Habari za Punde

TUJITOKEZE KWA WINGI KUISHANGILIA TWIGA STARS-MAJALIWA

Na.Khadija Mussa            

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wajitokeze kwa wingi kesho katika uwanja wa Taifa kuishangilia timu ya Twiga Stars ili ishinde kwa mabao mengi na kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga hatua inayofuata.

Amesema viingilio vya mchezo huo vimepunguzwa, ambapo wanawake watalipa sh. 500 tu na wanaume ni sh. 1,000, lengo ni kutoa fursa kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Aprili 4, 2019) wakati akiwasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2019/2020.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwatakia maandalizi mema na ushindi Twiga Stars katika mchezo wao wa kesho tarehe 5 Aprili 2019 dhidi ya timu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Mashindano hayo yanalenga kuwania kufuzu michuano ya Olimpiki mwaka 2020 huko Tokyo, Japan.

“Vilevile, niwatakie kheri, maandalizi mema na ushindi timu zetu zote ikiwemo Serengeti Boys katika mashindano ya AFCON - U17, Taifa Stars katika mashindano ya AFCON huko Misri Juni 2019 na Klabu ya Simba katika hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa Barani Afrika.”

Kwa upande wa riadha, Waziri Mkuu amesema timu ya Tanzania hivi sasa inashiriki michezo ya riadha nchini Rwanda. “Ni matarajio yetu kwamba timu hiyo ya riadha itarejea nyumbani na medali za kutosha. Tunawatakia ushiriki mwema na mafanikio katika mashindano hayo.”

Taifa Stars

Waziri Mkuu amewapongeza wachezaji timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), viongozi, benchi la ufundi, kamati za uhamasishaji wa ushindi, mashabiki na Watanzania wote kwa kutimiza ndoto ya muda mrefu ya kushiriki michuano hiyo mikubwa kabisa Barani Afrika.

Amesema itakumbukwa kwamba imepita takriban miaka 39 tangu Tanzania ishiriki kwa mara ya mwisho michuano ya mpira wa miguu kwa nchi za Bara la Afrika maarufu kama AFCON.

“Hata hivyo, kusubiri huko kulikoma tarehe 24 Machi 2019 baada ya vijana wetu wa Taifa Stars kupata ushindi mnono wa mabao matatu bila majibu dhidi ya jirani zetu wa Uganda. Ushindi huo, unaipeleka Taifa Stars katika AFCON 2019 huko nchini Misri.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa viongozi, wachezaji na walimu wafanye kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye michezo iliyotangulia ili kujiweka sawa na michuano ya Juni 2019.

Waziri Mkuu amewataka wachezaji hao pamoja na viongozi wao watambue  kwamba lengo la Serikali ni kwenda kushindana na si kushiriki. “Niwatakie maandalizi mema na mafanikio katika michuano hiyo inayokuja.”

Akizungumza kuhusu Serengeti Boys, Waziri Mkuu amesema endapo itaibuka na ushindi katika michezo yake miwili itakuwa imekata tiketi ya kushiriki mashindano ya dunia huko nchini Brazil kwa vijana wa umri huo.

Pia, Waziri Mkuu ameipongeza timu ya vijana wenye ulemavu wa akili kwa kuibuka na ushindi wa medali 15 katika Michezo Maalumu ya Olimpiki iliyohusisha riadha na mpira wa wavu iliyofanyika Machi 2019 Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mwakinyo

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza mwanamasumbwi wa Kitanzania, Hassan Mwakinyo kwa kuendelea kuwa mfano bora kwenye tasnia hiyo ya masumbwi.

“Tarehe 23 Machi 2019 Mwakinyo aliendelea kung’ara katika anga za masumbwi na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania baada ya kumtwanga mpinzani wake Muargentina Sergio Gonzalez, huko Nairobi.”

Hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa vyama vya michezo nchini viendelee kuwalea vema wanamichezo hususan vijana ili waweze kuipaisha bendera ya Tanzania kwenye medani mbalimbali za michezo ndani na nje.

Simba

Waziri Mkuu amesema, kwa muda mrefu vilabu vya mpira wa mguu nchini vimekuwa havifanyi vizuri katika medani ya michuano ya Klabu Barani Afrika, hivyo huu ni wakati wa kila Mtanzania kuthamini michezo na kutambua kuwa michezo ni ajira na michezo inalipa.

Waziri Mkuu amesema katika msimu wa 2018/2019 Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam imeweza kulitoa Taifa kimasomaso baada ya kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Amesema kufanya vizuri kwa Klabu ya Simba kunaongeza uwezekano wa Tanzania kupatiwa nafasi nyingine mbili na kufanya jumla ya vilabu vinne vitakavyoshiriki mashindano hayo makubwa ya vilabu Barani Afrika katika misimu ijayo. 

Vilevile, Waziri Mkuu amesema ushindi wa Taifa Stars na Simba una manufaa makubwa kwa nchi yetu yakiwemo kuitangaza vyema nchi na kufungua fursa za ajira kwa vijana wetu hususan wanaojihusisha na soka.

“Nitumie fursa hii kuwapongeza wachezaji, viongozi, benchi la ufundi na mashabiki wote wa Klabu ya Simba kwa mafanikio hayo makubwa. Tupo pamoja nanyi.”

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
 41193 – Dodoma, 
                    
ALHAMISI, APRILI 4, 2019.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.