Habari za Punde

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora akabidhi Ofisi

 Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma  na Utawala Bora Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman akiweka saini wakati alipokuwa akikabidhiana Ofisi na Waziri wa Katiba na Sheria  Waziri Khamis Juma Mwalim 


Na Raya Hamad OR-UUB

Mashirikiano na uaminifu unaendana na uwajibikaji  wa kazi ndio siri ya mafanikio  katika kukuza ufanisi na kuleta maendeleo endelevu pia  kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza mahali popote na wakati wowote hatimae kuwa na maamuzi sahihi kwa maendeleo na mustakabali mwema wa kazi

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma  na Utawala Bora Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman ameyasema hayo wakati wa makabidhiano kufuatia mabadiliko yaliyofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dk Ali Mohamed Shein ambapo Wizara iliyokuwa Ofisi ya Rais Katiba  Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora  imegaiwa mara mbili .

Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora inaongozwa na Waziri Haroun  Ali Suleiman , Katibu Yakout Hassan Yakout na Naibu Katibu Seif Shaaban Mwinyi kwa upande wa  Wizara ya Katiba na Sheria  inaongozwa na Waziri Khamis Juma Mwalim , Katibu Mkuu ni George Kazi
Waziri Haroun amesisitiza baadhi ya  mambo ya msingi ambayo bado yanahitaji kusimamiwa ikiwemo Sheria ya Mufti ambayo bado haijakamilika na kusisitiza kufanyiwa kazi ili kikao kijacho cha Baraza la Wawakilishi iweze kusomwa kwa mara ya kwanza.
Aidha amemkumbushia Waziri wa Katiba na Sheria kuwa kwa nafasi yake anakuwa  Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wawakilishi, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa  inayoshughulikia masuala ya Udhalilishaji, Mjumbe wa Kamati ya Kupambana na Dawa za Kulevya .
Akitoa shukurani zake kwa Watendaji wa iliyokuwa  Ofisi ya Rais Katiba  Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora  Waziri wa Katiba na Sheria  inaongozwa na Waziri Khamis Juma Mwalim  amesema mashirikiano  ya pamoja na uwajibikaji kwa wote ndio siri ya mafanikio ambayo yamelekea kuleta ufanisi katika kazi katika kipindi chote kabla ya kugaiwa kwa Wizara
Ndugu Khamis pia amemshukuru Waziri Haroun na kuelezea kuwa alitumia muda ili kupata ushauri na maelekezo katika masuala ya kazi , Jimbo  na hata familia “ nilifanya hivyo kwani Mwalim Haroun ni mkongwe na ni shina la mti wa mafanikio  ambae ana hikima na busara na nashukuru hakuwa mchoyo kunifahamisha, kuniongoza,  kuniendeleza na kunipa ushauri ”alisisitiza
Ameahidi kudumisha na kuendeleza mshikamano na  viongozi pamoja na wafanyakazi kushirikiana kufanya kazi kwa pamoja na kutekeleza majukumu yaliyopo na kuandaa taratibu na mipango imara ya uwajibikaji kwa maslahi ya Taifa
Nae Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria ndugu George Kazi ameahidi kusimamia mfumo wa Katiba na Sheria na kuahidi kushirikiana na watendaji na wafanyakazi na kila mmoja kuwajibika ipasavyo pamoja na  kutekeleza na kusimamia vyema  Ilani ya Chama Cha Mapinduzi
Akitowa shukurani kwa niaba ya wafanyakazi na watendaji wote Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Bi Fatma Moh’d  suala la mashirikiano ni muhimu kwa sekta zote kwani haiwezekani  kuwa na  utawala bora bila ya kuwa na sheria , Uwazi na Uwajibikaji “ tunafanya yale ya muhimu na wajibu ili Zanzibar itawalike hivyo basi nakuahidini tutawakaguwa nyote hata kama tuko nyumba moja kama sheria na Katiba ya nchi inavyoeleza” alisisitiza 
Aidha Katibu wa Mufti Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga  ambae nae alitowa  wasia mfupi kwa kusema  ufanisi hauwezi kupatikana isipokuwa kwa juhudi kubwa na Taufiq haipatikani isiokuwa kwa Allah hivyo ni wajibu wetu sote kumuomba sana Mwenyezi Mungu .  
Viongozi hao wote kwa pamoja wamemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dk Ali Mohamed Shein juu ya namna anavyosimamia Utawala bora  na pia  kuwaamini na kuwateuwa kuwa viongozi katika Taasisi hizo

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.