Habari za Punde

RC Wangabo awataka Ma DC kufanya kazi usiku na mchana kutekeleza maagizo ya Serikali

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia) akiongozana na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda (Kushoto) baada ya kutoka katika jengo la OPD linaloendelea kujengwa katika kukamilisha ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Nkasi. 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa maelekezo kwa mafundi (hawapo pichani) aliowakuta wakiendelea na ujenzi wa Hospitali ya wilaya ya Nkasi. 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akisaidia kuweka mchanganyiko wa Zege katika ndoo ya mmoja wa mafundi wanaoendelea na kuweka jamvi katika moja ya majengo ya hospitali ya Wilaya ya Kalambo wakati alipofanya ziara ya kuona maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo. 

 Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Bi. Julieth Binyura akipokea ndoo ya zege kutoka kwa mmoja wa kinamama aliyeajiriwa kama kibarua katika ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kalambo. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akimpa mama lishe fedha kuwalipia chakula kinamama vibarua katika ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kalambo. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka Wakuu wa za wilaya zinazotekeleza ujenzi wa hospitali za wilaya kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kuweza kukamilisha ujenzi huo kwa wakati ikiwa ni kutekeleza kwa ufanisi maaagizo ya serikali juu ya ukamilishwaji wa ujenzi wa hospitali hizo.
Amesema kuwa hakurudhishwa na maendeleo ya ujenzi wa hospitali mbili za Wilaya ya Nkasi pamoja na Wilaya ya Sumbawanga huku akipongeza ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kalambo kwa kupiga hatua tofauti na alivyodhania tangu alipotembelea katika eneo hilo la ujenzi wiki tatu zilizopita.
“Katika Wilaya hii ya Kalambo hali ya Ujenzi nikilinganisha na nilivyofika hapa tarehe 19 mwezi wa nne ilikuwa hali ni mbaya, kwasababu mvua zilikuwa zinanyesha magari yalikuwa hayapiti kuja hapa kwa hali hiyo hata vifaa mbalimbali vya ujenzi vilikuwa vinashindwa kufika kwa wakati, lakini hali ya leo baada ya mvua kukatika, hakika waefanya kazi kubwa sana kwasababu hawa ndio walikuwa na changamoto kubwa sana kuliko hospitali zile nyingine mbili, sasa mhandisi fanya kazi hapa usiku na mchana na Mkurugenzi msimamie,” Alisisitiza.
Halikadhalika amewataka wakurugenzi kuhakikisha wanakamilisha malipo ya mafundi ili wasiweze kuzembea na hatimae kujenga chini ya kiwango na kuongeza kuwa wakati wakiendelea kufikia hatua ya usawa wa linta wahakikishe wanaanza kununua vifaa kama milango, mbao kwaajili ya kenchi na mabati tayari kwaajili ya kufikiria hatua ya uwezekaji kwani fedha sio tatizo katika kulifanikisha hilo.
Mh. Wangabo ameyasema hayo alipotembelea hospitali za wilaya tatu ndani ya siku moja kwa kuzunguka zaidi ya kilomita 450 ili kujionea maendeleo ya ujenzi wa hospitali hizo zilizopo katika mkoa huo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh. Suleiman Jafo, kuwa kabla ya tarehe 14 majengo yote ya hospitali hizo yanatakiwa kufikia usawa wa linta.
Aidha, Mh. Wangabo amewataka mafundi wote kuhakikisha hadi kufikia tarehe 12 mwezi Mei wanafikia katika usawa wa linta ili kutekeleza agizo hilo kwa wakati na kuwataka wakuu wa wilaya hao kuwafikisha mafundi watakaoshindwa kufukia hatua hiyo katika kamati za ulinzi na usalama za wilaya ili waweze kujieleza.
Mkoa wa Rukwa unatekeleza ujenzi wa hospitali tatu za Wilaya ambazo tayari zimeshapatiwa shilingi Bilioni 1.5 kila Wilaya kwaajili ya ujezni wa majengo saba ya hospitali hizo ambayo yanatakiwa kumaliza na kuanza kutumika ifikapo tarehe 30 mwezi juni mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.