Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Alhajj Ali Mohamed Shein, akihutubia Baraza la Eid El Fitry katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.
BISMILLAHI RAHMANI RAHIM
Assalam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh
IDD MUBARAK
Kwa hakika, ni wajibu wetu kumshukuru
Mwenyezi Mungu; Subhanahu wa Taala, Mwingi wa Rehema na Utukufu. Mola ambaye kwa rehema na utukufu wake
ametujaaliya neema ya uhai na afya njema tukaweza kuifikia sikukuu hii ya Idd
el Fitr, tukiwa salama na wenye amani na furaha. Kwa mapenzi na rehema zake Allah, tumeweza
kuikamilisha ibada ya saumu ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kuifikia siku hii
ya Idd. Tumsalie na tumtakie rehema na amani Mtume wetu Muhammad (S.A.W), yeye
na ahli zake, Masahaba, Maulamaa na Wafuasi wake wote walioongoka kwa kufuata
mwendo na miongozo yake.
Katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani tulioumaliza
jana, kuna ndugu, jamaa na Waislamu wenzetu ambao tulianza kufunga pamoja nao
na hivi sasa wameshafika mbele ya haki. Kwa hivyo, sisi tulio hai hadi leo,
tunapaswa kuzitafakari rehema za Mwenyezi Mungu kwa mazingatio makubwa.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu awarehemu Waislamu wenzetu wote waliokwishatangulia
mbele ya haki na sisi atujaalie khatma njema.
Kwa baraka za siku hii, namuomba Mola wetu
Mtukufu awape subira wale wote walioondokewa na ahli zao, wazazi, ndugu, watoto
na wahisani ambao walitegemea kula nao sikukuu pamoja. Kadhalika, tunamuomba Mwenyezi
Mungu awajaalie afya njema wagonjwa wetu walioko hospitali na nyumbani. Vile vile, na sisi na familia zetu atujaalie sikukuu
njema na kila lenye kheri. Aizidishie nchi yetu amani na utulivu, na atudumishe
katika mapenzi na mshikamano zaidi baina yetu.
Ndugu
Wananchi,
Natoa salamu zangu za Idd kwenu nyote mliohudhuria
kwenye Baraza hili, wale wanaotufuatilia katika vyombo vya habari, kwa wananchi
na Waislamu wote duniani katika kuisherehekea siku hii. Leo tumekusanyika
katika Baraza la Idd kwenye ukumbi huu wa Marehemu Sheikh Idris Abdulwakil,
tukiungana na Waislamu wote duniani kwa ajili ya kuisherehekea Sikukuu ya Idd
el Fitr. Shughuli hii ilitanguliwa na
sala ya Idd wakati wa asubuhi, ambayo Kitaifa kwa upande wa Zanzibar ilisaliwa katika
viwanja vya Maisara na vile vile, ilisaliwa katika misikiti mbali mbali. Kwa hakika, Mwenyezi Mungu ametuwekea siku
hii, ili iwe ya furaha baada ya kukamilisha utekelezaji wa maamrisho yake ndani
ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Tunamuomba Mola wetu Mtukufu azikubali saumu
zetu tulizozitekeleza pamoja na ibada zote tulizozifanya katika mwezi wa
Ramadhani tukitaraji malipo kutoka Kwake, ikiwa ni pamoja na kutusamehe makosa
yetu mapya na yaliyotangulia kabla. Imepokelewa hadithi ya Mtume wetu Muhammad
(S.A.W), kutoka kwa Imaam Al-Bukhariy na Muslim inayosema:
“Atakayefunga
Ramadhani kwa imani na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake
yaliyotangulia”.
Inshaallah Mwenyezi Mungu, atujaalie tuwe ni
miongoni mwa watu hao, atulipe fadhila nyingi pamoja na kutusamehe makosa yetu
kwa baraka na utukufu wa mwezi wa Ramadhani.
Ndugu
Wananchi,
Baraza la Idd ni kikao chenye haiba na
umuhimu mkubwa. Haiba ya mkusanyiko huu
inadhihirika katika nyuso zetu za furaha na mavazi yetu ya kupendeza katika
siku hii. Kadhalika, hafla hii inatupa wasaa wa kukutana na ndugu,
jamaa, marafiki na viongozi mbali
mbali, kwa pamoja, ili tuweze kukumbushana na kubadilishana mawazo juu ya mambo
mbali mbali yenye mnasaba na siku
hii, yaliyopita na yaliyopo ambayo yanahusiana na ustawi wa maendeleo ya nchi
yetu.
