Naibu Katibu Mkuu Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili na Utalii, Uvuvi na Mifugo kutoka
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Islam Seif Salum akifungua mkutano wa
wadau uliojadili masuala ya uchumi endelevu wa Bahari ‘Sustainable Blue
Economy’ unaotarajiwa kufanyika Nchini Kenya. Kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa
Tanga Bi. Zena Said.
Prof. Kassim Kulindwa kutoka
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akitoa majumuisho ya mkutano huo ulifanyika katika
Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa washiriki wa Kikao
hicho Balozi Celestine Mushi kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mtwara akichangia
jambo katika mkutano wa wadau uliojadili masuala ya uchumi endelevu wa Bahari
‘Sustainable Blue Economy’
Na.lulu mussa..
Katika jitihada za kujenga uelewa juu ya dhana nzima ya
uchumi endelevu utokanao na rasilimali za
bahari, mabwawa na mito Ofisi ya Makamu wa Rais imeendesha kikao cha
wadau kutoka taasisi mbalimbali zinazojishughulisha na sekta ya uvuvi na
mazingira kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ili kwa pamoja kuandaa msimamo wa Nchi
katika Mkutano unaotarajiwa kufanyika Nchini Kenya hivi karibuni.
Akifungua kikao hicho Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo,
Maliasili na Utalii, Uvuvi na Mifugo kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
Dkt. Islam Seif Salum amesema kuwa ni muhimu kwa Tanzania kama nchi kunufaika
ipasavyo na fursa za uchumi endelevu wa bahari katika nyanja za uvuvi, utafiti
na uchimbaji wa mafuta na gesi na katika sekta ya utalii.
“Tuko hapa kujadiliana na kuweka mikakati ya pamoja kama
nchi katika kuelekea Mkutano mkubwa wa masuala ya kunufaika na rasilimali za
uvivu katika bahari, mito, maziwa na mabwawa, dhana hii ni mpya hapa nchini
kwetu ingawa tunatekeleza kwa kiwango kidogo.” Alisisitiza Dkt. Salum.
Dkt. Salum amesema kuwa mkutano huo utajenga fursa zaidi
za kuwekeza katika rasilimali za baharini ili kutimiza lengo la kukuza uchumi
na kuendeleza Tanzania ya Viwanda.
Kwa upande mwingine Afisa Uvuvi Mkuu kutoka Ofisi ya
Makamu wa Rais Bi. Emelda Teikwa amesema kuwa dhana ya ‘Blue Economy’ ni ngeni
hapa nchini ila ni muhimu sana katika uchumi. “Tunaangalia namna ambavyo Uchumi
wa bahari unaweza kuchangia katika kukuza pato la Taifa, kwa kuwa na uvuvi
endelevu na kukuza sekta ya utalii”. Alisisitiza Bi. Teikwa.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazoshiriki katika
Mkutano Mkubwa wa uchumi endelevu wa Bahari ‘Sustainable Blue Economy’
unaotarajiwa kufanyika Nchini Kenya mwishoni mwa mwezi huu.
No comments:
Post a Comment