ukumbiwa Ikulu Mjini Zanzibar,(kushoto) Naibu Msajiliwa Vyama vya Siasa Tanzania Bw.Mohammed Ali Ahmed [Picha na Ikulu ]25/09/2018.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itaendelea kutoa mashirikiano kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania
ili Ofisi hiyo iweze kutekeleza vyema majukumu yake katika kuimarisha
demokrasia nchini
Dk. Shein aliyasema hayo
leo alipokuwa na mazungumzo na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania Mohammed
Ali Ahmed aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais
akiwa amefuatana na Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania Jaji Francis Mutungi.
Katika maelezo yake Rais
Dk. alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua umuhimu wa Ofisi
hiyo pamoja na uongozi wake kwa Taifa, hivyo kuna kila sababu ya kutoa ushirikiano
wake kwa lengo la kuimarisha demokrasia.
Dk. Shein alimpongeza
Naibu Msajili huyo wa Vyama vya siasa kwa kuteuliwa nafasi hiyo na kueleza
matumaini yake makubwa ya utendaji kazi wa kiongozi huyo.
Aidha, Rais Dk. Shein
alimuhakikishia kiongozi huyo kwamba kwa upande wa Zanzibar atapewa kila aina
ya msaada na mashirikiano ili aweze kufanikisha kazi zake vyema hasa
ikizingatiwa kuwa ofisi yake ipo hapa Zanzibar.
Nae Jaji Francis Mutungi
aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk.
Shein kwa mashirikiano makubwa inayoyapata Ofisi yake hatua ambayo imeweza kusaidia
kufanikisha vyema kazi za Ofisi hiyo.
Mapema Naibu Msajili wa
Vyama vya Siasa Mohammed Ali Ahmed alitoa shukurani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo ambao
aliahidi kuutumikia vyema.
Naibu Msajili huyo ameahidi
kutekeleza vyema majukumu yake ya kazi kwa kusimamia vyema sheria za vyama vya
siasa nchini huku akieleza kuwa atahakikisha anatekeleza ipasavyo sheria hizo
kwa lengo la kuwatumikia wananchi ili waweze kupata maendeleo sambamba na kuimarisha
amani, utulivu, umoja na mshikamano mkubwa uliopo nchini.
Rais Dk. John Magufuli
alimteua Mohammed Ali Ahmed tarehe 20 Juni 2018 ambapo kabla ya uteuzi huo
alikuwa Mwanasheria na mtafiti katika Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar
ambaye amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Rajab Baraka Juma ambaye amestaafu.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment