Habari za Punde

Zanzibar yathamini michango mikubwa ya kimaendeleo kutoka taifa la China

Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar                                      28.9.2018
Zanzibar imeeleza kuthamini michango mikubwa inayotolewa na Taifa la China katika kusaidia nchi changa katika masuala mbali mbali ya maendeleo ikiwemo Elimu, Afya na Teknolojia ya kisasa.
Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed alisema misaada ya Taifa hilo imepelekea Mataifa ya Afrika kupiga hatua kubwa ya maendeleo na kutatua changamoto zinazozikabili nchi hizo.
Waziri Hamad Rashid alieleza hayo kwenye maadhimisho ya miaka 69 ya Ukombozi wa Taifa la China yaliyofanyika Hoteli ya Zanzibar Beach Resourt Mbwen.
Alisema Tanzania ni moja ya nchi inayofaidika sana na misaada inayotolewa na Taifa la China ambayo mara nyingi imekuwa haina masharti magumu.
Waziri wa Afya alisema Zanzibar ambayo imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na China imenufaika katika kuimarisha sekta ya Afya kwa kujenga Hospitali mpya ya Abdalla Mzee Mkoani Pemba na kuleta madaktari bingwa na vifaa tiba kutoka nchi hiyo.
 Aliitaja misaada mengine kuwa ni pamoja na kukuza sekta ya Elimu na Michezo kwa kujengewa Uwanja mpya wa Mao tse tung na Ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume uliopo Kisauni.
Waziri wa Afya alieleza matumaini yake kuwa miradi inayoendelea kutekelezwa na China itakamilika katika muda uliopangwa ili iweze kuwahudumia wananchi. 
Katika hatua nyengine Waziri Hamad alitoa pongezi maalum kwa wafanyakazi wa Ubalozi mdogo wa China ulipo Zanzibar kwa kujenga mashirikiano ya karibu na Serikali na wananchi kwa jumla.
Alisema mashirikiano hayo yamewezesha wafanyakazi wengi wa Zanzibar kupata fursa ya kwenda nchini China kwa mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu katika fani mbali mbali.
Balozi mdogo wa China aliepo Zanzibar Xie Xiuowu alisema nchi yake itaendelea kuimarisha uhusiano wake na Mataifa ya Afrika ili kuona yanapiga hatua katika kufikia maendeleo ya kweli na kusiadia wananchi wake.
Alisema kutoka na mipango ya muda mrefu iliyowekwa na China, hivi sasa ni nchi ya pili  kwa uchumi bora duniani na mwaka jana uchumi wan chi hiyo umekuwa kwa asilimia 6.9 kutokana na ukuaji wa viwanda nchini humo.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.