Ilivyokuwa ni jana tu Mwenyezi Mungu
ametujaalia tumeikamilisha funga ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kwa hivyo, ni
vyema tukaendelea kukumbushana na
kuhimizana juu ya umuhimu wa kuyadumisha tuliyojifunza katika mwezi wa
Ramadhani na tufungamane nayo, ili iwe ni tabia itakayojengeka katika kuyaendesha
maisha yetu. Kwa hakika, tukifanya hivyo ndipo tutakuwa tumehitimu vyema kwenye
mafunzo tuliyoyapata na tutaweza kutimiza lengo la kuumbwa kwetu hapa duniani, ambalo
ni kumuabudu Mwenyezi Mungu mmoja Subhaanahu wa Taala, bila ya kumshirikisha na
chochote. Mwenyezi Mungu ametaja uovu wa kumshirikisha katika aya kadhaa ndani
ya Kitabu Chake kitakatifu cha Qurani, na miongoni mwao ni Aya ya 13 ya Surat
Luqman ambayo tafsiri yake inasema:
“Na
(wakumbushe), Luqmani alipomwambia mwanawe, na hali ya kuwa anampa nasaha. Ewe
mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu maana shirki ndio dhulma kubwa”.
Ndugu
Wananchi,
Katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani tulizidisha
uchamungu wetu kwa kufanya vitendo vingi vyenye kheri. Kama kawaida, ibada zetu
za saumu zilifuatiwa na sala za faradhi na sunna, ambapo misikiti ilifurika
waumini kwa sala na darsa zilizoongozwa na Maimamu, Mashehe na Walimu wetu.
Tulisimama imara kwa umoja wetu bila ya kujali muda katika sala za tarawehe.
Tulijenga mapenzi na huruma kwa kupeana sadaka mbali mbali, kupelekeana vyakula
vya tunu, kuftari pamoja na kusaidiana katika njia za kheri. Tumejifunza mengi
juu ya kuishi kwa umoja na mshikamano.
Vile vile, tuliendeleza kusoma sana Qurani
na tulishuhudia mashindano ya kuhifadhi Qurani yaliyowashirikisha watoto wetu
wa umri tafauti. Kadhalika, waumini wengine waliushindikiza Mwezi wa Ramadhani
kwa kukaa itikafu misikitini. Mambo haya yote yalikuza imani zetu na kumcha
Mwenyezi Mungu. Vile vile, yalituwezesha
kurejesha mwenendo na utamaduni mzuri wa maisha yetu.
Ni dhahiri mambo hayo yote mazuri
tuliyoyafanya yalikuwa ni kwa lengo la kufuata sheria za dini yetu, ili
kutafuta radhi, fadhila na baraka za Mwenyezi Mungu katika Mwezi Mtukufu wa
Ramadhani. Mwenyezi Mungu Inshaallah atutakabalie ibada zetu, ili ziwe ni
sababu ya kupata malipo ya daraja ya juu, kama ambavyo Mwenyewe Azza wa Jalla
alivyotuahidi katika Aya ya 20 ya Suratul Muzammil, ambayo tafsiri yake ni kama
ifuatavyo:
“Na chochote mnachokitanguliza kwa (ajili ya)
nafsi zenu katika mambo ya kheri (basi) mtakikuta kwa Mwenyezi Mungu kikiwa
bora (zaidi) na malipo makubwa (zaidi)”.
Ndugu
Wananchi,
Ibada ya saumu ilitufunza kuwa watiifu kwa
kujiepusha na mambo yote ambayo yangeweza kuzibatilisha funga zetu. Tulijitahidi sana kujiepusha na vitendo vya
dhulma, wizi, kusema uongo, kusengenya na maasi mengine. Mwenendo huu
ulichangia kutufanya tuwe waumini wazuri na raia wema. Kwa hivyo, ili tuongeze ufanisi katika
maendeleo ya jamii yetu, nasisitiza kwamba tuendelee na mwenendo mzuri wa
kutafuta radhi za Mola wetu hata katika miezi mingine baada ya kumalizika kwa mwezi
Mtukufu wa Ramadhani. Bila ya shaka, kuuendeleza
mwenendo huo baada ya mwezi wa Ramadhani ni jambo muhimu, kwani kutaiwezesha
jamii yetu isiwe na vitendo vya uvunjaji wa sheria na ukiukaji wa maadili,
silka na utamaduni tulioachiwa na wazee wetu.
Ndugu
Wananchi,
Mwezi wa Ramadhani ni mwezi mtukufu wenye
ubora wa pekee kwa wanaadamu hasa kwa Waislamu.
Kila Muislamu ana wajibu wa kuuheshimu kutokana na ubora wake. Miongoni
mwa mambo yanayoufanya mwezi wa Ramadhani kuwa bora ni kwamba ndani ya mwezi
huu iliteremshwa Quran tukufu. Mwenyezi
Mungu ametueleza katika Suratul Qadr aya
1 na ya 3, katika tafsiri isemayo:-
1. “hakika
tumeiteremsha (Qurani) katika Laylatul - Qadr (usiku wenye hishima kubwa),
(usiku wa mwezi wa Ramadhani).
