Habari za Punde

Mfuko wa Khalifa Fund Kuwawezesha Vijana wa Zanzibar Katika Kupata Utaalam na Masuala ya Kiufundi Ili Kuweza Kujiajiri.


Mkurugenzi wa Mfuko wa Khalifa Fund, wenye Makao Makuu ya Nchini Abu Dhabi UAE.Ndg. Nizar Cheniour, akizungumza na Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar,kwa ziara ya Siku Tatu Nchini Zanzibar.

MKURUGENZI wa Mfuko wa ‘KhalifaFund’ Naizar Cheniour, amesema mfuko huo umeazimia  kuwawezesha vijana wa Zanzibar katika nyanja mbali mbali za kiuchumi ili kuweza kujiajiri na kuinua hali zao za maisha.

Mkurugenzi huyo amesema hayo leo wakati  alipozungumza na waandishi wa habari, mara baada ya ujumbe wa Mfuko huo ulipowasili katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar.

Ujumbe huo upo nchini kwa ziara maalum, ikiwa ni muendelezo wa mazungumzo na Serikali, yenye lengo la kufanikisha utekelezaji wa programu mbali mbali katika sekta za biashara, ujasiriamali, miundombinu na nyenginezo.

Alisema Mfuko umelenga kuwawezesha vijana wa Zanzibar katika upatikanaji wa rasilimali fedha, utaalamu na masuala ya kiufundi ili waweze kujiajiri kupitia shughuli za ujasiriamali na hivyo kuweza kujitegemea.

Aliwataka vijana na Wazanzibari kwa ujumla kutarajia mafinikio makubwa kutokana na  program mbali mbali zitakazotekelezwa kupitia Mfuko huo.

Alisema mfuko wa KhalifaFund, una uzoefu mkubwa katika utekelezaji wa programu za maendeleo na shughuli za kiuchumi, ambapo umekuwa ukifanya kazi hizo katika nchi mbali mbakli duniani.

Mapema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda,Ndg.Juma Ali Juma alisema ujio wa Viongozi wa Mfuko wa’ KhalifaFund’  umelenga kukamilisha mazungumzo yaliofikiwa katika kikao kilichopita ili kuwa tayari kwa utekelezaji wa yale yalioafikiwa.

Alisema mfuko huo wa kifedha, wenye makao makuu yake Abu Dhabi ,UAE utatowa msukumo mkubwa  katika utekelezaji wa program mbali mbali za kimaendeleo na kiuchumi, sambamba na kuwawazesha vijana kupitia kazi za ujasiriamali.

Alisema wakati ukiwa nchini utakutana na kufanya mazungumzo na taasisi mbali mbali za Serikali pamoja na kutembelea maeneo tofauti.

Hii ni mara ya pili kwa viongozi wa Mfuko wa ‘KhalifaFund’ kuja nchini kwa ajili hiyo, ambapo kabla ulipata fursa ya kutembelea sekta tofauti za maendeleo na kiuchumi Unguja na Pemba.

Aidha, ujio wa mfuko huo unafutia ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein aliyoifanya Umoja wa nchi za Falme ya Kiarabu (UAE) Januari mwaka uliopita. 

Abdi Shamnah, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.