Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Ahutubia Maadhimisho ya Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar Uwanja wa Gombani Kisiwani Pemba.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa kutokana na juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuimarisha uchumi wake ukusanyaji wa mapato umeimarika.

Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika uwanja wa Gombani Pemba, Mkoa wa Kusini Pemba katika Kilele cha Sherehe za miaka 55 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964

Alieleza kuwa jumla ya TZS bilioni 688.7 zilikusanywa mwaka 2017/2018 na Taasisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) ikilinganishwa na TZS bilioni 521.8 zilizokusanywa na Taasisi hizo mwaka 2016/2017.

Alisisitiza kuwa kiwango hicho ni sawa na ongezeko la TZS bilioni 166.9 sawa na asilimia 32 ambapo mafanikio hayo yameiwezesha Serikali kutekeleza mipango yake ya kuzidi kuinua uchumi na kuwasogezea wananchi huduma za kijamii kwa wepesi na kwa ufansi mkubwa.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa kasi ya ukuaji uchumi huo ilikuwa asilimia 7.7 mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 5.8 mwaka 2016 ambapo pia, pato la mtu binafisi liliongezeka na kufikia TZS milioni 2.1 sawa na US$ 944 kwa mwaka 2017 ikilinganishwa na TZS milioni 1.89 sawa na US$ 868 mwaka 2016.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa mfumko wa bei nao uliendelea kudhibitiwa katika tarakimu moja katika mwaka 2018 ambapo kasi ya mfumko wa bei ilifikia asilimia 3.9 ikilinganishwa na asilimia 5.6 katika mwaka 2027.

Alieleza kuwa mafanikio hayo yaamechangiwa na juhudi mbali mbali za Serikali ikiwemo kuwashajiisha wazalishaji wa ndani na kuweka mazingira mazuri ya biashara katika uagiziaji na usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi.

Rais Dk. Sheina alisema kuwa katika kipindi cha miaka 55 ya Mapinduzi, yamepatikana mafanikio makubwa sana na kuimarika kwa huduma za elimu ambapo kabla ya Mapindzi ya 1964 huduma  hizo zilikuwa chache na zilikuwa kwa ubaguzi na wachache waliopata fursa ya elimu walilazimika kulipia.

Alisema kuwa Serikali inaendelea na uamuzi wake uliotoa tarehe  Machi 3, 1965 wa kuwapa wananchi matibabu bure ambapo lengo ni kuhakikisha kuwa wananchi wote wa Unguja na Pemba wanapata huduma za kinga na tiba kwa ajili ya kuendeleza afya na kusisitiza kuwa Serikali itafanya kila iwezalo ili huduma za afya ziendele kuwa bure.

Katika utekelezaji wa mradi wa maji wa Mkoa wa Mjini Magharibi, kwa mkopo wa Benki ya Manedleo ya Afrika Rais Dk. Shein alisema kuwa kazi kuwa tayari imeshafanyika na jumla ya visima 9 vipya tayari vimeshachimbwa na 23 vya zamani vimefanyiwa matengenezo.

Aliongeza kuwa pampu mpya zitafugwa kwenye visima hivyo, mabomba mapya yamelazwa na ujenzi wa matangi makubwa ya maji unaendelea huko Saateni na Migombani Mnara wa Mbao.

Kwa upande wa huduma za umeme alieleza kuwa hadi kufikia mwezi wa Disemba mwaka 2018 Serikali imezifikisha huduma za umme katika vijiji 2,694 kati ya vijiji 3,259 vya Unguja na Pemba ikiwa ni sawa na asilimia 83 ambapo kati ya vijiji hivyo, vijiji 55 vilipatiwa umeme mwaka 2018.

Aidha, alisema kuwa kuwanzia mwezi wa Novemba 2018 utafiti mwengine wa Mafuta na Gesi Asilia umeanza kufanyika katika maeneo yenye maji madogo huko Pemba na baadae utaendelea kwa upande wa Unguja.

Alisema kuwa kwa mujibu wa Mkataba sasa Kampuni ya RAKGAS imeidhinishwa rasmi kufanya kazi ya utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia katika Kitalu cha Pemba-Zanzibar.
Katika hatua za kuliimarisha Shirika la Meli la Zanzibar, alisema kuwa Serikali inajenga meli mpya ya mafuta itakayojulikana kwa jina la MT Ukombozi II ambayo ujenzi wake unafanyika na Kampuni ya Damen Shipyard ya Uholanzi na meli hiyo inatarajiwa kwuasili nchini miezi michache ijayo.

Vile vile Dk. Shein alisema sekta ya Utalii imeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka, huku idadi ya watalii ikiongezeka, ambapo katika mwaka 2018 jumla ya watalii 520,809 waliwasili nchini, ikilinganishwa an watalii 433,116 waliowasili nchini mwaka 2017, ikiwa ni ongezeko la watalii 87,693 sawa na asilimia 20.

Alisema lengo la Serikali la kufikia watalii 500,000 kwa mwaka ifikapo mwaka 2020 tayari limefikiwa kabla ya wakati huo.

Dk Shein aliwahakikishi wananchi wote na wageni wanaoitembelea Zanzibar kuwa iko salama na itaendelea kubaki salama na kwamba Serikali zote mbili zitaendelea kutekeleza wajibu wao huo wa Kikatiba na Sheria katika kulinda amani, utuliu na maisha ya wananchi na mali zao.

Alisisitiza kuwa wakati Serikali zote mbili zikitimiza wajibu wao wananchi nao wanapaswa wazitii sheria jambo ambalo ni muhimu na la lazima katika kulifanikisha suala la amani na utulivu.

Aliongea kuwa iila mmoja anapaswa atekeleze wajibu wake huo kwa kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa na Sheria za nchi zinafuatwa kwani wote wana wajibu mkubwa wa kuyalinda, kuyaenzi na kuyadumisha Mapinduzi sambamba na kuuendeleza na kuudumisha Muungano.

Rais Dk. Shein aliwahakikishia wananchi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendeleza na kuimarisha Muungano uliopo.

“Mimi na Dk. John Pombe Joseph Magufuli tutahakikisha kuwa Muungano wetu unadumu na unaimarika kwa dhamira ile ile ya viongozi wetu wa awamu zilizotangulia, ili nchi yetu iendelee kupiga hatua kubwa zaidi na ibaki kuwa ya amani na utulivu”,alisema Dk. Shein.

Mapema Dk. Shein alipokea maandamano ya wananchi kutoka  Wilaya zote za Unguja na Pemba,ikifuatiwa na wafanyakazi kutoka Taasisi,  Idara na Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar , waliovalia sare  ya miaka 55 ya Mapinduzi hayo.

Aidha, sherehe hizo zilifuatiwa na gwaride rasmi lililoandaliwa, ambalo lilivishirikisha vikosi vya Ulinzi na Usalama, ikiwemo JWTZ, Polisi,  Mafunzo, KMKM, Zimamoto  na KZV, ambavyo vilipita mbele ya mgeni rasmi na kutoa heshima zao,  kwa mwendo wa pole na haraka.

Vile vile, uwanja huo kwa nyakati tofauti ulirindima shangwe na hoi hoi, kutokana na maonyesho mbali mbali yaliofanyika, huku wapiganaji wa  Jeshi la Polisi wakionyesha ustadi wa kucheza ‘kwata la Tarabushi’, gwaride lililochezwa na jeshi hilo  kabla Mapinduzi ya 1964.

Nao, wapiganaji wa JWTZ wakazipamba sherehe hizo kwa maonyesho ya gwaride la kimya kimya pamoja na yale ya askari wake kukabiliana na adui bila kutumia silaha.
Sambamba na hilo, ngoma mbali mbali za Utamaduni za Msewe, Chaso, Msi haya  nazo zikatoa burudani za aina yake  kwa wananchi waliohudhuria sherehe hizo.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na maelfu ya wananchi pamoja na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa ana Serikali akiwemo Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bejamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Amani Abeid Karume, Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.