Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akimsikiliza Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzanbia (UWT) Mhe.Gaudensia Kabaka, alipofika Ikulu Zanzibar, kujitambulisha leo akiongozana na Uongozi wa UWT.kulia Makamu Mwenyekiti wa UWT Mhe. Thuwaiba Kisasi na Bi Queen Mlozi Katibu Mkuu wa UWT, wakiwa katika ukumbi wa mkutano huo.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa wanawake wa Tanzania ndio waliokuwa mstari wa mbele katika kupigania uhuru wa Tanzania Bara na Zanzibar hivyo ni vyema wakapewa kipaumbele ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na uongozi wa Umoja
wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, ulioongozwa na Mwenyekiti wa Umoja huo Gaudensia Kabaka
ambao ulifika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais.
Katika maelezo yake
Rais Dk. Shein ambaye pia, ni Makamo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Zanzibar, aliueleza uongozi huo kuwa wanawake wana nafasi maalum katika Chama
na Serikali kutokana na majukumu yao sambamba na juhudi zao.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa bila ya akina mama mafanikio zaidi hayatofikiwa katika Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na ndani ya (CCM) hasa ikizingatiwa kuwa wana umuhimu mkubwa katika
jamii.
Alieleza kuwa kina
mama ni vyema wakapewa nafasi katika kukitumikia chama chao na Serikali yao na
ndio maana (CCM) ikaunda Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), ambao tokea
kuasisiwa kwake umepata mafanikio makubwa na umekuwa muhimili muhimu wa (CCM).
Aidha, Rais Dk. Shein
alieleza matumaini yake makubwa kuwa uongozi huo mpya wa (UWT) chini ya
Mwenyekiti wake Gaudensia Kabaka utafanya vizuri kwa azma ya kuendeleza
mafanikio katika Umoja huo na CCM kwa ujumla.
Akitoa wito kwa Umoja
huo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuendeleza umoja, mapenzi na na mshikamano miongoni mwa Wanajumuiya
sambama na kufanya kazi wakiwa wamoja.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alisisitiza haja kwa uongozi huo kuwaandaa vijana kushika nafasi za
uongozi katika Umoja huo wa (UWT) hapo baadae hasa ikizingatiwa kuwa kiongozi
huandaliwa hivyo ni vyema wakaandaliwa vijana watakao kitumikia chama chao cha (CCM).
Nae Mwenyekiti wa (UWT)
Taifa Gaudensia Kabaka alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa kutekeleza vyema
Ilani ya Uchaguzi ya (CCM) ya mwaka 2015-2020 huku akitumia fursa hiyo
kumpongeza Dk. Shein kwa kupata kura zote katika mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika Disemba mwaka 2017.
Mwenyekiti huyo
alieleza kuwa kupata kura zote kwa Rais Dk. Shein ambaye ni Makamo Mwenyekiti
wa (CCM) Zanzibar kunatokana na kuwa (CCM) inamkubali na inazikubali kazi zake
anazozifanya katika kuiongoza Zanzibar na watu wake pamoja na chama hicho.
Aidha, Mwenyekiti huyo
alizipongeza juhudi za Rais Dk. Shein kutokana na mafanikio makubwa
yaliopatikana katika kuendeleza na kuimarisha miradi ya maendeleo Unguja na
Pemba sambamba na hatua alizozichukua za kuwaenzi wazee wa Zanzibar na kuwapa
nafasi za uongozi akina mama katika Serikali anayoiongoza.
Pia, Mwenyekiti huyo
alieleza azma, malengo pamoja na mikakati iliyowekwa katika Umoja huo katika
kuhakikisha (CCM) inaendelea kushinda katika chaguzi zote ukiwemo uchaguzi ujao
wa mwaka 2020 sambamba na kusisitiza mchakato wa ziara watakazozifanya Zanzibar
ambazo zitaanzia kisiwani Pemba mara tu baada ya sherehe za miaka 55 za Mapinduzi
mwaka huu.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment