Habari za Punde

Balozi Mpya wa UAE Nchini Tanzanbia Akijiatambulisha Kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Ali Mohamed Shein Ikulu Leo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Ali Mohamed Shein, akizungumza na Balozi Mpya wa UAE Nchini Tanzania Mhe. Khalifa Abdulrahman Al Marzooqi, alipofika Ikulu leo kujitambulisha na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar.

Rais Dk. Shein alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi mpya wa Umoja wa Nchi za Falme za Kirabu (UAE) Khalifa Abdulrahman Mohamed Al-Marzooqi Ikulu mjini Zanzibar ambapo balozi huyo ameeleza hatua zilizofikiwa na (UAE) za kuanzisha ubalozi mdogo hapa Zanzibar.

Dk. Shein kwa upande wake alipongeza hatua hizo zilizofikiwa na (UAE) za kuanzisha Ubalozi mdogo hapa Zanzibar ambazo zinatokana na mazungumzo yake aliyoyafanya kati yake na  Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, Mrithi na Mtawala wa Abu Dhabi na Naibu Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi wa (UAE), wakati wa ziara yake katika nchi za Umoja huo mapema mwaka huu.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alieleza kuwa hatua hiyo inaonesha wazi jinsi Umoja wa nchi hizo unavyochukua juhudi za makusudi za kuhakikisha uhusiano na ushirikiano kati ya pande mbili hizo unazidi kuimarika kwa manufaa ya pande zote.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza hatua zilizofikiwa katika kuendeleza mikakati ya kukuza uchumi hapa Zanzibar na kuzipongeza nchi za Umoja huo katika hatua zake za kuiunga mkono Zanzibar ikiwemo Ras-Al-Khaimah ambayo hivi karibuni ilisaini Mkataba wa Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia, kati yake na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Balozi Al-Marzooqi alimueleza Rais Dk. Shein hatua zilizofikiwa katika mchakato wa kuanzisha Ubalozi huo mdogo hapa Zanzibar ambao alisema utazidi kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo wenye historia.

Kiongozi huyo alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa Umoja wa Nchi za Falme za Kirabu (UAE) utaendelea kuiunga mkono Zanzibar  katika kuendeleza miradi ya maendeleo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.