Habari za Punde

Kasi ya Ukuaji Sekta ya Madini Imeongezeka- Rais Magufuli.



                                                                                  
                                                                                      
Na.Paschal. Dotto. Maelezo                                                                                                                  .  
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amesema kuwa kasi ya ukuaji wa sekta ya madini imeongezeka kutoka asilimia 4 mwaka 2015 mpaka asilimia 4.8 mwaka 2018 baada ya marekebisho ya baadhi ya sheria na usimamizi bora katika sekta hiyo.

Akizungumza leo katika Mkutano wa Sekta ya Madini uliokutanisha wadau, wachimbaji wadogowadogo wa madini, wafanyabiashara wa madini pamoja na wafanyakazi wa Wizara ya Madini uliofanyika Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema kuwa kwa marekebisho ya sheria ya Madini yam waka 2010 imewezesha rasilimali ya madini kuwa mali ya watanzania.

Rais Magufuli aliseme kuwa katika kufanya mageuzi makubwa katika Sekta hiyo Serikali ililzimika kuunda Wizara ya Madini iliyopewa dhamana ya kulinda rasilimali hiyo mnamo mwaka 2017 na kuweza kupata mafanikio makubwa kwa miaka miwili iliyopita.

“Marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 ilifanya mambo mengi sana katika sekta ya madini ikiwemo kurudisha umiliki wa rasilimali madini kwa watanzania na kuwezesha usimamizi na udhibiti wa utoroshwaji madini huku ikiwezesha ujenzi wa ukuta katika eneo la madini ya Tanzanite (Mererani) hii iliiwezesha Tanzania kulinda kwa ukaribu madini yetu”, alisema Rais Magufuli

Rais Magufuli alisema kuwa sekta hiyo chini ya Wizara ya Madini ilikuwa kwa kasi na kuwezesha utoaji wa leseni za wachimbaji wadogowadogo 15,209 huku wachimbaji wengine 5303 wakipata mafunzo ya uchimbaji Madini katika mikoa 14 nchini.

Aidha kasi hiyo ilihusisha Serikali kutoa ruzuku ya fedha za kitanzania bilioni 7.616 ya uchimbaji madini mbalimbali hapa nchini, huku ikiwezesha uzalishaji wa madini kuwa mkubwa zaidi ukilinganisha na miaka ya nyuma, takwimu zinasema kuwa katika mgodi wa almasi Mwadui uzalishaji uliongezeka kwa kuzalisha karati 341,000 mwaka 2018, kiasi ambacho kwa mara ya mwisho kuzalishwa ilikuwa ni mwaka 1977 karati 317,000 zilizalishwa kiwango ambacho kinakaribia kwenye kiwango cha sasa.

“Mabadiliko makubwa katika sekta hii sasa tumeanza kuyaona hasa katika uzalishaji wa madini katika migodi mbalimbali ikiwemo Mgodi wa Almasi Mwadui ambao ulizalisha karati 341,000 mwaka 2018, hiki ni kiasi kikubwa na kwa mara ya kwanza kwa mgodi huu kuzalisha kiasi kikubwa ilikuwa mwaka 1977 ambapo ulizalisha karati 317,000 kwa hiyo hii inathibitisha kuwa uzalishaji katika sekta hii ya madini umekuwa kwa kasi”, alisema Rais Magufuli.

Pia Serikali imeweza kukusanya na kuvuka malengo ya ukusanyaji mapato ya shilingi bilioni 194 badala yake kuweza kukusanya shilingi bilioni 301 katika sekta ya madini ikiwa ni ongezeko la asilimia 53, na katika nusu ya mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali ilipanga kukusanya shilingi bilioni 160 lakini iliweza kuvuka malengo kwa kupata shilingi bilioni 167.54 sawa na asilimia 8 ya makusanyo.

Rais Magufuli aliongeza kuwa uzalishaji umeongezeka kwa wachimbaji wadogowadogo wa madini ya Tanzanite kutoka  kilo 147.7 mwaka 2017 na 164.6 mwaka 2016 hadi  kilo 781.2 mwaka 2018, huku wakiweza kuongeza mapato kutoka shilingi milioni 166.094 mwaka 2017 mpaka bilioni 1.436 mwaka 2018 baada ya udhibiti na usimamizi mzuri katika sekta hiyo.

Rais Magufuli pia aliwaagiza watendaji wa Wizara ya Mdaini kufanya kazi kwa kushirikiana na Wadau, Wachimbaji, Wafanyabiashara wa Madini ili kuiboresha sekta ya madini nchini kuweza kutoa mapato makubwa kwa Serikali na kusema kuwa anawapongeza Wizara hiyo pamoja na wadau wenginewa madini kwa mafanikio hayo yaliyopatikana ndani ya muda mfupi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.