Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk Ali Mohamed Shein, Aendelea na Ziara Yake Wilaya ya Kakazini "A" Unguja na Kufungua Skuli ya Sekondari ya Kijini Matemwe leo.17-2-2019.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akikata utepe kuashiria kuifungua Skuli ya Sekondari ya Kijiji Wilaya ya Kaskazini "A" Unguja iliojengwa na Kampuni ya Island Lodge, inayomilika Hoteli ya Mnemba.Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akishuhudia uzinduzi huo uliofanyika leo 17-2-2019.

Na.Abdi Shamnah. Ikulu Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Moahmed Shein amesema uzinduzi wa Mabanda ya madarsa ya skuli ya Sekondari Kijini, una mnasaba mkubwa na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2015 – 2020.
Amesema wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2015, Viongozi wa Chama hicho waliahidi kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi na kijamii, ikiwemo uimarishaji wa sekta ya elimu,
Dk. Shein amesema hayo katika hafla ya uzinduzi wa madarasa manne (4) ya kusomea katika skuli ya Sekondari Kijini, Mkoa wa Kaskazini Unguja, yaliojengwa na Mwekezaji kutoka Kampuni ya “AndBeyond” iliyowekeza katika Hoteli ya Mnemba Lodge.
Ujenzi wa mabanda hayo  ulioanza February 2018 hadi Octoba, 2018 umegharimu zaidi ya shilingi Milioni 148.5 hadi kukamilika kwake, ikiwa pamoja na ununuzi wa samani za walimu na wanafunzi.
Dk. Shein alimpongeza mwekezaji huyo na kusema ameonyesha njia  kuelekea maendeleo ya kielimu nchini, sambamba na kuahidi Serikali kuendeleeza juhudi hizo ili kuimarisha sekta hiyo.
Akigusia sekta ya elimu kabla ya Mapinduzi, Dk. Shein alisema hadi kufikia mwaka 1948, Zanzibar ilikuwa na skuli chache za msingi na sekondari , wakati ambapo Mkoa wa Kaskazini ulikuwa na skuli ya Mkwajuni pekee.
Alisema Wazanzibari wanyonge walishindwa kupata elimu, kwa vile ilikuwa ikitolewa kwa misingi ya matabaka na  uwezo wa mtu.
Aidha alisema wananchi wa Nungwi walinyimwa haki ya kupata elimu baada kupotoshwa juu ya faida zake, sambamba na kuharibu utamaduni wao.
Alisema Mapinduzi ya 1964 yalikuja kumkomboa Mzanzibari, baada ya elimu kutolewa bure, ikiwa ni utekelezaji wa sera ya Chama cha ASP iliyowekwa wakati wa kupigania uhuru.
Alisema hivi sasa sekta ya elimu imeimarika nchini na  imekuwa ikipatikana katika ngazi zote kuanzia ngazi ya shina, wadi, Wilaya hadi Mikoa.
Alisema mnamo mwaka 2014, Serikali ilipanga kuandikisha wanafunzi wa elimu ya msingi kwa asilimia mia moja hadi kufikia mwkaa 2020, jambo ambalo limetekelezwa kabla ya wakati, ambapo hivi sasa tayari wanafunzi walioandikishwa wamefikia asilimia 116 (116%), huku elimu ya sekondari wakifikia asilimia 86 (86%).
Dk. Shein, alisema hivi sasa Serikali inakamilisha ujenzi wa skuli tisa za Ghorofa katika maeneo mbali mbali  Unguja na Pemba, wakati ambapo kuna  Vyuo Vikuu vitatu vya elimu yajuu, kimojawapo kikiwa cha serikali.
Alisema lengo la serikali ni kuwaandaa wanafunzi ili kuwa na wataalamu katika fani tofauti, kwa lengo la kulisaidia Taifa pamoja na kuwasaidia wazazi wao.
Alisema Jimbo la Kijini lina bahati kubwa, hivyo linapaswa kuendelea kuimarishwa kielimu, akibainisha matarajio yake katika kipindi cha miaka kumi ijayo ya jimbo hilo kupata  Chuo Kikuu.
Aidha, Dk. Shein aliwataka wazee na wazazi wa kijiji hicho kuwa imara na kuwaelimisha watoto wao, sambamba na kuepuka upotoshaji na udanganyifu unaosambazwa na watu wasiowatakia mema.
Katika hatua nyengine Dk. Shein aliwahakikishia wananchi wa Kijini na maeneo jirani kuwa barabara ya Mkwajuni – Kijini hadi Mbuyutende itajengwa mwaka ujao, mara tu baada ya barabara ya Bububu – Mkokotoni kumalizika ujenzi wake.
Alisema maandalizi ya ujenzi wa barabara hiyo unaendelea vyema ,ambapo tayari serikali  imeagiza vifaa vinavyohitajika.
Mapema, Makamo wa Pili wa Rais wa Mapinduzi ya  Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, aliwataka wawekezaji wengine wenye miradi katika maeneo hayo kuiga mfano wa kampuni ya Andbeyond’  ili kuisaidia jamii inayowazunguka.
Alisema kuna wawekezaji wengi katika maeneo hayo, hivyo akataka kutumia sehemu ya faida wanayopata kusaidia huduma za kijamii.
“Kutokana na uwekezaji Serikali hunufaika kutokana na kupata mapato sambamba na wananchi kunufaika kutokana na faida kupitia sekta za kijamii kama vile upatikanaji wA huduma za maji, afya na barabara”, alisema.
Aliwataka wananchi hao kushirkiana na wawekezaji wa maeneo hayo ili hatimae waweze kunufaika na matunda yatokanayo na uwekezaji.
Nae, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma aliishukuru Kampuni ya ‘Andbeyond’ kwa misaada mbali mbali inayotowa kwa wananachi wa maeneo hayo, ikiwemo uimarishaji wa elimu.
Alisema misaada hiyo inakuja kutokana na mazingira bora yaliowekwa na Serikali kupitia sekta ya uwekezaji na kutoa fursa kwao ya kuisaidia jamii.
Aliwataka wazazi kutumia vyema fursa zinazotolewa na serikali na kushirikiana nayo ili kufanikisha dhana ya uimarishaji wa sekta ya elimu nchini.  
Aidha, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu naMafunzo ya Amali Madina Mjaka alisema ujenzi wa madarasa hayo utapunguza msongamano  wa wanafunzi madarasani, hadi kufikia wanafunzi 45 kwa darasa moja.
Aliwashajiisha wazazi na walezi wa maeneo hayo kuthamini juhudi zinazochukuliwa kwa kuandikisha wanafunzi wote wanaopasa kuanza masomo.
Naibu Katibu Mkuu huyo alitoa shukurani kwa kampuni iliyofanikisha ujenzi huo kwa juhudi kubwa iliyofanya, sambamba na kushirikiana vyema na wananchi wa eneo hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.