Habari za Punde

Mapendekezo Bajeti ya Serikali 2019/2020 Kuzingatia Mpango wa Maendeleo wa Taifa


Na: Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa mapendekezo ya Bajeti ya Serikali yanazingatia Mpango wa Maendeleo wa Taifa sanjari na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi.

Amesema hayo leo Bunge jijini Dodoma alipokuwa akiwasilisha Hotuba ya Mapitio na Mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2019/2020.

"Mpango wa Maendeleo wa  Taifa unatekelezwa sanjari na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 - 2020, ahadi za Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na zile alizozitoa katika hotuba yake ya kuzindua Bunge hili mwezi Novemba, 2015." amesema  Waziri Mkuu Majaliwa.

Amesema, vipaumbele vya mpango wa mwaka 2019/2020 ni kuendelea kuimarisha msingi wa uchumi wa viwanda, kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu, kuendelea kuboresha mazingira wezeshi kwa uendeshaji  wa biashara na uwekezaji na kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa mpango.

Aidha amesema kuwa, katika Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya mwaka 2019/2020, Serikali itaendelea kutekeleza Mradi wa Umeme wa Maji wa Mto Rufiji (Stiegler's Gorge), ujenzi wa miundombinu ya reli ya kisasa (SGR), barabara pamoja na kukuza sekta ya anga.

Utekelezaji wa miradi hiyo ya miundombinu wezeshi ya kiuchumi una lengo la kufungamanisha ukuaji wa sekta hizo na sekta nyingine hususan za biashara, kilimo na utalii.

Waziri Mkuu amesema kuwa, kuimarika kwa sekta hizo kutachochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Wananchi kwa ujumla
Ameendelea kusema, katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli yamepatikana mafanikio mengi ambayo wananchi wanapaswa kufahamishwa.

Amesema, Mhe. Rais Magufuli ameonesha dhamira ya dhati ya kisiasa katika kujenga msingi wa uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea. Halikadhalika, ameweza kuhakikisha dhamira hiyo ya kujenga uchumi imara usiyo tegemezi inaenea kwa viongozi wengine, watendaji na wananchi kwa ujumla.

Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni kuendelea kukua na kuimarika kwa uchumi ambao unachochewa na jitihada za Serikali za kuwekeza kwenye miundombinu ya usafirishaji ikiwemo ujenzi wa barabara, reli, viwanja vya ndege sanjari na kutengemaa kwa upatikanaji wa nishati ya umeme.

Ameongeza kuwa kuimarika kwa Shirika la Ndege Tanzania ni sehemu ya mafanikio hayo, ambapo Serikali imefanikisha ununuzi wa ndege saba mpya ikiwemo Dreamliner Boeing 787.

Ununuzi wa ndege hizo umesaidia kuitangaza nchi, kuongeza mapato ya Serikali, fursa za ajira kwa vijana na kuwa kichocheo kwa Sekta za ajira kwa vijana na kuwa kichocheo kwa sekta nyingine kama vile kilimo, utalii, mifugo na uvuvi.

Vilevile, mpango wa elimu msingi bila malipo umesaidia kuongezeka idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa kutoka wanafunzi milioni 1.57 mwaka 2015 hadi milioni 2.08 mwaka 2016 sawa na ongezeko la asilimia 35.2 kwa mwaka  2019 uandikishaji ulikuwa milioni 1.58.

Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuimarisha uchumi na mafanikio yanayoonekana, ambapo katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2018, Pato la Taifa lilikuwa kwa asilimia 6.7 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2017.

Ukuaji huo wa uchumi umechangia kutoa ajira na kuongeza mapato ya Serikali yaliyowezesha ujenzi na uboreshaji wa miundombinu kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na kijamii. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.