Habari za Punde

Balozi Seif Amesema Mapinduzi Yamesaidia Kuwaunganisha Wananchi Ikiwa Ndio Chanzo cha Maendeleo.Yaliopo Sasa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif akisalimiana na Waziri Kiongozi Mstaafu  wa Zanzibar  Mh. Shamsi Vuai Nahodha kwenye Hosteli ya Misali Wesha Chake Chake Pemba walipotengewa Viongozi wa Kitaifa kupata Chakula cha Mchana. Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Wananchi wa Zanzibar wataendelea  kuthamini Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 pamoja na yale yote yaliyoletwa na yanayoendelea kupatikana kutokana na Mapinduzi hayo.
Alisema Mapinduzi hayo yamesaidia kuwaunganisha Wananchi wote  ikiwa  ndio chanzo cha Maendeleo yaliyopo hivi sasa yakineemesha Jamii yote iliyokuwa imegubikwa na mfarakano uliotokana na kugaiwa kimatabaka na Tyawala za Kikoloni.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akijiandaa kumkaribisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein kulihutubia Taifa katika Kilele cha Maadhimisho ya Sherehe za kutimia Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar  kwenye Uwanja wa Michezo Gombani Chake Chake Kisiwani Pemba.
Alisema Mzanzibari ameweza kukomboka kutokana na Mapinduzi hayo ya Zanzibar  yaliyosaidia kuondosha manyanyaso na mateso yaliyoambatana na hali duni ya Maisha na Kiuchumi kwa Waafrika waliowengi na kusababisha kukosa haki ya kumiliki Ardhi ndani ya Visiwa hivi.
Balozi Seif  alisema juhudi na ueledi wa usimamizi na utunzaji mzuri wa Amani unaosimamiwa na Viongozi wa Serikali zote Mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar  umewezesha kuimarika kwa Uchumi na Miundombinu itakayoipeleka Tanzania kufika uchumi wa kati katika kipindi kifupi kijacho.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea faraja yake kutokana na Sherehe za Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar kuibua Miradi 35 ya Maendeleo iliyofunguliwa na Miradi 18 iliyowekewa Mawe ya Msingi.
Alisema sherehe hizo zimekwenda sambamba pia na ushirikishwaji wa matukio 15 ya shughuli mbali mbali ikiwemo mashindano ya Michezo pamoja na Matamasha yaliyofanyika katika Wilaya tofauti za Unguja na Pemba.
Balozi Seif aliipongeza kwa dhati  Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa pamoja na Kamati zake zote ndogo ndogo kwa kazi kubwa ilizofanya za kufanikisha Sherehe hizo tokea mwanzo wa matayarisho hadi zilipofikia hitimisho lake.
Aidha Balozi Seif akiwa Mwenyekiti wa Halmshauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa pia aliwashukuru Wananchi wote wa Unguja na Pemba kwa kujitokeza kwa wingi kwenye sherehe zote zilizoandaliwa za uzinduzi na uwekaji wa Mawe ya Msingi na Miradi yote ya Maendeleo Nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.