Habari za Punde

Wajasiriamali Kujengewa Masoko ya Wazi.Kuuza Bidhaa Zao.

Waziri wa Biashara na Viwanda Zanzibar Mhe.Balozi Amina Salum Ali akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya (MKURABITA) waliofika ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar kumuelezea changamoto walizozigundua zinazowakabili Wajasiriamali wa Zanzibar.

Na Faki Mjaka –Maelezo Zanzibar .28.06.2019
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepanga kuanzisha Masoko ya Wazi kwa kila Wilaya ili yatumike kwa ajili ya kuuzia Bidhaa za Wajasiriamali Unguja na Pemba.
Masoko hayo yatawasaidia Wajasiriamali kupata maeneo maalum ya kuonesha bidhaa zao kwa Wateja na kuondokana na mazoea ya kuzitumia nyumba zao kama sehemu ya Soko la bidhaa wanazozizalisha.
Waziri wa Biashara na Viwanda Zanzibar Balozi Amina Salum Ali ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya Ofisi ya Mpango wa kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) waliofika ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar.
Amesema Serikali muda wote imekuwa ikifikiria namna ya kuwasaidia Wajasiriamali wa Zanzibar kwa kufahamu kwamba mazingira mazuri ya kazi zao huchochea ukuwaji wa biashara zao na kulipa Kodi serikalini kwa urahisi.
Balozi Amina ameongeza kuwa utaratibu mbaya unaotumiwa na Wajasiriamali wengi wa Zanzibar kuzifanya Nyumba zao za makaazi kuwa Soko la bidhaa hupunguza Wateja wengi kwa kushindwa kuziona bidhaa zao.
Hivyo amesema kuwa kuwepo kwa Maeneo tengefu ya Masoko ya wazi katika kila Wilaya kutawahakikishia Wajasiriamali idadi kubwa ya wateja watakaoenda kununua bidhaa zao.
“Tayari tumeshaandaa maeneo tofauti kama vile Nungwi, Dunga na Pemba ili Wajasiriamali waweze kuuza bidhaa zao katika maeneo hayo na sio majumbani mwao” Alisema Waziri Amina.
Hata hivyo Waziri Amina ameelezea kusikitishwa kwake na baadhi ya Wajasiriamali waotengeneza bidhaa zao bila kuangalia mahitaji ya soko.
Amesema tabia hiyo huwapelekea kukosa wateja na kupata hasara ya mitaji yao na gharama wanazotumia katika kuandaa bidhaa hizo.
“Utakuta mtu anatengeneza bidhaa za Unga wa Muhogo lakini bila hata kujua nani atamuuzia bidhaa hizo..mwishowe wanalalamika kuwa hawapati Soko, kumbe walipaswa kwanza wafanye uchunguzi wa mahitaji ya soko kwanza”  Alisema Balozi Amina.
Kutokana na hali hiyo Balozi Amina amesema Serikali itaendelea kuchukua jukumu la kuwalewesha Wananchi hao ili kuondokana na tabia ya kutengeneza bidhaa bila kujua mahitaji ya Soko.
Awali Mwenyekiti wa kamati ya Uongozi ya MKURABITA Balozi mstaafu Daniel Ole Njolay wakati akisoma Taarifa ya ziara yao ya siku tano Kisiwani Unguja alimueleza Waziri wa Biashara kuwa Wajasiriamali wengi wa Zanzibar walilalamika kuhusu Soko la bidhaa zao.
Aidha Balozi Njolay ameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendelea kutoa elimu kwa Wajasiriamali na kurasimisha biashara zao ili ziweze kutambuliwa kisheria.
Kamati hiyo ya MKURABITA pia ilipata nafasi ya kufanya utalii wa ndani katika maeneo ya kihistoria ya Zanzibar kama vile Mnara wa Kumbukumbu ya Mapinduzi Kisonge, Kasri ya Mfalme  Forodhani na Ngome. Picha na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.