Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, Awaapisha Viongozi Aliowateuwa Hivi Karibu.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akimuapisha Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar Ndg. Juma Hssan Juma Reli, hafla hiyo imefanyika leo katika Ukumbi wa Ikulu Zanzibar.  

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amewaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni kushika nyadhifa mbali mbali katika Taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Viongozi walioapishwa na Rais Dk. Shein katika hafla iliyofanyika Ikulu Mjini Zanzibar ni Abeid Juma Ali anaekuwa Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘’A’’ Unguja. Kapteni Khatib Khamis Mwadini anaekuwa Mkuu wa Wilaya ya Wete Pemba,

Wengine ni Juma Hassan Reli anaekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Viwanda na Mwita Mgeni Mwita anaekuwa Katibu Mtendaji Tume ya Mipango.

Hafla hiyo, ilihudhuriwa na viongozi kadhaa akiwemo Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar  Omar Othman Makungu ,Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan Said, Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan Juma pamoja na Makatibu Wakuu.

Wengine ni Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih, Sheikh Hassan Othman Ngwali Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Mahmoud Mussa Wadi Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar, Mkuu wa  Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud, Meya wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar Khatib Abrahman Khatib, Washauri wa Rais wa Zanzibar, na viongozi wengine wa Serikali pamoja na wanafamilia.
Nao viongozi walioapishwa hivi leo walieleza kuwa uteuzi huo unaashiria kuwa ni uthibitisho unaoonesha kwamba bado Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein anawaamini katika utekelezaji wa majukumu yao.

Aidha,viongozi hao waliomba ushirikiano katika taasisi wanazokwenda kuzifanyia kazi ili kufanikisha malengo yaliokusudiwa katika kuiletea Zanzibar maendeleo pamoja na wananchi wake.

Sambamba na hayo, viongozi hao waliahidi kusimamia na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 ikiwa ni Dira katika kutekeleza  na kusimamia maendeleo katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar , Kutekeleza Mipango Mikuu ya Maendeleo ambayo ni MKUZA III, Dira ya Maenedeleo ya 2020 pamoja na Mpango wa Dunia wa Maendeleo Endelevu.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.