Habari za Punde

Dk.Shein Asisitiza Suala Zima la Amani na Utulivu Ndio Msingi wa Maendeleo Kila Mmoja Anapaswa Kuilinda.


Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe. Hassan Khatib Hassan akitowa shukrani kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, baada ya kumalizika kwa hafla ya Futari aliowaandalia Wananchi wa Kusini Unguja katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa Tunguu Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein amefutari pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja na kuwataka waumini wa dini ya Kiislamu kuzidisha ibada na upendo katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani.

Hafla hiyo ya futari iliyoandaliwa na Rais Dk. Shein kwa ajili ya wananchi wa Mkoa huo wa Kusini Unguja ilifanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Tunguu, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja na kuhudhuriwa  na viongozi mbali mbali wa Serikali, dini, vyama vya siasa pamoja na wananchi wa Mkoa huo.

Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya Rais Dk. Shein, Mkuu wa Mkoa huo Hassan Khatib alisisitiza kuwa mwezi Mkutukufu wa Ramadhani ni mwezi wa kuzidisha ibada na upendo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanaofunga wanapata futari.

Aliongeza kuwa kuzidisha ibada na upendo katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani ndio njia moja wapo ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu sambamba na kuufanyia wema mwezi huo ambao una rehma nyingi ndani yake.

Aidha, alisisitiza suala zima la amani na utulivu ndio msingi wa maendeleo hivyo kila mmoja anapaswa kuilinda na kuiendeleza kwa nguvu zake zote.

Alieleza kuwa maendeleo yote yaliopatikana katika Mkoa huo yanatokana na kuwepo kwa amani, utulivu na upendo mkubwa ambayo ndio chachu ya mafanikio.

Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya wananchi Mkuu wa Mkoa huyo alimpongeza Rais Dk. Shein na Serikali anayoiongoza kwa azma yake ya ujenzi wa barabara katika Mkoa huo ikiwemo barabara ya Charawe na Ukongoroni itakayojengwa kwa kiwango cha lami itakayoanzia Jozani, ujenzi unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Sambamba na hayo, wananchi wa Mkoa huo pia, wamefurahishwa na ahadi ya Rais Dk. Shein aliyoitoa katika ziara yake aliyoifanya katika Mkoa huo mwezi Februari mwaka huu ya ujenzi wa daraja kati ya kisiwa cha Uzi na Unguja Ukuu kwa lengo la kurahisisha usafiri wa barabara hali ambayo itaondosha usumbufu wa usafiri kwa wananchi wa kisiwa hicho iliyodumu kwa muda mrefu.

Pia, Mkuu huyo wa Mkoa alieleza kuwa wananchi wa Mkoa huo wameendelea kupata mafanikio makubwa kutokana na amani iliyopo hatua iliyopelekea kupungua kwa matukio kadhaa mabaya yakiwemo udhalilishaji wa wanawake na watoto pamoja na kutokuwepo kwa ajili za barabarani katika kipindi hichi Mkoa humo.

Wananchi wa Mkoa huo walitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa kuendeleza utamaduni wake huo wa kufutari nao pamoja katika mwezi mtukufu wa Ramadhani na kumuombea dua kwa Mwenyezi Mungu ili azidi kumpa afya, nguvu na uzima yeye na Aila yake ili waungane nae tena katika mwezi wa Ramadhani wa mwakani.

Alhaj Dk. Shein aliwatakia Ramadhani njema wananchi wa Mkoa huo na kuwasisitiza kuutukuza mwezi huu mtukufu wa Ramadhan kwa kusoma sana Qur-an kwani ndio mwezi ulioshuka kitabu hicho kitakatifu.

Dk. Shein aliwataka wananchi wa Mkoa huo kuendelea kushirikiana na kupendana sambamba na kuwa wamoja na kuwataka kuachama na mambo yote yaliyokatazwa ndani ya mwezi huu na miezi mengineyo ili waendelee kupata neema za Allah.

Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein aliwashukuru wananchi wote waliohudhuria katika futari hiyo aliyowaandalia na kupongeza jinsi walivyoonesha upendo mkubwa kwake wa kukubali muwaliko wake huo.

Wakati huohuo, nae Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein kwa upande wake aliungana na viongozi wanawake wa kitaifa pamoja na wananchi wa Mkoa huo wa Kusini Unguja katika futari hiyo maalum aliyoianda Rais Dk. Shein.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.