3.“huo
usiku wa hishima (huo) ni bora kuliko miezi elfu”.
Kwa
mnasaba wa aya hizi, tunatakiwa tuuheshimu
na tufanye ibada kwa wingi na kwa nia safi,
ili tufaidike na baraka na neema za Mola wetu. Mwenyezi Mungu ameendelea
kuonya juu ya kwenda kinyume na maamrisho yake.
Mwenyezi Mungu ametutaka tutoe neema alizotupa kwa njia ya kutafuta
radhi Zake na tuepukane kabisa kuzitumia neema hizo kwa njia isiyofaa kama
alivyosema katika aya ya 195 ya Suratul Baqarah; yenye tafsiri isemayo:-
“Na
toeni katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo.
Na fanyeni wema, hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema”.
Inasikitisha kuona kwamba pamoja na nasaha
mbali mbali kutoka kwa Mola wetu kuhusu kuzitumia kwa njia sahihi neema
alizotupa, nasaha ambazo sisi waumini tumekuwa tukizikariri, ili kutanabahisha
juu ya kuuenzi mwezi wa Ramadhani, bado tulisikia vikiripotiwa vitendo
viovu vilivyoashiria baadhi ya watu
kutouheshimu mwezi huo. Yaliripotiwa matukio ya wizi madukani unaofanywa na
watu wasio waaminifu. Kuliripotiwa vitendo vya baadhi ya vijana kukutwa
wakivuta sigara mchana hadharani. Vile vile, tumesikia matukio yanayohusiana na
matumizi ya dawa za kulevya. Zaidi ya
yote, bado taarifa za kuendelea kwa vitendo vya ubakaji vilisikika katika mwezi
Mtukufu wa Ramadhani.
Kwa hakika, hayo si mambo ya kuridhisha hata
kidogo. Vitendo vya aina hii sio tu vinaiaibisha jamii yetu, bali, vilevile,
vinakwenda kinyume cha maadili mema
ambayo Mola wetu ametuamrisha tuwe nayo hasa katika Mwezi wa Ramadhani. Natoa wito kwa wananchi wote waviache vitendo
vya aina hio ambavyo ni kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Nawanasihi Mashekhe
na Walimu wetu waendelee kutoa mawaidha juu ya umuhimu wa kuyaheshimu maamrisho
ya Mwenyezi Mungu kwa kufuata mwenendo wa maadili mema na kubainisha madhara ya
kuhalifu maamrisho ya Mola wetu Subhanahu Wataala. Mategemeo yangu ni kuwa nasaha hizo
zitasaidia kuiepusha jamii yetu na mitihani ya aina hio kwa sasa na baadae.
Ndugu
Wananchi,
Nnawanasihi wananchi wenzangu kuwa tunapaswa
tuzitii sheria za nchi yetu, ili na wageni wanaoitembelea nchi yetu waweze kuuiga
mfano wetu, na hatimae tuendelee kuishi katika hali ya salama na amani. Nchi
inayothamini na kufuata misingi ya utawala bora, watu wake huwa na uvumilivu
maalum wa kuishi pamoja katika jamii yenye watu wenye imani tafauti za kidini
na kiutamaduni. Watu wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla, tumekuwa ni kigezo
kizuri miongoni mwa nchi kadhaa duniani katika kuuendeleza ustaarabu huo wa
uvumilivu tangu hapo kale na dahari. Kwa hakika uvumilivu ni miongoni mwa sababu
zinazotuepusha na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe nchini mwetu. Tumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kutupa tunu hii, tutahakikisha kwamba tunailinda amani na
usalama nchini mwetu kwa kila hali.
Ni jukumu letu kwamba kila wakati tutafakari
hali za wenzetu waliokosa amani katika baadhi ya nchi duniani. Tunayaona na tunayasikia
katika vyombo vya habari madhila na
mateso wanayoyapata watu wa nchi hizo. Kuna Waislamu wenzetu ambao wametekeleza
ibada ya saumu katika hali dhalili ya taharuki na unyonge kutokana na tatizo la
kukosa amani na usalama, tena wakiwa katika nchi zao wenyewe. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuepushie mbali na
hayo na wao awaondoshee mtihani huo.
Ndugu
Wananchi,
Kuwepo kwa amani na utulivu nchini
kumetuwezesha kuzidi kupiga hatua za ufanisi za utekelezaji wa mipango yetu
mikuu ya maendeleo ambayo ni MKUZA III, Dira ya Maendeleo ya 2020, Mpango wa
Dunia wa Maendeleo Endelevu na Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya Mwaka
2015-2020. Utekelezaji wa mipango yetu
hio umetuwezesha kupata mafanikio katika ukuaji wa uchumi na uimarishaji wa
huduma mbali mbali. Katika hali hii ya
kupata mafanikio makubwa, tunapaswa tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha
kuyafikia mafanikio haya.
Katika Aya ya 7 ya Suratul Ibrahim, Mwenyezi
Mungu ameahidi kutuzidishia neema tutakapomshukuru aliposema:
“Na
(kumbukeni) alipotoa tangazo Mola wenu (kwamba), iwapo mtanishukuru (kwa neema
nilizokujaalieni), basi nitakuzidishieni (neema hizo); (lakini) iwapo
mtazikufuru (neema hizo) basi hakika adhabu yangu ni kali (kabisa)”.
Kutokana na aya hii, sote tuna wajibu wa kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kuwa na uchumi unaokua mwaka hadi mwaka. Katika
mwaka wa fedha wa 2018 uchumi wetu ulikua kwa asilimia 7.1, kutoka asilimia 7.0
na mfumko wa bei uliendelea kushuka;
kutoka kasi ya asilimia 5.6 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 3.9 mwaka 2018.
Katika kuimarika kwa uchumi wetu, makusanyo ya mapato yameongezeka na kufikia TZS
bilioni 668.70 mwaka 2017/2018 kutoka TZS bilioni 181.48 mwaka 2010/2011. Hii ni sawa na ongezeko la mara 3.7. Kadhalika, pato la mtu binafsi ambalo
lilikuwa TZS 942,000 mwaka 2010, limeongezeka na kufikia TZS 2,323,000 mwaka
2018 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 146.7
Kasi yetu hio ya makusanyo na utekelezaji wa
mipango yetu ya maendeleo, inatupa matarajio ya kukua kwa uchumi wetu kufikia
asilimia 7.8 katika mwaka wa fedha wa 2019/2020. Kwa hivyo hapana shaka kwamba Zanzibar
itafikia nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020, kama ilivyolengwa katika
Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2020.
Mafanikio hayo makubwa tuliyoyapata katika
kuongeza mapato na kukuza uchumi wetu, yametokana na jitihada za pamoja za Viongozi,
Wizara, Washirika wa Maendeleo, Taasisi mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar ikiwemo Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato ya
Zanzibar (ZRB), Wakulima, Wafanyakazi pamoja na wananchi wote kwa jumla. Natoa shukurani kwenu nyote kwa ushirikiano
wenu. Ni dhahiri kuwa tuna wajibu wa
kuongeza bidii katika kutekeleza majukumu yetu, ili tuendelee kupata ufanisi na
kupiga hatua zaidi za mafanikio.
Ndugu
Wananchi,
Historia ya Uislamu inaeleza kwamba katika
matayarisho ya vita vya Taabuk ambavyo jeshi la Warumi lilipanga kupigana na
jeshi la Waislamu, Bwana Mtume Muhammad (S.A.W) aliwatangazia Waislamu
kuchangia, ili kuliongozea nguvu jeshi hilo liweze kuelekea katika mapambano
kwa uhakika na ufanisi.
Tukizingatia mantiki ya historia hii kwa
mnasaba wa maendeleo ya nchi yetu na watu wake, tutaihusisha na ulipaji wa
kodi. Serikali haina uwezo wa kumpa kila
mtu mmoja mmoja pesa za matumizi katika kuendesha maisha yake, ila humlipa
kupitia huduma mbali mbali Serikali inazozitoa kwa wananchi. Kwa hivyo, kila
kiongozi, kwa nafasi aliyo nayo, itamlazimu asimamie suala la ulipaji kodi
pamoja na utoaji wa risiti. Tuendelee kushajiishana juu ya utoaji na uchukuaji
wa risiti, ili kuhakikisha kwamba kila senti inayopaswa kukusanywa na Serikali
inakusanywa. Hata Uislamu umetufundisha haja ya kuandikiana mahali ambapo
miamala ya pesa inafanyika, kwa sababu kuwepo kwa stakabadhi ya maandishi ni
ushahidi madhubuti. Aya ya 282 ya Suratul Baqara inatoa taswira ya mafundisho
haya.
Natoa wito kwa wafanyabiashara wetu watambue
umuhimu wa kutoa risiti zilizo halali katika biashara zao na kulipa kodi kwa
mujibu wa sheria. Ni dhahiri kuwa sehemu kubwa ya mapato yetu inatokana na
kodi. Kwa hivyo, nawahimiza wafanyabiashara
wauendeleze utaratibu huo kwa imani na mapenzi kwa kutambua kuwa huo ni wajibu
wao wa kisheria, ili Serikali ipate fedha za kutolea huduma na kuiendeleza
miradi mbali mbali ya maendeleo. Serikali ni sisi wenyewe wananchi. Tunapokuwa
tayari kuichangia Serikali, huwa tunaharakisha maendeleo ya nchi yetu ambayo
yanafanywa kwa lengo la kuleta ustawi wetu kwa wananchi wote.
Ndugu
Wananchi,
Katika kusimamia utekelezaji wa kazi za
Serikali pamoja na kusimamia mapato na matumizi ya fedha za Serikali, kuanzia
tarehe 13 Mei, 2019 hadi tarehe 27 Mei, 2019, niliendelea na utaratibu wetu wa
vikao vya uwasilishaji wa utekelezaji wa Mipango Kazi kwa kila robo mwaka
(maarufu kwa jina la Bango Kitita). Wizara zote za Serikali na Taasisi zake, ziliwasilisha
kwa mujibu wa malengo na majukumu ya msingi ya kila Wizara. Vikao hivyo huwa
vinafanyika Ikulu. Kwa jumla, Wizara
zote zimeonesha ufanisi mkubwa katika kuhakikisha fedha zilizoidhinishwa kwa
matumizi ya robo tatu ya mwaka kuanzia Julai, 2018 hadi Machi, 2019 zimetumika
vyema na mafanikio makubwa ya utekelezaji wa kazi zilizopangwa yamepatikana.
Miongoni mwa mambo yaliyochangia mafanikio
yetu ni umakini tulioutumia na usimamizi madhubuti katika kudhibiti uvujaji wa mapato pamoja na matumizi ya fedha
za Serikali na wahisani wetu wa maendeleo kwa mujibu wa bajeti na mipango
tuliyojipangia kuitekeleza. Serikali
imeridhika na kiwango cha uwajibikaji kilichooneshwa na Wizara zetu zote na
Taasisi zake katika kutumia fedha zilizoidhinishwa na Baraza la Wawakilishi kwa
mujibu wa sheria na taratibu za matumizi zilizopo.
Kwa mnasaba huu, natoa pongezi kwa Mawaziri,
Manaibu Mawaziri, Watendaji na Watumishi wote wa Serikali na Taasisi zake kwa
mafanikio hayo na ufanisi tunaoendelea kuupata katika kukuza uchumi, kuimarisha
huduma za wananchi na kuwapatia huduma mbali mbali wananchi kwa ufanisi. Natoa wito kwa viongozi wote katika Wizara na
Taasisi za Serikali waendelee kusimamia vizuri utekelezaji wa shughuli zao, na
watendaji wengine waongeze bidii, ili tupate mafanikio zaidi. Ni vyema tukaiga mbinu za mwanariadha mzuri
ambaye huwa anaongeza kasi na bidii kwa kadiri anavyokaribia mfundani. Maendeleo
ya nchi hayana kikomo, kwani kadri miaka inavyoingia na kutoka huwa inakuja na
mambo na taratibu mpya, kwa sababu ulimwengu unasonga mbele. Na sisi, ili
tusiachwe nyuma inatulazimu twende na kasi ya maendeleo duniani kwa mujibu wa
uwezo tulio nao. Kwa hivyo, mfunda wetu ni ile mipango yetu tunayoipanga
kuitekeleza katika kipindi cha mwaka mmoja lazima tuitekeleze. Ni wajibu wetu
tukaze kamba, ili tuweze kufika kwa ufanisi katika mfunda huo. Nna matumaini
makubwa kuwa tunaweza kufanya vizuri zaidi iwapo kila mmoja wetu atatimiza
wajibu wake kwa uzalendo mkubwa.
Ndugu
Wananchi,
Ushirikishwaji
wa wananchi katika mipango na shughuli zao za maendeleo ni miongoni mwa nguzo
za utawala bora. Kwa kuzingatia ukweli huu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kuanzia mwezi Julai, 2017, ilianzisha rasmi mfumo wa ugatuzi, ili kushusha
madaraka kwa wananchi kutoka Serikali kuu na kuyaweka katika usimamizi wa
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Kwa hatua za awali, tumeanza na sekta tatu ambazo ni elimu ya msingi na
maandalizi, afya ya msingi na kilimo katika huduma za ugani. Mfumo huu ni mpya hapa petu, lakini ni mfumo
unaotumika katika nchi mbali mbali ambazo zimepata mafanikio makubwa.
Sote
tunafahamu kuwa “Mwanzo mgumu”. Kwa vile upya wa jambo lolote huwa na
changamoto zake, bila ya shaka na hapa petu mfumo wa ugatuzi tumebaini tayari
una changamoto kadhaa. Lakini nataka niwathibitishie wananchi kuwa tumeanza
kupata mafanikio katika kuimarisha huduma za sekta zilizogatuliwa katika
kuwatumikia wananchi.
Kwa hivyo,
changamoto zinazojitokeza katika kipindi hiki cha mpito kama vile uhaba wa baadhi ya wataalamu,
ufinyu wa nafasi za ofisi za kufanyia
kazi, nyenzo za kufanyia kazi, na kadhalika.
Changamoto hizi zisiwe sababu ya kuturudisha nyuma na kuona kwamba mfumo
wa ugatuzi haufai. Natoa wito kwa
mamlaka zinazohusika katika sekta zilizogatuliwa zikae pamoja na wazifanyie
kazi kwa haraka changamoto hizo.
Ndugu Wananchi,
Hatuna budi
tufahamu kwamba kujadili mambo yetu kwa kushauriana kwa lengo la kutatua matatizo yetu, ni jambo
tuliloagizwa katika Uislamu. Tukirejea katika Qurani Tukufu Suratul Shuuraa,
Aya 38 inatwambia:
“Na wale waliomwitikia Mola wao
(kwa kila amri Zake) na wakasimamisha sala na wanashauriana katika mambo yao..”
Kwa hivyo,
ni matumaini yangu kwamba tutaendelea kushauriana jinsi ya kutatua changamoto
hizo, ili hatimae tuone jinsi utaratibu wa ugatuzi unavyoweza kuleta mafanikio
tuliyoyatarajia kama zilivyofanikiwa nchi nyengine. Lengo letu ni lazima
tuondokane na urasimu usio wa lazima katika kuwatumikia wananchi, kwani
tunafahamu kwamba wananchi ndio waajiri wetu waliotupa dhamana ya
kuwatumikia. Tutaendelea kufanya kazi
kwa uzalendo mkubwa na tutawajibika zaidi, tukiamini kuwa maendeleo yetu tutayaleta
sisi wenyewe.
Natoa
pongezi kwa wananchi kwa kuendelelea kushirikiana na viongozi wa ngazi mbali mbali za Serikali za
mitaa katika kuyatekeleza maagizo na miongozo inayoendelea kutolewa na Serikali
Kuu, kuhusu kuyahifadhi mazingira
pamoja na utunzaji na utumiaji wa
rasilimali zisizorejesheka, hasa uchimbaji wa mchanga, mawe, kifusi na kadhalika.
Mafanikio katika masuala haya, yatategemea sana juhudi za viongozi wa Mikoa, Wilaya
na wa Serikali za Mitaa kwa kuzingatia kwamba utendaji wao unayagusa moja kwa
moja maisha ya kila siku ya wananchi. Kwa pamoja tuendelee kushirikiana katika
kuhakikisha kwamba tunakuwa na mipango madhubuti na endelevu ya kuzitunza
vizuri rasilimali zetu kwa faida yetu na kwa vizazi vijavyo. Lazima tufanye jitihada katika kuzuia
uharibifu wa mazingira kabla ya uharibifu huo haujatokea. Tukumbuke msemo maarufu usemao: “Kinga
ni bora kuliko tiba”.
Ndugu Wananchi,
Kama
tunavyoelewa kwamba mwezi Mtukufu wa Ramadhani uliingia katika msimu wa mvua za
masika ambazo kwa kiasi fulani bado zinaendelea. Tumeshuhudia mvua kubwa
zilizonyesha katika kipindi hiki cha mwezi wa Mei ambapo kituo cha Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa cha Abeid Amani Karume kimerikodi milimita 167.2 kwa muda wa
saa 24, kwa mvua iliyonyesha tarehe 5 Mei, 2019.
Kutokana na
mvua zilizonyesha katika siku chache kuanzia tarehe 5 Mei, Kamisheni ya
Kukabiliana na Maafa Zanzibar iliripoti uharibifu wa miundo mbinu ya barabara katika sehemu mbali
mbali za Unguja na Pemba, ikiwemo baadhi ya misingi inayoendelea kujengwa
kupitia Mradi wa Uendelezaji wa Huduma za Miji (ZUSP). Kadhalika, katika ripoti
hio ilielezwa kuwa nyumba zipatazo 2,120 zimeathiriwa na mvua hizo. Hata hivyo,
katika baadhi ya maeneo ya Mji wa Zanzibar katika sehemu ambazo misingi hiyo
imejengwa, imebainika kuwa hakukuwa na uharibifu na kwamba misingi hio ilileta
nafuu kubwa.
Ndugu Wananchi,
Serikali
inaendelea na jitihada zake za kuifanyia kazi changamoto inayoendelea
kutukabili ya uharibifu wa miundombinu ya barabara pamoja na madaraja katika
msimu wa mvua. tumepata matumaini makubwa kuona kwamba matengenezo yaliyofanywa
yametuwezesha kuzitumia barabara hizo, licha ya mvua kubwa zilizokuwa zikinyesha.
Bila ya shaka, ujenzi wa miundombinu ya baadhi ya barabara, madaraja na misingi
utakapokamilika rasmi matatizo yaliyokuwa yanajitokeza katika maeneo hayo
wakati wa mvua yataondoka.
Natoa
pongezi kwa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kwa kutekeleza agizo
nililowapa la kulitafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo la maji la Kibonde Mzungu
kwa kujenga daraja la kisasa. Naiagiza Wizara hio iendelee na kazi ya kuiunganisha barabara ya Fuoni kutoka kwenye kituo cha
Polisi hadi ifike Kibonde Mzungu. Vile
vile, naithamini sana kazi inayofanywa na Wizara hio kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha
kupitia Mradi wa ZUSP ya kutekeleza agizo langu la
kuinyanyua barabara katika eneo
la Bwawa la Mwanakwerekwe. Vile vile, nakupongezeni kwa kazi nzuri mlioifanya
ya ujenzi wa msingi mkubwa kwa ajili ya kuyaondoa maji yaliyokuwa yakituama
katika eneo la Kiembesamaki. Msingi huo
uliopitia Mbweni hadi pwani ya Mazizini, umelipatia ufumbuzi wa tatizo la miaka
mingi. Nakuhimizeni muharakishe mipango mliyonayo ya kuzifanyia matengenezo
barabara zetu zilizoharibika kwa mvua mara baada ya mvua hizi zitakaposita
kunyesha.
Natoa pole
sana kwa wananchi wote waliopata athari kutokana na mvua zinazoendelea
kunyesha. Serikali ilifanya tathmini ya
athari hizo na hatua za kuwasaidia wananchi waliofikwa na maafa hayo zimeshaanza
kuchukuliwa. Hata hivyo, kwa mara nyengine nawanasihi wananchi waache kujenga
katika maeneo ya mabondeni na katika njia za maji, ili kuepuka hasara
zinazotokana na mvua. Wakati wote
tuzingatie msemo mashuhuri usemao: “Tahadhari, kabla ya athari”.
Katika
jitihada za kuimarisha miundombinu ya barabara, Serikali imenunua mtambo wa lami wa kisasa pamoja na kuagiza zana na vifaa vya kisasa
kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara mpya pamoja na
ukarabati wa baadhi ya barabara za zamani za Unguja na Pemba. Mtambo huo wa
lami pamoja na vifaa vilivyoagizwa vimegharimu jumla ya TZS bilioni 14.8. Kazi ya ufungaji wa Mtambo wa lami inaendelea
wakati zana na vifaa tulivyoviagiza vinategemewa kuwasili nchini mwezi huu. Kuwepo kwa vifaa hivi vya kisasa, kutapunguza
utegemezi wa kampuni za kigeni katika kuendeleza na kuimarisha barabara zetu na
kutatuwezesha kutekeleza miradi mingi ya bababara kwa wakati mmoja kwa Unguja
na Pemba.
Ndugu Wananchi,
Wakati
tulipokuwa katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani, wenzetu Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi wamekuwa wakiendelea na vikao kwa ajili ya kusoma, kujadili na kupitisha bajeti za Serikali kwa mwaka wa
Fedha wa 2019/2020. Nachukua fursa hii
kumpongeza tena Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza la Wawakilishi,Naibu
Spika wa Baraza la Wawakilishi, Wenyeviti wa Baraza, Viongozi wa Kamati za
Kudumu za Baraza na Waheshimiwa Wawakilishi wote kwa kazi nzuri wanayoifanya ya
kuwawakilisha wananchi na kuisimamia Serikali.
Nimekuwa nikifuatilia mijadala ya vikao hivyo na nimeridhishwa sana na
michango ya Waheshimiwa Wajumbe ambayo inaonesha wazi kuwa ina lengo la kuendeleza
jitihada za Serikali na kuongeza kasi yetu ya maendeleo.
Natoa
shukurani kwa viongozi wa Serikali katika Baraza la Wawakilishi wakiongozwa na
Makamo wa Pili wa Rais Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, kwa namna
wanavyoiwakilisha Serikali na kujibu hoja za Waheshimiwa Wawakilishi. Nalitakia Baraza letu kila la kheri na
mafanikio katika kumalizia kazi yao hio ya kikatiba.
Ndugu Wananchi,
Ombi langu
kwenu wananchi ni kuwa muendelee kuzisikiliza na kuzifuatilia Hotuba za Bajeti
za Wizara mbali mbali za Serikali kadri zinavyoendelea kuwasilishwa katika
Baraza la Wawakilishi. Hadi hivi sasa tayari Wizara kumi na moja zimeshawasilisha
Hotuba zao za Bajeti na zimepitishwa na Baraza.
