Habari za Punde

Sherehe za Mahafali ya 29 ya Skuli ya Sekondari ya Ufundi Mikunguni.

Katika kuhakikisha maendeleo na ufaulu mzuri wa wanafunzi unapatikana, Mashirikiano ya pamoja baina ya Walimu, Wazazi, Walezi na Wanafunzi yanahitajika ili kufikia malengo hayo.
 Akizungumza katika sherehe ya mahafali ya 29 ya Skuli ya Sekondari ya Ufundi Mikunguni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Riziki Pembe Juma, amesema mashirikiano mazuri ndio chanzo cha mafanikio katika sekta ya Elimu.
 Amesema ni lazima Walimu kuhakikisha wanatumia mbinu mbalimbali na ubunifu katika kazi zao ili kuongeza idadi kubwa ya ufaulu kwa wanafunzi wao.
 Mhe Riziki amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imefuta michango yote katika Skuli zenye kutoa Elimu ya lazima ili jamii nzima iweze kufaidika na matunda ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 ili taifa liwe na wasomi bora.
 Aidha Waziri huyo amewataka Wanafunzi kupambana katika masuala mazima ya vitendo vya udhalilishaji hasa kwa wanawake ili kulinda  heshima yao pamoja na kudumisha mila na utamaduni wa nchi.
Akizungumzia juu ya suala la ufaulu, Mhe Riziki ameiopongeza Skuli hiyo ya Sekondari ya ufundi Mikunguni kwa kushika nafasi ya 6 katika Mkoa wa mjini Magharibi pamoja na kushika nafasi ya 328 kati ya Skuli 3488 Kitaifa.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dkt. Idrissa Muslim Hija amesema Wizara imeandaa mradi maalum kwa ajili ya kuifanyia matengenezo Skuli hiyo ya Sekondari ya ufundi Mikunguni pamoja na kujengwa jengo la kisasa lenye hadhi na liendane na taaluma inayotolewa katika Skuli hiyo.
Mapema akisoma risala yao mwanafunzi aliehitimu Faridi Mwinyi Ramadhan kwa niaba ya wanafunzi wenziwe, wameiomba Wizara kuwasaidia tatizo la upungufu wa madarasa kutokana ongezeko la idadi ya Wanafunzi pamoja na kupatiwa vifaa vipya vya maabara kwani vilivyopo ni chakavu, pamoja na kutaka  kupatiwa Walimu wa masomo ya Ufundi.
Katika mahafali hiyo Mhe Riziki  amewapatia zawadi  Walimu na kuwapatia vyetu Wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.