Habari za Punde

Wazazi na walezi waashauriwa kushirikiana na Walimu kutatua matatizo yanayowakabili

Wilaya ya magharibi B.                  
Wazazi na Walezi wa Al-madrasatul-Arshi iliopo Fuoni Kigorofani wamewashauriwa kushirikiana na Waalimu katika kutatua matatizo yanayowakabili ili  kupeleka mbele Kitabu cha Mwenyezi Mungu.
Ushauri huo umetolewa na Diwani wa Kuteuliwa Wilaya ya Magharibi B Thuwaiba Jeni Pandu wakati alipokuwa katika hafla ya Maulid ya kuzaliwa Bwana Mtume Muhammad (S.A.W) iliofanyika huko Fuoni Kigorofani Wilaya ya Magharibi B.
Amesema uongozi wa madrasa hiyo unakusudia kujenga jengo jipya na la kisasa ili kuondosha msongamano wa wanafunzi lakini bila kuwepo kwa mashirikiano jambo hilo halitoweza kufanikiwa.
Aidha amewaomba Viongozi wa Madrasa hiyo kuweka vikao vya mara kwa mara na Wazazi ili kukaa pamoja na kujadili mapungufu yaliopo na kuweza kuyapatia ufumbuzi.
Pia amewakumbusha Wazazi kuwalea watoto wao katika maadili mema na kuchukuwa bidii ya kudurusu masomo kwa faida yao na Taifa kwa ujumla.
Nae Mwalimu Mkuu wa Madrsa hiyo Mila Kesi Ameir amesema wanakabiliwa na matatizo ikiwemo ya Udogo wa eneo la kufundishia,Uhaba wa vitendea kazi kama vile Vitabu,Misahafu na Vijuzuu mambo ambayo yanarudisha maendeleo ya Madrasa hiyo.
Hata hivyo amewaomba Wafadhili na Watu wenye uwezo kuwasaidia kwa hali na mali ili wapate kusomesha katika Mazingira yanayoridhisha na kufikia lengo la kupeleka mbele Elimu ya Dini ya Kiislam.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.