Habari za Punde

Shadya akemea ukatili dhidi ya wazee

Baadhi ya wazee wakiwa wameshikilia bango lenye ujumbe Zuia unyanyasaji dhidi ya wazee kwenye maandamano ya siku ya kujenga uelewa wa uwepo wa udhalilishwaji wa wazee Duniani Juni 15 iliyofanyika ukumbi wa ZSSF Kariakoo Mjini Zanzibar.
Naibu Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Shadya Mohammed Suleiman akiwahutubia wazee katika siku ya kujenga uelewa wa uwepo wa udhalilishwaji wa wazee Duniani iliyoadhimishwa Juni 15 katika ukumbi wa ZSSF Kariakoo Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi, Kituo cha Msaada wa Kisheria na Kijamii kwa Wazee Zanzibar Maria Obel Malila akiwasilisha mada ya Udhalilishaji wa Wazee katika Sherehe ya Siku ya kujenga uwelewa wa uwepo wa udhalilishwaji wa wazee iliyoadhimishwa Juni 15 ukumbi wa ZSSF Kariakoo.
Bi. Tatu Lisweko Mlekwa wa kijiji cha Bumbwisudi popo akitoa ushuhuda wa namna walivyowahi kukumbwa na mambo ya unyanyasaji kabla ya kusaidiwa na Jumuiya ya Wastaafu na Wazee Zanzibar (JUWAZA).
Mzee Nassor Salum Hamad wa Dunga kiembeni akitoa ushuhuda wa namna walivyowahi kukumbwa na mambo ya unyanyasaji kabla ya kusaidiwa na Jumuiya ya Wastaafu na Wazee Zanzibar (JUWAZA).
Baadhi ya wazee wakifuatialia hutuba ya Naibu Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Shadya Mohammed (hayupo pichani) katika madhimisho ya siku ya kujenga uelewa wa uwepo wa udhalilishwaji wa wazee Duniani.
Picha na Makame Mshenga.
Na. Salum Vuai.
JAMII nchini imetakiwa kuacha tabia ya kuwanyanyapaa wazee kwa kutumia upungufu wao wa nguvu kuwatendea vitendo visivyokuwa vya kiungwana ikiwemo kuwasingizia uchawi.
Akizungumza katika kongamano la kupinga unyanyasaji dhidi ya wazee lililofanyika jana kwenye ukumbi wa ZSSF Kariakoo mjini Zanzibar, Naibu Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Shadya Mohammed Suleiman, amesema wazee wanastahili matunzo na heshima na sio kudharauliwa.
Kongamano hilo lililokuwa sehemu ya maadhimisho ya siku ya kujenga uelewa na kupinga ukatili na unyanyasaji dhidi ya wazee duniani, lilihudhuriwa na wanachama kutoka jumuiya ya wazee pamoja na taasisi nyengine zinafanya kazi ya kulitetea kundi hilo muhimu kwa ustawi wa taifa.
Shadya alisema si jambo jemba kwa vijana kuwatenga wazee na kukataa kuwapa msaada wanaouhitaji, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanakuwa na afya nzuri na kuishi kwa faraja baada ya kutumia nguvu zao kuwalea vijana hao na kujenga taifa kwa jumla.
“Suala la kuwatunza wazee halina mbadala kwetu, kwani hata viongozi waasisi wa taifa letu marehemu mzee Abeid Karume na hayati Mwalimu Julius Nyerere, waliuona umuhimu wa wazee na kuwajengea mazingira mazuri ya kuishi  wanapofikia umri mkubwa na kupungua nguvu za mwili,” alisema.
Kwa hivyo alisema, wakati serikali zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi Zanzibar zinafanya jitihada ya kuwaenzi wazee, sio vizuri baadhi ya watu wawanyanyase na kuwatendea vitendo visivyostahili.
Alieleza kuwa, miongoni mwa mambo yanayofanywa na  serikali ni kuunda na kuyaimarisha mabaraza ya wazee ili kuwawezesha kupata haki zao za msingi ikiwemo matibabu, usafiri, na mafao ya uzeeni kwa wakati.
Alisema hakuna hata nchi moja duniani iliyopata maendeleo bila mchango wa wazee, na kuongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inafanya kila jitihada kuhakikisha wazee 53,311 wenye umri kuanzia miaka 60 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, wanaishi kwa furaha katika uzee wao.
Alisema hatua ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kuwapatia wazee wenye umri wa miaka 70 na kuendelea pensheni ya shilingi 70,000 ni kielelezo kwamba serikali inajali na kuthamini mchango wa wazee.
Hata hivyo, kwa upande mwengine, Naibu Waziri huyo aliwataka wazee kutokuona muhali pale wanapofanyiwa vitendo vibaya na watu wa  familia zao, majirani na wengine, akisema muhali umechangia kurejesha nyuma maendeleo  na kuiweka Zanzibar katika hali ngumu ya kupungua kwa ustawi.
Alihitimisha kwa kusema, ni matumaini yake kuwa serikali, taasisi na wadau mbalimbali wa  maendeleo, wataongeza ushirikiano ili kuhakikisha kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu isemayo; “Tuungane pamoja kwa kupaza sauti za wazee”, inasaidia kumaliza ukatili dhidi ya wazee na kulifanya jambo hilo kuwa historia.
Mapema, katika risala iliyosomwa na mjumbe wa kamati tendaji ya Jumuiya ya Wastaafu na Wazee Zanzibar (JUWAZA) Amour Haji Nassor, ilielezwa kuwa, kuna matukio mengi yanayotokea ambayo yanaonesha kuwa wazee katika sehemu mbalimbali nchini hawako salama.
Alisema wazee wa Zanzibar wanakabiliwa na changamoto nyingi kama vile lishe duni, huduma za matibabu zisizoridhisha, usafiri, makaazi, kupungukiwa na fedha na misaada ya hali na mali kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki wa karibu.
Aliiomba serikali kuongeza jitihada katika kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo, akiitaka wizara iwawekee wazee vituo maalumu vya huduma za afya, kuwezesha uundwaji na uimarishwaji wa mabaraza ya wazee nchini na kujenga mtandao wa kuyaunganisha kupitia ngazi ya shehia.
Aisga aliwataka vijana wa sasa na watoto kutambua kwamba nao wanaelekea huko, kwani uzee na ‘kuzeeka haukwepeki’.
Katibu wa JUWAZA Dk. Yussuf Nuhu Pandu, kwa niaba ya Mweyekiti alitumia fursa hiyo kuwashajiisha wazee wasione vibaya kupaza sauti zao pale wanapotendewa vitendo vilivyo kinyume na ubinadamu.
“Unapojiona umesimama katika daladala usione shida kumuinua mtu hata kwa kumkemea, au pale unaporushiwa maneno ya ufedhuli na kijana, tumia nguvu zako zilizobaki kushika bakora umtandike ndipo atakapokuwekea heshima,“ alisema Dk. Nuhu.
Siku hiyo ilizinduliwa mwaka 2006 na Mtandao wa Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee Duniani kwa kushirikiana na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO), ikilenga kuwajengea mazingira salama wazee ili waishi bila ya vitisho, ukatili, unyanyapaa, ubakaji na kukosa misaada kutoka kwa marafiki wa karibu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.