Habari za Punde

Meli ya Sea Star yapata hitilafu ya umeme yashindwa kuondoka bandari ya Wete

Na Masanja Mabula -PEMBA
JUMLA ya abiria 950 waliokuwa wanasafiri na meli ya MV Sea Star 1 kutoka bandari ya Wete kwenda Unguja wamekwama kuondoka bandarini hapo  baada ya kutokea hitalafu ya umeme ndani ya meli hiyo.
Baadhi ya abiria akiwemo Ali Hussein, Shehe Jamali na Halma Ali wamepongeza hatua zilizochukuliwa na vyombo vya ulinzi katika kuokoa maisha yao, na kuushauri uongozi wa meli kufanya ukaguzi kabla ya meli haijaanza safari .
Akizungumza Ali Hossein amesema ni vyema uongozi wa meli hiyo kuifanyia ukaguzi meli yao kabla haijaanza safari ,ili kuzuia kutokea maafa ambayo yanaweza kuepukika.
“Tunamshukuru Mungu kwamba tukio hili limetokea tukiwa bado hatujaanza safari, ilikuwa majanga makubwa , hivyo ni vyema uongozi wa meli kuhakikisha wanafanya ukaguzi kabla ya meli haijaanza safari”alishauri.
Aidha sheha wa shehia ya Sellem Ali Khatib Chwaya ameutaka Uongozi wa meli hiyo kuwapatia chakula abiria hao kwani baadhi wanawatoto wachanga na hela ya kijikimu hawana.
Amesema kampuni hiyo isiangalie maslahi yake, bali pia inatakiwa kuwaonena huruma abiria ambao ni wateja wao.
 Nahodha wa meli hiyo Nassor Abubakar amesema hakuna tatizo kubwa lililojitokeza na kusema kuwa meli itaanza safari baada ya ukaguzi kufanywa na Mamlaka husika.
Amesema hitilafu iliyotokea ni ya kawaida , na inaweza kutokea katika meli yoyote , na kuwataka abiria kuondoa hofu kwani meli iko salama na inaweza kuanza safari yake kama kawaida.
“Ni hitilafu ya umeme na tumefanya ukaguzi tumebaini mashine zote mbili ziko vizuri , lakini kuna tatizo dogo kwenye njia ya umeme”alifahamisha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini PembaKamishna Msaidizi Mwandamizi Mohammed Shekhan Mohaamed amesema hali ya ulinzi imeimarishwa
Amesema jeshi la polisi limejipanga kuhakikisha kwamba abiria wanakuwa katika hali ya usalama wakati wote wakati wanasubiri kufanya safari yao.
“Ulinzi tumeimarisha lengo ni kuhakikisha abiria wanakuwa katika hali ya usalama na utulivu muda wote wakati wanasubiri safari yao”alisisitiza  kamanda.
Katibu Tawala Wilaya ya Wete Mkufu Faki Ali amewataka wananchi kuwa wastahamilifu wakati tatizo hilo linatafutiwa ufumbuzi.
Aidha baahi ya abiria wametaka kuhaulishwa mizigo yao na kupelekwa kwenye meli ya MV Mapinduzi TWO , ili wawahi safari kwani wanaenda kuangalia wagonjwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.