Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Azungumza na Viongozi wa Timu ya Yanga

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi kulia akimkabidhi Mwenyekiti wa Klabu ya Dar es salaam Young African Dr. Mshindo Msolla mchango wake wa Shilingi Milioni 2,000,000/- kwa Klabu hiyo kukamilisha ahadi aliyotoa kwa uongozi huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumzana Uongozi wa Dar es salaam Young African Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumzana Uongozi wa Dar es salaam Young African Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Mwenyekiti wa Klabu ya Dar es salaam Young African Dr. Mshindo Msolla akimueleza Balozi Seif  Malengo ya Uongozi Mpya wa Klabu hiyo kongwe Tanzania.
Baadhi ya Viongozi wa Dar es salaam Young African wakifuatilia mazungumzo yao na Makamu waPili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif hayupo pichani.

Na.OthmanKhamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameunga mkono mfumo wa Klabu Maarufu ya Mchezo wa soka ya Dar es salaam Young African wa kuanzisha Miradi ya kujitegemea katika azma ya kuiondoshea na utegemezi Klabu hiyo.
Alisema tabia ya kutembeza kutegemea Mtu binafsi au wakati mwengine kutembeza Bakuli mara zote huleta migogoro baina ya Wanachama na Viongozi na hatimae uwajibikaji au malengo ya Klabu hukosekana na kubakisha huzuni kwa Wanachana pamoja na Wapenzi wa Klabu.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati akizungumza na Uongozi wa Klabu ya Dar es salaam Young African ambao ulikuwepo Zanzibar kushiriki uzinduzi wa Shughuli ya Wiki ya Mwananchi ya kuchangia Yanga.
Alisema Taasisi, Jumuiya na hata vikundi vya Jamii vinapofikia hatua ya kuanzisha Miradi ya Kiuchumi hupelekea kujitegemea, kujiamini na hata kuwa na maamuzi yanayopelekea ufanisi wa yale wanayokusudia kuyatekeleza kwa faida ya Taasisi au jumuiya hizo.
Balozi Seif alisema kwa kuwa Klabu hiyo ina dhamira sahihi ya kuendeleza Wachezaji wake katika azma njema ya kuimarisha ustawi wao yeye binafsi pamoja na Serikali iko tayari kusaidia nguvu zake ili kuona malengo iliyojipangia yanafanikiwa vizuri.
Aliusisitiza Uongozi wa Klabu hiyo Kongwe Nchini Tanzania kuzingatia umuhimu wa kusimamia vyema makusanyo katika vianzio vyake ili mapato yatakayopatikana yaendeshe Klabu bila ya vikwazo vyovyote.
Alisema Klabu za soka na hata Taasisi nyingi hukumbwa na mogogoro mara pale mhasibu au mshika fedha muhusika anapotakiwa kutoa maelezo ya makusanyo au fedha zilizopo katika mfuko wa Klabu.
Akizungumzia uimarishaji wa Wachezaji Vijana kwenye Klabu hiyo Kongwe Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliukumbusha Uongozi huo wa Klabu ya Dar es salaam Young African kuzingatia suala hilo ambalo ni muhimu kwa Taasisi yoyote ya Michezo.
Alisema Tanzania bado ina upungufu mkubwa wa vyuo maalum vinavypaswa kuwaendeleza Wanamichezo wachanga hasa wale wenye vipaji Maalum ambao huwa tegemeo la Taifa hapo baadae katika Nyanja za Kimataifa.
Alieleza kwamba Vijana wengi waliopo hivi sasa ndani ya Dimba la Michezo ni wale wenye mapenzi na mchezo wa soka ambapo muda mwingi wanapokuwa mazoezini hukosa mbinu na maarifa ya kufanya vyema katika mfumo wa Kitaalamu zaidi.
Mapema Mwenyekiti wa Klabu ya Dar es salaam Young African Dr. Mshindo Msolla alimueleza Balozi Seif  kwamba Uongzi Mpya wa Klabu hiyo umelenga kuyasimamia mambo matano makubwa yatakayosaidia kuipeleka Klabu hiyo katika mafanikio makubwa.
Dr. Msolla aliyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kuleta Umoja katika kuipeleka Timu kwa Wanachama, kuimarisha Miradi iliyopo Klabuni na kubuni mengine mipya, uwajibikaji na Utawala Bora pamoja na kuiendeleza miradi iliyopo Visiwani Zanzibar.
Alisema katika mfumo huo Mpya utakaoanzishwa, Wanachama watakuwa na uwezo wa kujua mapato na matumizi ya Klabu kupitia Mtandao wa Kisasa wa Habari na Mawasiliano utakaokwenda sambamba na kuongeza Wanachama kutoka 17,000 hadi kufikia Milioni 1,000,000.
Mwenyekiti huyo wa Klabu ya Dar es salaam Young African alisisitiza kwamba mpango maalum utaandaliwa katika matumizi sahihi ya Nembo ya Klabu ambapo itatolewa tenda na Kampuni itakayoshindaitakuwa na haki ya kuuza Jazi zenye Rangi ya Klabu na kila Jezi moja kutakuwa na asilimia ya Klabu.
Alisema kutokana na Historia kubwa ya uwepo wa wanachama wengi, Klabu hiyo lazima irejee katika Heshima yake ya kuwa chanzo cha kutoa Wachezaji bora watakaotegemewa katika kikosi cha Timu ya Taifa.
Uzinduzi wa shughuli ya Wiki ya Mwananchi ya kuchangia Yanga uliofanyika Zanzibar kutokana na Historia ya Klabu hiyo pamoja na mambo mengine ulihusisha pia shughuli za Kijamii Mitaani ikiwemo usafi wa Mazingira pamoja na Mikutano ya Wanachama.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.