Habari za Punde

Mafunzo kwa kamati za Kitaalamu za Taasisi ya Viwango Zanzibar ZBS

 Afisa Viwango kutoka Taasisi ya Viwango Zanzibar ZBS Hafsa Ali Slim akiwasilisha Mada ya utangulizi wa Viwango katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakil Kikwajuni mjini Unguja
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Taasisi ya Viwango Zanzibar ZBS, Professa Ali Seif Mshimba katikati akifunguwa Mkutano wa siku moja wa mafunzo kwa kamati za Kitaalamu za ZBS
 Wajumbe wa Kamati za Kitaalamu wakisikiliza Mada zilizokuwa zikiwasilishwa katika mafunzo ya kuzijengea uwezo Kamati za Kitaalam za ZBS
Wajumbe wa Kamati za Kitaalamu wakisikiliza Mada zilizokuwa zikiwasilishwa katika mafunzo ya kuzijengea uwezo Kamati za Kitaalam za ZBS 

Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar  
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) Prof. Ali Seif Mshimba amewataka Wajumbe wa Kamati za wataalamu za uandaaji wa viwango kuzingatia mafunzo wanayopatiwa ili yasaidie kuandaa viwango vya ubora wa bidhaa vinavyokubalika na kutumika kimataifa.
Prof. Mshimba ametoa wito huo wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa wajumbe wa kamati hizo yaliyofanyika katika ukumbi wa sheikh Idiss Abdul Wakili, Kikwajuni mjini Unguja.
Amefahamisha kuwa lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati hizo ili wafanye kazi zao kwa ufanisi na kuhakikisha Zanzibar inakuwa salama dhidi ya matumizi ya bidhaa zisizo na ubora.
Alisema taasisi hiyo ina jukumu kubwa la kuhakikisha watumiaji wa bidhaa na huduma nchini wanakuwa salama kutokana na kutumia bidhaa na huduma bora kwa lengo la kulinda afya za watumiaji na mazingira.
Prof. Mshimba amewataka Wajumbe wa kamati hizo kuwa wafufatiliaji wa mambo na kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia ili kusudi bidhaa wanazozipitisha ziendane na mahitaji ya sasa.
“Kwa vile dunia inaenda kasi sana na teknolojia inakuwa siku hadi siku Wajumbe inakulazimuni pia kufuatilia mambo kwa ukaribu ili ikusaidieni katika kutekeleza vyema majukumu yenu”
Akitoa maelezo ya utangulizi katika mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa taasisi hiyo Haji Abdulhamid alizitaka Kamati hizo kuangalia uwezekano wa kuandaa viwango vya bidhaa ndogo ndogo za viungo ili kusaidia kukuza miradi ya wajasiriamali wadogo na wa kati.
Ameeleza kuwa kupatikana kwa Alama ya ubora kwa bidhaa hizo kutatanua wigo wa soko na kuaminika miongoni mwa watumiaji.
Hivyo amewataka Wajumbe wa Kamati hizo kurahisisha upatikanaji wa haraka wa Alama za Ubora wa bidhaa za Wajasiriamali wa Zanzibar ikiwemo Achari na Viungo.
“Wito wangu tuwasidie Wajasiriamali wetu wadogo wadogo ambao wanalitegemea soko la utalii kwa bidhaa zao, hivyo wanahitaji kupatiwa kwa haraka ithibati ya ZBS kwa bidhaa zao ili zipate soko na kuaminiwa na wageni” alinasihi Kaimu Mkurugenzi.
Wakiwasilisha mada katika mafunzo hayo Mafisa viwango wa ZBS Hafsa Ali Slim, kidawa Hassan hakim na Afisa mwandamizi wa Shirika la viwango Tanzania TBS Rosemary Ndesamburo waliwataka Wajumbe wa Kamati hizo kuwa makini na kujiamini wanapokuwa katika kazi ya uandaaji wa viwango.
Wawasiliaji hao pia waliwashauri wajumbe hao kila mmoja kuzingatia na kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia maslahi ya taifa na kuinua uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.
Walisema iwapo wajumbe hao watasimamia kikamilifu wajibu na majukumu yao watasaidia kujenga afya, uchumi na ustawi wa jamii hivyo ushiriki wao ni jambo la msingi.
Nao washiriki wa mafunzo hayo wameiomba taasisi ya viwango Zanzibar kuhakikisha viwango vinavyoandaliwa na taasisi hiyo vinasimamiwa na kutekelezwa ipasavyo ili kuyafikia malengo ya kuanzishwa kwa viwango hivyo.
Walisema ili kuongeza ufanisi wa viwango vinavyoandaliwa na taasisi hiyo kuna haja ya kutangazwa kwa umma ili viweze kujulikana na kujenga uelewa wa jamii.
Mafunzo hayo ya siku moja yaliandaliwa na ZBS ambapo mada tatu ziliwasilishwa na kujadiliwa kwa lengo la kujenga uelewa wa wajumbe wa kamati za kitaalamu ili ziweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.