Naibu Waziri Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima akihutubia katika Mkutano wa
24 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi unaoendelea
Katowice Poland. Pamoja na mambo mengi Mhe. Sima amezitaka Nchi zilizoendelea kutimiza wajibu wao wa kutoa michango ya fedha ili
kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi kwa nchi zinazoendelea.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)
Mhe. Mussa Sima amezitaka nchi zilizoendelea kutimiza wajibu wao wa kutoa
michango ya fedha na kuwezesha upatikanaji wa teknolojia za kisasa kwa nchi
zinazoendelea kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kukabiliana na changamoto za
mabadiliko ya Tabianchi kwa mujibu wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi pamoja
na Makubaliano ya Paris.
Akihutubia Mkutano wa 24 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa
Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi unaoendeleo Nchini Poland Mhe. Sima ameeleza
kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoathirika zaidi na athari za mabadiliko
ya tabianchi duniani, ikiwa ni pamoja na kuathiriwa na ukame, mafuriko na
kuongezeka kwa ujazo wa bahari, jambo ambalo huathiri zaidi wakazi wa mwambao
wa bahari pamoja na shughuli zao za kiuchumi ambazo ni msingi wa maisha yao.
Mhe. Sima amesema kuwa athari hizo zimethibitishwa pia
katika taarifa maalumu ya kisayansi iliyotolewa na Jopo la Kimataifa la
Wataalamu wa Mabadiliko ya Tabianchi kuhusu athari zitakazojitokeza iwapo joto la
dunia litaongezeka zaidi ya nyuzijoto 1.5 (1.50C). “Kwa sasa joto la
dunia limeongezeka kwa nyuzijoto 0.85 kulinganisha na kipindi kabla ya
mapinduzi ya viwanda, natoa rai kwa jumuia ya kimataifa kuchukua hatua za haraka
na za makusudi kukabiliana na changamoto hii” Sima alisisitiza.
Katika Hotuba yake Naibu Waziri ameeleza juhudi za
Tanzania katika kukabiliana na changamoto hizi ambazo zinaendana na mpango wa
maendeleo wa Taifa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), Mfumo wa
usafiri wa mwendo kasi katika jiji la Dar es Salaam, ujenzi wa barabara za juu
(flyovers and interchange) na ujenzi wa bwawa la umeme wa maji katika mto
Rufiji ambao unatarajiwa kuzalisha umeme kiasi cha MW 2,115.
Mhe. Sima amesema kuwa nishati ya umeme ambayo ni salama
kimazingira itasaidia katika ukuaji wa uchumi wa viwanda, undeshaji wa treni za
umeme na kurahisisha upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa matumizi ya
majumbani na kusisitiza kuwa kuwa hizi ni hatua muhimu katika kusaidia kupunguza
uzalishaji wa gesijoto zinazochangia ongezeko la joto duniani.
Mhe. Mussa Sima yuko nchini Poland akiongoza ujumbe wa
Tanzania katika mkutano huu ulioanza tangu tarehe 2 Desemba 2018 na utamalizika
tarehe 14 Desemba, 2018.
No comments:
Post a Comment