Habari za Punde

Katika kusherehekea kutimia miaka 42 ya CCM Timu za mpira wa pete za Fujoni na Kitope zakutana

 Mke wa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Mama Asha Suleiman Iddi akisalimiana na Wachezaji wa Timu ya Pete na Fujoni iliyopambana na Kitope katika Mchezo wa Kusherehekea kutimia Miaka 42 ya CCM hapo Uwanja wa Kiwanda cha Sukari.
 Mama Asha akifungua mchezo wa Mpira wa Pete wa Kusherehekea kutimia Miaka 42 ya CCM iliyowakutanisha Timu za Fujoni na Kitope hapo Uwanja wa Kiwanda cha Sukari.
 Mafahali wa Timu za Mchezo wa pete za Fujoni na Kitope wakichuana kwenye mchezo wa Kusherehekea kutimia Miaka 42 ya Chama cha Mapinduzi.
Mama Asha Suleiman Iddi akitoa zawadi za Vifaa tofauti vya Mchezo wa Pete kwa Timu za Mchezo wa pete za Fujoni na Kitope wakichuana kwenye mchezo wa Kusherehekea kutimia Miaka 42 ya CCM.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Uongozi wa Jimbo la Mahonda umejikita kuimarisha Sekta ya Michezo katika azma nzima ya kuinua kiwango cha Michezo kitakachowawezesha Vijana ndani ya Jimbo hilo kujiwekea njia ya kupata ajira kupitia fani hiyo muhimu kwa sasa hapa Duniani.
Uimarishaji huo unakwenda sambamba na ile Ilani ya CCM ya Mwaka 2015 -2020 iliyozielekeza Serikali zote mbili Nchini Tanzania kuimarisha Sekta hiyo kwa kuinua viwango vya Michezo kwa kutanua wigo wa vyanzo endelevu vya Miundombinu ya kuendeleza Michezo.
Mke wa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Mama Asha Suleiman Iddi alisema hayo baada ya kushuhudia pambano la kirafiki la Mchezo wa Mpira wa Pete {Netball} uliozikutanisha Timu za Madada wa Fujoni dhidi ya Kitope lililofanyika katika uwanja wa mahonda Kiwandani.
Mama Asha alisema utaratibu wa kuwapatia vifaa katika Michezo tofauti Vijana wa Jimbo hilo utaendelea ili kuwajengea ari ya kupenda Michezo licha ya kuimarisha Afya bora zitakazowaepusha na Maradhi mbali mbali pamoja na kuwa mbali na vikundi vya kihuni.
Aliwataka Vijana hao kujikita katika masuala ya Kijamii na kuacha kasumba na mambo yanayoendelea kuenezwa na Watu walioshindwa kutafuta masuala ya msingi yatakayowawezesha Vijana hao kujitegemea zaidi.
Katika pambano hilo mbali ya kutafuta Timu ya Kombaini ya Netball ya Jimbo la Mahonda lakini pia ulikwenda sambamba na shamra shamra za maadhimisho ya Sherehe za kutimia Miaka 42 ya Chama cha Mapinduzi tokea kilipoasisiwa kwenye Uwanja wa Amani Mjini Zanzibar mnamo Mwaka 1977.
Timu ya Fujoni iliyovalia sare rangi ya wardi ilitoka na ushindi wa Goli 16 dhidi ya 11 ya Kitope pambano lililotawaliwa na ushindani mkali uliopelekea baadhi ya Wachezaji wa Timu zote mbili waliokuwa hawana mazoezi kwa kipindi kirefu kupata taabu kubwa ya pumzi.
Mama Asha Suleiman Iddi alifurahishwa na pambano hilo na kupelekea kusaidia vifaa vya Michezo kwa Timu zote mbili zilizopambana kwenye mchezo wa kusherehekea Miaka 42 ya CCM.
Vifaa hivyo vitakavyoamsha ari ya Wanamichezo hao ni pamoja na Seti za Jezi, Mipira pamoja na Magoli kwa Viwanja vya Timu zote Mbili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.