Habari za Punde

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Akutana na Uongozi wa Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti na Matibabu ya Maradhi ya Saratani na Mionzi ya Nchini Cuba.

Katibu Mkuu Afya Bibi Asha wa Tatu kutoka Kulia akisisitiza jambo wakati wa kikao cha kubadilishana mawazo na Uongozi wa Taasisi ya Taasisi ya Utafiri na Tiba ya Maradhi ya Saratani Nchini Cuba Mjini Havana.
Wa Kwanza Kulia ni Mratibu Mtaalamu Mkuu wa Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti na Utibabu wa Maradhi ya Saratani na Mionzi ya Nchini Cuba Profesa Lorenzo Anasagasti.
Bibi Asha wa Tatu kutoka Kulia akiwa katika Picha ya pamoja na Wataalamu wa Taasisi ya Taasisi ya Utafiri na Tiba ya Maradhi ya Saratani Nchini Cuba Mjini Havana.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Bibi Asha Ali Abdullah wa kwanza Kutoka Kushoto akizungumza na Uongozi wa Taasisi ya Utafiri na Tiba ya Maradhi ya Saratani Nchini Cuba alipofika na Ujumbe wake kujifunza kwenye Makao Makuu ya Taasisi hiyo Mjini Havana.Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Kamis OMPR.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Bibi Asha Ali Abdulla alisema Cuba ina Historia ndefu katika Sekta ya Afya ambayo inaweza kuendelea kutoa funzo kwa Zanzibar iliyojipanga kuimarisha  miundombinu  itakayowezesha kutoa huduma bora za Afya kwa Wananchi wake.
Bibi Asha alieleza hayo akiiongoza Timu ya Wakurugenzi wa Wizara yake wakati akizungumza na Uongozi wa Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti na matibabu ya Maradhi ya Saratani na Mionzi  ya Nchini Cuba kwenye Makao Makuu ya Taasisi hiyo Mjini Havana Cuba wakiwa katika ziara ya siku Nne ya kujifunza mbinu na masuala mbali mbali ya Afya.
Alisema Zanzibar tayari imeanzisha kitengo Kidogo cha matibabu   ya Saratani katika kipindi cha hivi karibuni ambacho kitahitaji kupata msukumo wa Kitaaluma kupitia Wataalamu waliobobea wa fani hiyo akitolea Mfano Wataalamu waTaasisi hiyo ya Kitaifa ya Tiba ya Saratani ya Cuba wanaoweza kusaidia nguvu zao.
Hata hivyo Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar aliishukuru Serikali ya Cuba kupitia Taasisi zake mbali mbali za Sekta ya Afya zinazoendelea kuiunga mkono Zanzibar katika mafunzo ya juu kwa Watumishi wake wa Sekta ya Afya  Visiwani Zanzibar na Nchini Cuba chini ya usimamizi wa Wataalamu wa Nchi hiyo Rafiki.
“ Kitengo cha tiba ya Maradhi ya Kensa kwa Zanzibar bado kipya ambacho Wataalamu wa Cuba  wanaweza kusaidia mbinu na Taaluma katika kuona mpango huo unafanikiwa kwa faida ya Ustawi wa Wananchi wote”. Alisisitiza Bibi Asha.
Alisema juhudi zimechukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya katika kukiimarisha Kitengo hicho kwa kuwapatia Mafunzo ya juu Madaktari Watatu  wa kutibu Maradhi ya Kensa ili Zanzibar ifikie hatua ya kuwa na Wataalamu wake katika azma ya kuwaondoshea usumbufu Wananchi wake kufuata huduma hiyo nje ya Zanzibar.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Utafiti Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Mayasa aliushauri Uongozi wa Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti na matibabu ya Maradhi ya Saratani na Mionzi  ya Nchini Cuba kujenga ushirikiano na Zanzibar katika masuala ya Utafiti, ufundishaji wa Madaktari pamoja na Wauguzi ambao wako katika Kitengo cha Saratani.
Dr. Mayasa alisema ushirikiano wa pamoja baina ya Taasisi ya Utafiti wa Afya ya Zanzibar {ZAHRI} na ile ya Cuba unapaswa kuelekezwa pia katika Dawa asili za Mitishamba ambazo zinaweza kusaidia tiba ya Saratani.
Mapema Mratibu Mtaalamu Mkuu wa Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti na Utibabu wa Maradhi ya Saratani na Mionzi ya Nchini Cuba Profesa Lorenzo Anasagasti alisema Taasisi hiyo imeasisiwa mnamo Mwaka  1945 ikilenga kuimarisha  Afya za Wananchi wake.
Profesa Lorenzo alisema hatua mbali mbali za utafiti zilianza kuchukuliwa baada ya kutokea  kesi ya kwanza ya maradhi ya Saratani mnamo Mwaka 1637  katika kukabiliana na changamoto zinazosababisha maradhi hayo yaliyopelekea kifo cha kwanza cha maradhi hayo Mwaka huo wa 1637. 
Alisema Madaktari wa Cuba wameanza safari ya kujiingiza katika Utafiti wa Kina kufuatia kuanzishwa kwa Chuo cha Sayansi chini ya Mabingwa kutoka Nchini Uingereza,ujerumani pamoja na  Ufaransa kwa kutumia vifaa vya Teknolojia ya  kisasa.
Alifahamisha kwamba utaalamu wa kutumia Mionzi kwa kutibu maradhi ya Kensa uliongezeka zaidi mnamo Mwaka 2014 na kusaidia kutibu Wagonjwa kutoka Nchi 14 Duniani yakiwemo Mataifa ya Bara la Afrika.
Alieleza kwamba Taasisi hiyo ya Utafiti na utibabu wa maradhi ya Saratani Nchini Cuba imelenga kuongeza vituo zaidi kutoka Vinane Nchini humo kuanzia Mwaka 2020 hadi ifikapo Mwaka 2030 vitakavyokwenda sambamba na matakwa ya Shirika la Afya Ulimwenguni {WHO}.
Profesa Lorenzo Anasagasti alifahamisha kwamba kuongezeka kwa umri mrefu wa Binaadamu , kupungua kwa gharama za  matibabu pamoja na kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kufanya kazi unapatikana kutokana na wagonjwa wachache wa maradhi ya Kensa.
Akizungumzia suala ya Takwimu Profesa Lorenzo alisisitiza umuhimu wa kuwepo  vielelezo vitakavyotowa muelekeo wa upatikanaji wa Taarifa sahihi za muenendo mzima wa Matibabu ya maradhi ya Saratani {Kensa}.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Ujumbe wa Timu hiyo ya Wizara ya Afya Zanzibar Mkurugenzi Tiba Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Juma Salum Mbwana {Mambi} alimpongeza Mtafiti huyo wa Taasisi ya Mambo ya Saratani na Mionzi ya Cuba Profesa Lorenzo kwa uweledi wake uliopelekea kuwapa mwanga wa matumaini katika Tiba ya Mambo ya Saratani.
Dr. Juma Mambi alisema utibabu wa mionzi na sindano katika kutibu Maradhi ya saratani hasa ya Ngozi imeonekana kuleta mafanikio makubwa katika Kisiwa cha Cuba ingawa zipo Saratani zilizoshinda kutibika kwa njia zote muhimu ambazo ni asilimia ndogo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.