Habari za Punde

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar aonya Wabunge na Wawakilishi kutokupita majimboni


Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dr. Juma Abdulla Saadala { Mabodi } akiufungua Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Mahonda ulioelezea Utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha Miaka Mitatu kuanzia Mwaka 2015 hadi 2019 hapo Ukumbi wa CCM Mkoa uliopo Mahonda.

 Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi akiwasilisha Utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Kipindi cha Miaka Mitatu kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Mahonda.
 Mbunge wa Jimbo la Mahonda Mheshimwa Bahati Abeid Nassir akiwasilisha Utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Kipindi cha Miaka Mitatu kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Mahonda
 Mbunge wa Jimbo la Mahonda Mheshimiwa Bahati Abeid Nassir akimkabidhi Ufunguo wa Gari ya Kubebea Wagonjwa ya Jimbo la Mahonda Naibu Katibu Mkuu wa CCM  DR. Juma Abdullah Saadala kwa ajili ya kuizindua Rasmi.
 Dr. Juma Abdullah Saadala {Mabodi} aliyevaa kofia ya CCM akikata utepe kuashiria kuizindua Rasmi Gari ya Kubebea Wagonjwa kwa ajili ya Jimbo la Mahonda iliyotolewa na Mbunge wa Jimbo hilo Mh. Bahati Abeid Nasir akitekeleza ahadi aliyoitoa wakati wa Kampeni ya Uchaguzi.
Kushoto ya Dr. Mabodi ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi eif Ali Iddi, Kulia ya Dr. Mabodi nia Mbunge wa Jimbo la Mahonda Mh. Bahati Abeid Nassir na nyuma yao ni Mwenyekiti wa Jimbo hilo Nd./Mwinyi Mahfoudh.
Dr. Mabodi akijaribu kuiwasha Gari ya Kubebea Wagonjwa ya Jimbo la Mahonda baada ya kuizindua huku baadhi ya Viongozi wakishuhudia kitendo hicho.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Naibu Katibu Mkuu wa CCM  Zanzibar Dr. Juma Abdullah Saadala { Mabodi } alionya kwamba kitendo cha baadhi ya Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wenye kushindwa kupita Majimboni ni kitendo cha kidhalimu kisichokubalika na wapiga kura wao pamoja na Chama cha Mapinduzi.
Alitoa onyo hilo wakati akiufungua Mkutano Mkuu wa CCM wa Jimbo la Mahonda ulioelezea utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa Mwakilishi na Mbunge wa Jimbo hilo katika kipindi cha Mwaka 2015 hadi 2019 uliofanyika  kwenye Ukumbi wa Mikutano wa CCM Mkoa uliopo Mahonda.
Dr. Abdullah Mabodi alisema kwamba tabia hiyo ya  utoro Majimboni kwa baadhi ya Wabunge na Wawakilishi ambayo kwa kiasi kikubwa hubebwa na mizozano inayosababishwa na Makundi ya Wabunge na Wawakilishi hao haitavumiliwa tena na Chama chenyewe.
Alisema ipo Timu ya Chama cha Mapinduzi iliyoteuliwa kufuatilia utendaji wa Chama katika ngazi mbali mbali kuanzia Matawi, Majimbo hadi Mikoa na kubaini baadhi ya changamoto zinazosababishwa na baadhi ya Viongozi ambazo iwapo zitaachiwa kuendelea zinaweza kupunguza nguvu za Chama kiutekelezaji.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM Zanzibar  aliupongeza Uongozi wa Jimbo la Mahonda  kwa kuibua Miradi muhimu ya Maendeleo kwa ajili ya Wananchi wao na kuitekeleza kwa mafanikio makubwa licha ya changamoto zinazojitokeza katika  utekelezaji wake.
Alisema katika utumishi wake wa Chama hajapokea malalamiko yoyote ya Kimaadili aliyopelekea kutoka Viongozi na Wanachama wa Jimbo la Mahonda  kitendo ambacho kinaleta faraja na kutoa funzo kwa Majimbo mengine Nchini kuiga mfano huo.
Dr. Abdullah Mabodi  aliuomba Uongozi wa Jimbo la Mahonda kuendelea kuwa Darasa kwa Majimbo mengine Nchini yasiyofikia kiwango chao cha Utekelezaji wa majukumu waliyojipangia ikiwemo Utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Akiwasilisha Utekelezaji wa Ilani ya CCM  katika Jimbo la Mahonda kuanzia Mwaka 2016 hadi 2019 Mwakilishi wa Jimbo hilo Balozi Seif  Ali Iddi alisema amekuwa Mtu mwenye furaha kutokana na ushirikiano anaoendelea kuupata katika kuwatumikia Wananchi kwa kasi kubwa.
