Habari za Punde

Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa Akutana na Spika wa Bunge la Misri Dkt. Ali Abdel Aal.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Spika wa Bunge la Misri, Dkt. Ali Abdel Aal kabla ya mazungumzo yao, ofisini kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Spika wa Bunge la Misri, Dkt. Ali Abdel Aal, ofisini kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma, Aprili 3, 2019.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Misri Dkt. Ali Abdel Aal ambapo ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka Misri waje nchini wawekeze kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda, kilimo, utalii na madini.

Amekutana na Spika huyo na ujumbe wake leo (Jumatano, Aprili 3, 2019) katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma. Amesema Tanzania na Misri zina uhusiano wa kihistoria kuanzia enzi za Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa pili wa nchi hiyo Gamal Abdel Nasser.

Pia, Waziri Mkuu amesema ushirikiano wa nchi hizo mbili umeendelea kuimarika na umedhihirishwa na viongozi wakuu wa Misri, Rais Abdel Fattah El Sisi pamoja na Waziri Mkuu Dkt. Mostafa Madbouly ambao kwa nyakati tofauti walifanya ziara nchini Tanzania.

“Ziara hii ya Spika wa Bunge la Misri inazidi kuimarisha uhusiano wetu. Pia ziara ya Spika pamoja baadhi ya wabunge inatoa nafasi ya kubadilishana uzoefu pamoja na namna ya kuendesha mabunge na wabunge kujifunza kutoka kila upande.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali imedhamiria kuendeleza sekta ya viwanda nchini ili kukuza uchumi na kufikia wa kati ifikapo 2025, hivyo amewakaribisha wawekezaji wa sekta mbalimbali waje wawekeze katika viwanda vya madini, dawa za binadamu na mifugo.

Waziri Mkuu amesema Serikali iko tayari kuwasaidia wawekezaji wote wanaokusudia kuwekeza nchinina kwamba Tanzania inazo fursa nyingi za uwekezaji ikiwemo ardhi ya kutosha, upatikanaji wa malighafi  na za uhakika. “Pia Tanzania ni nchi ya amani na utulivu,” alisisitiza Mheshimiwa Majaliwa.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Tanzania ina vivutio vingi vya utalii ikiwa ni pamoja na uwepo wa mlima Kilimanjaro, visiwa vya Zanzibar, mbunga zenye wanyama wa aina mbalimbali na fukwe nzuri, hivyo amewakaribisha watalii kutoka nchini Misri waje nchini na kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Misri Dkt. Ali Abdel Aal amesema nchi yao iko tayari kushirikiana na Tanzania katika mkakati wake wa kukuza uchumi kupitia mashirika na kampuni mbalimbali zitakazokuja kuwekeza katika miradi mikubwa.
“Tupo tayari kutoa wataalamu wa ujenzi wa miradi mikubwa ya miundombinu yakiwemo madaraja, barabara kwa kuwa wanauzoefu wa ujenzi wa miradi hiyo kwani tayari wameshaitekeleza katika nchi yao.
Pia, kiongozi huyo amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba nchi ya Misri iko tayari kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za matibabu, kilimo na mifugo.
Hata hivyo, Spika huyo ameiomba Serikali iwasaidie wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Misri waje nchini kuanzisha viwanda na kwamba watakikisha wanatoa ajira kwa wananchi pamoja na kuimarisha huduma za jamii katika eneo husika. “Sisi kampuni zetu zikija zitafanyakazi kama wenyeji.”
Akizungumzia kuhusu mradiwa umeme wa maporomoko ya maji ya Mto Rufiji (RHPP) unaojengwa Kampuni ya Arab Contractors na Elsewedy Electric zote kutoka nchini Misri, Spika huyo wa Bunge la Misri amesema atahakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.

Pia kiongozi huo ameishukuru Tanzania kwa kuwakaribisha Wamisri waje wawekeze nchini na kwamba amevitiwa na Tanzania, hivyo ameahidi yeye pamoja na familia yake atakuja nchini kwa ziara binafsi yenye lengo la kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
 41193 – Dodoma,  
                    

JUMATANO, APRILI 3, 2019.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.