Habari za Punde

Mlemavu na mgonjwa wa akili ajifungua mtoto wa kiume Hospitali ya Micheweni

Na Masanja Mabula –Pemba 
MKAAZI wa shehia ya Maziwang’ombe wilaya ya Micheweni Pemba, ambaye ni mlemavu na mgonjwa wa akili, amewashangaza wazazi wake baada ya kulea mimba kwa miezi tisa  bila ya wazazi kumfahamu ambapo imebainika wakati wa kujifungua.
Mwanamke huyo ambaye anaulemavu wa akili, bubu  na anaugonjwa wa kifafa , amejifungua mtoto wa kiume katika hospitali ya Micheweni.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mama mzazi wa mlemavu huyo, Bikaije Kombo Khatib amesema hakuwa anafahamu kwamba mtoto wake huyo alikuwa mjamzito.
‘’Nijitahidi kumlinda mwanangu huyo, na hata kama nilipokwnda shamba nilimfungia mlango na baadhi ya wakati nilikuwa nateembelea naye, hili la kuwa mjamzito limenishangaza kwa kweli’’alifahamisha.
Aidha aliongeza kwamba’’Siku ya tatu kabla hajajifungua nilimuona kaanza kuvimba tumbo na miguu , nikafikiri maradhi mengine yamemuingia, nilimuita Mkunga na aliniambia kwamba ni mjamzito’’alieleza.
Dada wa mlemavu huyo amesema  kitendo cha mdogo wake huyo kuwa mjamzito  kimemshangaza kwani hakukuwa na dalili yoyote  ya kuonyesha ishara ya mimba.
‘’Hakukuwa na dalili yoyote ya ujauzito kwa mdogo wangu, kwani hata hata kwenye siku zake alikuwa anaingia kama kawaida’’alifahamisha.
Mmoja wa wananchi Mkasha Sharif akizungumza  amewataka wananchi kuwalinda watu wenye ulemavu dhidi ya matendo ya udhalilishaji.
Amesema ni vyema jamii kushirikiana pamoja katika serikali kuhakikisha haki za  wenye ulemavu zinalindwa.
‘’Niiombe jamii tushirikiane pamoja katika kulinda haki  za wenye ulemavu, na kitendo hichi kwa kweli kinatakiwa kulaaniwa na kila mmoja’’alisema.
Sheha wa shehia hiyo Faki Hamad Juma naye akatoa wito kwa mwananchi mwenye taarifa juu ya aliyehusika na kitendo hicho.
Amesema kuwa suala la upelelezi dhidi ya aliyehusika na kitendo tunatakiwa kufanya kwa ushirikiano  wa jamii yote kutokana na aliyefanyiwa kutokuwa na uwezo  wa kuongea.
Mwakilishi wa Jimbo la Michweni Shamata Shaame Khamis ameelezea kutoridhishwa na tukio hilo na kuomba aliyehusika na ujauzito huo ajitokeze kutoa huduma kwa mtoto aliyezaliwa.
Aidha amewashauri wananchi walio na taarifa za awali juu ya aliyehusika na kitendo hicho kuwasilisha ushahidi wake kwenye vyombo vya sheria ili hatua zinazofaa ziweze kuchukuliwa.
‘’Taarifa hizi nimezipokea kwa masikitiko na mshangao mkubwa , kwani ukiachilia ulemavu alionao pia ni mtoto yatima , hivyo niwaomb wanajamii watakao guswa na tukio hili wajitokeze kumusaidia’’alisisitiza.
Mama mzazi wa mlemavu huo amebebeshwa mzigo wa pili , jambo ambalo  linaweza kudumaza shughuli zake kiuchumi, kwani hatakuwa na muda wa kujishughulisha baada ya kuongezea ulezi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.