Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi, alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo leo 11/4/2019.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amesisitiza kuwa wakati Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inatimiza miaka 55 ni vyema misingi ya Muungano ikaendelezwa ikiwa ni pamoja na
kuiimarisha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo Ikulu mjini Zanzibar, wakati alipofanya mazungumzo na Profesa
Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
aliyefika Ikulu ikiwa ni pamoja na kupokea maelekezo na miongozo kutoka kwa
Rais kufuatia kuteuliwa kushika wadhifa huo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli hivi karibuni.
Katika maelezo yake Rais
Dk. Shein alieleza kuwa ni miaka 55 ambayo inatimia rasmi mnamo Aprili 26 mwaka
huu tokea kuasisiwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao viongozi wake
walioasisi Muungano huo Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na Marehemu Julius
Kambarage Nyerere waliweka misingi madhubuti.
Hivyo, Rais Dk. Shein
alisisitiza haja ya kuimarishwa na kuendelezwa misingi hiyo ambayo leo
umeupelekea Muungano wa nchi mbili hizo kuwa imara, madhubuti sambamba na
kuleta maendeleo endelevu kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alieleza kuwa miongoni
mwa misingi hiyo ni pamoja na mashirikiano katika masuala mazima ya diplomasia
ikiwa ni pamoja na mashirikiano na mataifa ya nje chini ya taasisi inayohusiana
na Mambo ya Nje ambayo kwa hivi sasa ni
Wizara hiyo ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Rais Dk. Shein alieleza
kuwa Wizara hiyo ina umuhimu mkubwa katika kuendeleza masuala ya kidiplomasia
hivyo mashirikiano ya pamoja yanahitajika kwa pande zote mbili za Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ili liweze kufikiwa lengo lililokusudiwa.
Aliongeza kuwa azma ya
Wizara hiyo kuanzisha utaratibu wa kubadilishana uzoefu kati ya watendaji wa
Wizara hiyo wa upande wa Zanzibar na wale wa Tanzania Bara kuja Zanzibar
kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupanua wigo wa kiutendaji na mashirikiano.
Aidha, Rais Dk. Shein
alimpongeza Profesa Kabudi kwa kuteuliwa na kukubali kushika wadhifa huo na kusisitiza
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi wake chini ya uongozi wake
wataendelea kumpa mashirikiano ili Wizara hiyo iendelee kufanya kazi zake kwa
ufanisi mkubwa zaidi.
Rais Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kupongeza mashirikiano yaliopo kwa uongozi na watendaji wa Wizara
hiyo na kueleza kuwa hatua hiyo ndio siri kubwa ya mafanikio ambayo yamefikiwa
na yale yanayotekelezwa katika kuimarisha diplomasia ya uchumi.
Nae Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi alimueleza
Rais Dk. Shein kuwa Wizara hiyo mbali ya kujikita na masuala ya mahusiano na
mataifa ya nje pia ni sikio na jicho la mambo yote yanayohusu Muungano na yale yasiyohusu
Muungano kutokana na umuhimu wake.
Profesa Kabudi
alitumia fursa hiyo kutoka pongezi kwa Rais Dk. Shein pamoja na Rais Dk. John
Pombe Magufuli na Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu
Hassan kwa kumuamini kushika wadhifa wa kufanya kazi hiyo ya uwaziri katika
Wizara hiyo.
Waziri Kabudi aliongeza
kuwa kuna kila sababu ya kuiendeleza misingi ya Muungano ambao unatimiza miaka
55 mnamo Aprili 26 mwaka huu ambapo misingi hiyo imeleta mafanikio na maendeleo
makubwa kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri huyo alieleza
mikakati iliyowekwa na Wizara yake ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu kati
ya watendaji wa Ofisi ndogo ya Zanzibar na Makao Makuu ya Wizara hiyo kwa lengo
la kupanua wigo na kuimarisha utendaji.
Profesa Kabudi
alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa ataendelea kushirikiana na viongozi wote wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake kwa azma ya
kuendeleza na kuimarisha malengo ya Wizara hiyo sambamba na kutekeleza misingi
ya Muungano.
Pamoja na hayo, Waziri
huyo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alimueleza Rais Dk.
Shein mchakato uliopo hivi sasa wa kuandaa Sera ya Diaspora ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ambayo itapata msaada mkubwa kutoka Sera ya Diapora ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo imeshaundwa.
Pia, Waziri huyo
alieleza hatua zinazoendelea katika ujenzi wa Ofisi ya Ubalozi pamoja na nyumba
ya Balozi wa Tanzania huko Mascat nchini Oman ikiwa ni miongoni mwa kuimarisha
uhusiano na ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na nchi hiyo.
Sambamba na hayo,
Waziri huyo alipongeza maendeleo yaliyofikiwa Zanzibar hasa katika sekta za
afya, elimu, maji, miundombinu, utalii na uwekezaji hasa kwa wawekezaji wazawa
ambao wamewekeza hapa Zanzibar ukiwemo mradi wa mji mpya wa Fumba.
Pia, Waziri Kabudi alipongeza
juhudi zilizofikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuendeleza na
kuimarisha sekta ya utalii ambapo hivi sasa Zanzibar imekuwa kivutio kikubwa
cha watalii kutoka maeneo mbali mbali duniani likiwemo eneo la Masharki ya Kati.
Wakati huo huo, Rais
Dk. Shein alimuonesha Profesa Kabudi
chumba maalum kilichotumika kwa hatua za awali na viongozi waasisi wa
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa ajili ya kutiaji saini makubaliano ya Muungano.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment