Habari za Punde

Kero ya Mpaka Kati ya Kenya na Tanzania Kupatiwa Ufumbuzi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.  Dkt. Damas Ndumbaro akiwa Kenya na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akiwa Tanzania wakiwa wameshikana mikono kudhihirisha changamoto ya Mpaka huo uliopo Jasini Mkinga Mkoani Tanga.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mandakini Bw. Nasoro Mbarook, akieleza kuhusu kukamatwa kwa wavuvi 112 wa Tanzania na kulipishwa Sh. 5000 za Kenya kwa kosa la kuvua samaki eneo ambalo linachangamoto za Kimpaka. Kushoto ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.  Dkt. Damas Ndumbaro  na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb).
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.  Dkt. Damas Ndumbaro, pamoja na viongozi wa Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga wakielekea katika Mpaka wa Kenya na Tanzania ili kujionea changamoto zilizopo ambazo zinachangia kudhorota kwa shughuli za maendeleo
Kulia ni nyumba iliyopo Nchini Kenya na Kushoto ni Nyumba iliyopo Tanzania hivyo kuwa ishara tosha ya kutozingatiwa kwa taratibu za kuacha eneo la takribani  mita Thelathini kutoka nchi moja kwenda nyingine.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.  Dkt. Damas Ndumbaro, wakiangalia eneo la Mpaka wa Tanzania na Kenya katika Kijiji cha Mahandakini Wilayani Mkinga Mkoani Tanga.
 Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.  Dkt. Damas Ndumbaro akiwa Kenya na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akiwa Tanzania wakiwa wameshikana mikono kudhihirisha changamoto ya Mpaka huo uliopo Jasini Mkinga Mkoani Tanga.


Na. Peter Haule WFM, Tanga
Serikali imeahidi kutatua mgogoro wa Mpaka kati ya Tanzania na Kenya katika Kijiji cha Mahandakini, Wilayani Mkinga mkoani Tanga, baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wanakijiji wanaoishi katika mwambao huo wa Bahari ya Hindi baada ya kuzuiwa kufanya shughuli zao za uvuvi na kuwasababishia hali ngumu ya maisha.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro walipotembelea na kukagua eneo hilo la mpaka na nchi Jirani ya Kenya.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mahandakini,  Bw. Nasoro Mbarook, alisema kuwa wavuvi wa Kijiji hicho wanashindwa kuendelea na shughuli za uvuvi baada ya vifaa vyao vya uvuvi  kukamatwa na wavuvi takribani 112 kukamatwa na vikosi vya ulinzi vya Serikali ya Kenya nakufunguliwa mashtaka kisha kutozwa faini ya Sh. 5000 ya Kenya, jambo ambalo wavuvi hao wanaamini halikua sahihi kwa kuwa walikua wanavua katika maji ya Tanzania katika Bahari ya Hindi hivyo hawakutenda kosa kama ilivyodaiwa.
Manaibu Waziri hao, walisema dhumuni la ziara yao katika mpaka huo ni kujionea hali halisi na pia kuweka mikakati ya namna ya  kutatua changamoto zilizopo ikiwemo ya wananchi kushindwa kulipa kodi kutokana na kukosa kipato kilichotokana na uvuvi ambapo kwa sasa wanazuiwa kufanya shughuli za uvuvi.
Walisema kuwa wamejionea hali halisi ya mpaka huo hivyo Serikali itafanya tathmini kisha kufanya majadiliano na wenzao wa Kenya ili kulitafutia ufumbuzi suala hilo.
Aidha walibaini kuwa eneo la mpaka halijazingatia taratibu  kwa kuwa zipo nyumba ambazo zimejengwa chini ya umbali wa mita 30  mahali ambapo palipaswa kutokuwepo makazi hayo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Bw. Yona Mark, ameiomba Serikali kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Shule ya Msingi katika Kijiji cha Mandakini Wilayani humo ili wanafunzi waanze kusoma kwa kuwa kwa sasa watoto wanasoma katika shule iliyopo eneo la Kenya.
Pia ameomba  kujengwa kwa barabara katika eneo hilo la Kijiji ambalo linawakazi zaidi ya 3666 na Kituo cha kukusanya mapato kwa kuwa eneo hilo kuna bidhaa nyingi zinazoingia na kutoka nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.