Alisema katika kipindi cha Miaka Mitatu ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM   2016 hadi 2019 Jimbo la Mahonda limefanikiwa kusimamia Sekta za Afya. Huduma za Maji, Umeme, Elimu, Kilimo, Bara bara, Michezo, Vikundi vya Wajasiri Amali pamoja na kuimarisha Kazi na shughuli za Kisiasa za Chama Tawala.
Balozi Seif alisema  Jumla ya Shilingi Milioni Mia 433,237,700/- zimetumika katika kuendeleza Miradi mbali mbali  katika kipindi cha Miaka Mitatu ambayo imeleta faraja kwa Wananchi walio wengi ndani ya Jimbo hilo hasa ile Miradi ya Huduma za Maji, Elimu, Afya pamoja na Bara bara.
Alisema miongoni mwa Fedha zilizotumika shilingi Milioni Mia 390,839,000/- ni fedha zake binafsi pamoja na Wahisani walioamua kumuongezea nguvu pamoja na shilingi Milioni 42,398,700/- Fedha zilizotengwa kutoka katika Mfuko wa Jimbo.
Balozi Seif alisema pamoja na mambo mengine huduma za Maji Safi na Salama zimeendelea kuimarishwa katika maeneo mbali mbali Jimboni  Mahonda kwa kuweka Miundombinu ya upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa uhai wa Mwanaadamu.
Alisema uungwaji wa Maji umefanywa, uwekaji wa Matangi ya kuhifadhia Maji, Mashine za kusukumia Maji na ujenzi wa Minara umefanywa katika Vijiji tofauti vinavyolizunguuka Jimbo hilo lililopiga hatua kubwa ya Ustawi wa Wananchi wake.
Alifahamisha kwamba harakati hizo za Miundombinu katika Sekta ya Maji zilipelekea kuungwa mkono na Washirika wa Maendeleo ndani na Nje ya Nchi ili kuifanya huduma hiyo iwe endelevu na kuwapa Wananchi wake kujikita katika shughuli za Maendeleo badala ya kusaka Maji.
Akigusia uimarishaji wa Sekta ya Elimu katika kipindi cha Miaka Mitatu Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda alisema huduma za Maabara ziliboreka kwa Ujenzi wa Majengo Mapya yaliyokwenda sambamba na utiaji wa Vifaa vya Maabara kwa Skuli za Sekondari za Kitope na Fujoni.
Alisema uimarishaji huo wa Maabara ulizingatia mfumo wa kuwajengea uwezo wa ufahamu Wananfunzi wa Skuli hizo za Sekondari wa Jimbo hilo katika kumudu vyema masomo yao.
Alifahamisha kwamba Jengo kongwe la Skuli ya Msingi ya Mahonda lilokuwa limechakaa na kutoa sura isiyopendeza lilimsononesha na kufikia hatua ya kulifanyia Matengenezo makubwa yaliyojumisha pamoja na upatikanaji wa Vikalio vipya.
Katika kuunga mkono nguvu za Wananchi Balozi Seif  aliamua kuweka mwega katika Sekta hiyo ya Elimu kwa kusaidia Wananchi hao walioanzisha Majengo mapya ya Skuli katika maeneo yao kwa kuwapatia uwezeshaji wa fedha na Vifaa kukamilishia Miradi yao.
Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda aliwaeleza Wajumbe wa Mkutano huo wa Jimbo kwamba bado zipo changamoto za Huduma za Maji safi,Umeme na Bara bara ambazo Uongozi wa Jimbo hilo utaendeleza juhudi za kuzikabili kila inapopatikana fursa ya kuzitatua.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mahonda Mheshimiwa Bahati Abeid  Nassir  akiwasilisha Utekelezaji wa Ilani kwa Mwaka 2016 hadi 2019 alisema tatizo la huduma za Maji safi na salama lilikuwa sugu, lakini kutokana na jitihada kubwa zilizochukuliwa na Uongozi kwa kushirikiana na Wananchi changamoto hiyo imepunguwa kwa asilimia kubwa.
Mh. Bahari alisema ahadi alizozitoa wakati wa Kampeni ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 anatarajia kuzitekeleza kwa nguvu zake zote ndani ya kipindi cha Miaka Mitano huku akiamini kwamba wasaidizi wake wataendelea kumpa ushirikiano.
Alisema utekelezaji wa ahadi ya Upatikanaji wa Magari Mawili ya kubebea Wagonjwa ndani ya Jimbo la Mahonda katika Sekta ya Afya imeanza kutekelezwa katika Awamu ya kwanza kwa Gari ya kwanza  itakayohudumia Wananchi wa Wadi zote.
Mheshimiwa Bahati alifahamisha kwamba Gari ya Pili ya Kubebea Wagonjwa itapatikana kabla ya Mwaka 2020 ambapo kuamilika kwake kutatoa fursa ya matumizi kwa Wadi zote mbili zilizomo ndani ya Jimbo la Mahonda.
Jimbo la Mahonda liliomo ndani ya  Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa Kaskazini Unguja ni miongoni mwa Majimbo 58 ya Uchaguzi yaliyopo Unguja na Pemba ambalo limepata mafanikio makubwa kufuatia utekelezaji wa kasi wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kuanzia Mwaka 2016/2019.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.