Mwenyekiti wa Mamlaka ya Uhifadhi Nyaraka na Kumbukumbu katika serikali ya Oman Dk. Hamed Mohammed Al Dhawaiyan (mwenye kanzu katikati), akikabidhi vifaa vya kisasa vya kutunzia nyaraka kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar Salum Suleiman Salum (kulia), nje ya jingo la ofisi hizo Kilimani mjini Unguja.
Mwenyekiti wa Mamlaka ya Uhifadhi Nyaraka na Kumbukumbu katika serikali ya Oman Dk. Hamed Mohammed Al Dhawaiyan (mwenye kanzu katikati), akikabidhi vifaa vya kisasa vya kutunzia nyaraka kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar Salum Suleiman Salum (kulia), nje ya jingo la ofisi hizo Kilimani mjini Unguja. (Picha na Salum Vuai, WHUMK).
Na Salum Vuai, ZANZIBAR
SERIKALI ya Oman imeanza
kutekeleza kwa vitendo makubaliano iliyofikia na Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, katika kusaidia teknolojia ya kisasa ya uhifadhi wa nyaraka.
Septemba 3, 2018, ujumbe wa
Idara ya Nyaraka na Kumbukumbu ya Mambo ya Kale kutoka nchi hiyo, umekabidhi
mashine za kisasa za kutunza nyaraka na kumbukumbu kwa mfumo wa kidijitali
kuzuia kuharibika.
Makabidhiano hayo yalifanyika
katika ofisi za taasisi ya Nyaraka na kumbukumbu Zanzibar zilizopo Kilimani
mjini Unguja.
Vifaa hivyo ni mashine ya
kurudufu nakala na nyengine kwa ajili ya kuhifadhia nyaraka kwa njia ya
kidijitali.
Mwenyekiti wa Mamlaka ya
Nyaraka na Kumbukumbu wa Oman Dk. Hamed Mohammed Al Dhawiyan ndiye aliyekabidhi
vifaa hivyo kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar, Salum
Suleiman Salum.
Akizungumza baada ya
kukabidhi mashine hizo, Dk. Al Dhawiyan,
alisema msaada huo wameutoa ikiwa ni sehemu ya makubaliano kati ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Oman, wakati wa ziara ya Waziri wa Habari,
Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo na ujumbe wake nchini Oman
mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu.
Alifahamisha kuwa, nyaraka za
nchi ni vitu muhimu ambavyo vinahitaji kushughulikiwa na kuthaminiwa, ili
zidumu kwa miaka mingi na kutumiwa kwa tafiti mbalimbali.
“Ni vyema jambo hili
lifanyiwe kazi kikamilifu kutokana na umuhimu wake kwa taifa, wananchi, wageni
na wasomi wanaohitaji kumbukumbu kwa ajili ya tafiti zao,” alieleza Mwenyekiti
huyo.
Alieleza kuwa, vifaa hivyo ni
hatua ya awali katika misaada wanayokusudia kuipatia Zanzibar, na kuongeza
kuwa, vyengine vitaendelea kuletwa.
Aidha, alisema katika ujumbe
wao uliowasili nchini Septemba 1 na 2, wamo wataalamu maalumu waliobobea katika
matumizi ya vifaa hivyo, ambao wamekuja kwa lengo la kutoa mafunzo kwa wafanyakazi
wa taasisi hiyo ya Zanzibar ili wapate maarifa ya kutumia mashine hizo.
Dk. Al Dhawiyan alifafanua
kwamba, ni fahari kwa Oman ambayo imepiga hatua kubwa ya maendeleo katika sekta
mbalimbali, kutoa mchango wake katika kuzisaidia nchi nyengine ili nazo zipate
mabadiliko na ufanisi wenye tija kiuchumi na kijamii.
Mbali na ujuzi wa kuhifadhi
nyaraka kisasa, pia alisema nchi yake ina ujuzi wa kuziharibu kitaalamu kumbukumbu zilizopitwa na wakati ambazo
hazihitajiki tena, na ziko nchi nyingi zikiwemo Urusi, Iran na Belarusia
zinazoomba kufanyiwa kazi hiyo.
Alieleza kuwa, katika
ulimwengu wa sasa, nyaraka zinakuwa siri kwa muda maalumu na baadae hutangazwa
ama kuwa huru kwa watu mbalimbali kuziona kwa shughuli zao, au kuwa
hazihitajiki tena.
Akizungumza katika hafla
hiyo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar Salum Suleiman
Salum, alibainisha changamoto kadhaa zinazowakabili, ikiwemo hali ya joto ambayo
baadhi ya nyaraka haziwezi kuihimili kwa muda mrefu.
Kutokana na sababu hiyo,
alisema nyingi kati ya nyaraka zilizopo zimeshaanza kupoteza hadhi na uhalisia
wake, kwa hivyo alishauri uwezekano wa Oman kuliangalia pia eneo hilo kwa
msaada stahiki.
Mbali na hayo, alisema kwa
sasa jengo lao limekuwa dogo kulingana na wingi wa shughuli na halikidhi
matumizi ya taasisi hiyo kwa sasa.
Alisema pamoja na kuwepo
uwezekano wa kulitanua, lakini ni vizuri zaidi kujenga jengo jipya, kubwa na la
kisasa litakalokuwa na mahitaji yote ya
msingi kwa shughuli za uhifadhi wa kumbukumbu, pamoja na mazingira rafiki kwa
watu wenye ulemavu.
IMETOLEWA NA WIZARA YA
HABARI, UTALII NA MAMBO YA KALE ZANZIBAR- SEPTEMBA 3, 2018
CAPTION
MWENYEKITI wa Mamlaka ya
Uhifadhi Nyaraka na Kumbukumbu katika serikali ya Oman Dk. Hamed Mohammed Al
Dhawaiyan (mwenye kanzu katikati), akikabidhi vifaa vya kisasa vya kutunzia
nyaraka kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Zanzibar Salum
Suleiman Salum (kulia), nje ya jingo la ofisi hizo Kilimani mjini Unguja.
(Picha na Salum Vuai, WHUMK).
No comments:
Post a Comment