Hapana shaka wananchi mmekua mkiyafuatilia majadiliano yanayoendelea
kuhusu Bajeti za Wizara za Serikali.
Vile vile,
nataka nikukumbusheni wananchi nyote kwamba msikose kuisikiliza bajeti ya
Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020 itakayosomwa na Waziri wa Fedha na Mipango
inayotegemewa kuwasilishwa tarehe 20
Juni, 2019, ili muweze kuijua mipango ya Serikali na fedha zitakazotumika
katika kuitekeleza mipango hio kwa ajili ya maendeleo yetu.
Ndugu Wananchi,
Ni kawaida
katika Baraza hili la Idd el Fitr kuwatakia kheri na matayarisho mema Waislamu
wenzetu ambao Mwenyezi Mungu amewajaalia wasaa wa kwenda kuitekeleza ibada ya
Hija huko Saudi Arabia. Tunamuomba Mola
wetu Mtukufu awape afya njema, ili waweze kuitekeleza vyema ibada hio.
Tunawaombea safari yao ya kwenda na kurudi iwe ya salama na utulivu. Tunamuomba
Mwenyezi Mungu azikubali ibada zao zote. Mwenyezi Mungu awape uwezo, nguvu na hamu ya
kuitekeleza ibada ya Hija Waislamu wenzetu ambao bado hawajajaaliwa kwenda kuitekeleza
ibada hio.
Kadhalika,
natoa shukurani kwa wafanyabiashara wote ambao waliitikia wito nilioutoa katika
nasaha zangu za kuukaribisha mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kuwapunguzia wananchi
bei za bidhaa mbali mbali. Ndugu zetu wafanyabiashara wanapaswa wajue kuwa
hawakupoteza kitu, ila wametoa sadaka na kufanya uadilifu, mambo ambayo yana
malipo makubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Katika
kuwafikiria na kuwapa msaada watu wenye mahitaji, kuna hadithi ya Mtume
Muhammad (S.A.W) iliyopokelewa na Imam Muslim inayosema:
“Mtu mwenye kujali haja za ndugu zake, basi
Mwenyezi Mungu huzijali haja zake”.
Kwa hakika, wenzetu wafanyabiashara wana haja
nyingi zenye mnasaba na mafanikio ya shughuli zao. Kwa hivyo, kutokana na hadithi
hii bila ya shaka, Mwenyezi Mungu atawaongezea baraka na ufanisi katika biashara
zao.
Ndugu Wananchi,
Natoa
shukurani kwa uongozi na wafanyakazi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na
Nishati na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kwa kuwapatia huduma ya maji
wananchi wenzetu ambao huduma za maji hazipatikani vyema katika maeneo yao. Nnazo
taarifa kwamba katika kipindi cha mwezi wa Ramadhani, huduma za maji safi na
salama ziliimarika katika maeneo mengi ya Mkoa wa Mjini Magharibi. Mafanikio
haya, yanatihibisha kwamba ZAWA wana uwezo mkubwa wa kuimarisha utoaji wa
huduma za maji safi na salama. Juhudi hizi lazima ziendelezwe katika kipindi
chote.
Natoa
shukurani kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa ajili ya kusimamia ulinzi wa
nchi yetu katika maeneo yote, kusimamia hali ya usalama wa wananchi na
kukabiliana na madereva wanaovunja sheria za usalama barabarani. Hata hivyo, polisi wa usalama barabarani
waendeleze jitihada za kufanya wajibu wao, hasa katika kipindi hiki cha sikukuu
ambapo wananchi wengi hutumia barabara zetu.
Vile vile, wazazi na sisi walezi tuendelee kusimamia malezi na usalama
wa watoto wetu, ili tuwalinde na mambo ambayo yanaweza kuwadhuru na yanayoweza kutuondeshea
furaha ya sikukuu.
Namalizia
hotuba yangu kwa kukutakieni nyote sikukuu njema yenye furaha na amani. Tumuombe Mola wetu Mtukufu atuzidishie amani,
umoja na mshikamano. Aizidishie neema
nchi yetu na atupe uwezo mzuri wa kupanga na kuitekeleza mipango yetu ya
maendeleo kwa ufanisi zaidi. Mwenyezi
Mungu atupe neema ya mvua yenye kheri na baraka ya mazao na atuondoshee
mitihani na khofu, kwani Yeye peke yake ndiye tunaemtegemea. Namuomba Mwenyezi Mungu aturudishe sote
nyumbani kwa salama na amani.
IDD
MUBARAK
WAKULU
AAM WAANTUM BIKHEIR
Ahsanteni
kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment