Habari za Punde

Wahitimu mafunzo ya usalama wa anga watakiwa kufanya kazi kwa uadilifu

Na Mwashungi  Tahir  Maelezo- Zanzibar     
Wahitimu wa Mafunzo ya Usalama wa Anga wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu na kuepuka kurubuniwa na Wafanyabiashara wasioitakia mema Tanzania.
Wito huo umetolewa na Kanali Selenge Salum Mugoba  kutoka Brigedi ya Nyuki Zanzibar alipokuwa akitoa nasaha zake kwa Wahitimu wa mafunzo hayo katika Ukumbi wa Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Aman Abeid Karume.
Amesema Wahitimu hao wanafanya kazi nyeti inayohitaji uadilifu mkubwa ili kusiadia nchi kuepukana na matatizo mbalimbali yanayoweza kujitokea.
Kanali Serenge amefahamisha kuwa Wafanyabiashara wasio waaminifu huvitumia Viwanja vya ndege kama njia ya kupitisha bidhaa haramu ikiwemo madawa ya kulevya hivyo uaminifu wao utasaidia kupunguza tatizo hilo.
“Nawaomba mjiepushe na watu matapeli msikubali kurubuniwa na kupitisha vitu vilivyokuwa sio halali mtakuwa mumefanya kosa kubwa”. Alisema Kanali Serenge.
Ameongeza kuwa kuhitimu mafunzo hayo pia kutaongeza idadi ya Wataalamu wengi wenye uweledi katika kusimamia sekta ya Anga.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha usafiri wa anga Tanzania Aristid Kanje alisema lengo la mafunzo hayo ni kuongeza ufanisi na tija kwa Wafanyakazi katika majukumu yao.
Aidha amesema Mafunzo hayo pia yataboresha usalama katika viwanja vya ndege hali ambayo itachochea ukuaji wa uchumi nchini.
“Mtakapotoa huduma kwa kiwango cha hali ya juu mtasaidia kuchochea uchumi na kuvutia wageni mbalimbali wanaokuja nchini na kuufanya uchumi uende mbele” Alisema Mkuu wa Chuo
Jumla ya wanafunzi 50 wamehitimu mafunzo Usalama wa Anga na kukabidhiwa vyeti vyao .

Imetolewa na Idara ya Habari Maelezo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.