Naibu
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza akiwa kwenye
picha ya pamoja na sehemu ya washiriki wa mafunzo yakuwajemgea uwezo waandishi
wa habari hapa nchini ili waweze kuripoti habari zinazohusu Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC),
Hayo yemejiri leo Julai 8,2019 mjini Morogoro wakati wa ufunguzi wa awamu ya kwanza ya mafunzo hayo yanayofanyika
mjini Morogoro kwa siku tatu.
Na Frank Mvungi- MAELEZO, Morogoro
Waandishi wa Habari nchini wameaswa
kuzingatia uzalendo na weledi katika
utekelezaji wa majukumu yao wakati wote
wa kuripoti habari zinazohusu fursa zilizopo katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika (SADC) pamoja na mkutano wa
wakuu wa nchi wanachama utakaofanyika Jijini Dar es Salaam Agosti 17 na 18,
2019.
Akizungumza leo mjini Morogoro wakati
akifungua awamu ya kwanza ya mafunzo yakuwajengea uwezo waandishi wa habari ili waweze kuandika na
kuripoti habari za Jumiya hiyo, Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na
Michezo Mhe. Juliana Shonza amesema kuwa
mkutano wa Wakuu wa nchi wanachama unakuja na fursa nyingi zitakazowanufaisha
wananchi wote.
“Tunawaomba Waandishi wa Habari kutekeleza jukumu la kutangaza habari
zinazohusu SADC kwa uzalendo, weledi na kwa ufanisi ili watanzania waweze
kushiriki kikamilifu kutokana na umuhimu wa Jumuiya hii na kutumia fursa za
kiuchumi na biashara zinazopatikana kupitia wananchi takribani milioni 450 wa
nchi zote za SADC”Alisisitiza Mhe Shonza
Akifafanua Mhe Shonza amesema
kuwa kila mwandishi wa habari analo
jukumu la kuhakikisha kuwa kila mwananchi anafahamu fursa zilizopo katika Jumuiya
hiyo na mamna zinavyoweza kuwanufaisha wananchi wote katika nyanja za kiuchumi
na kijamii.
Aliongeza kuwa waandishi wa habari wa Tanzania kuna umuhimu
mkubwa wa kuwa na uelewa wa pamoja wakati wa mkutano huo kwa kutambua kuwa wao ni daraja kati ya wananchi
na Serikali pamoja na Jumuiya zote ambazo Tanzania ni mwanachama ikiwemo SADC.
“Ni matumanini yangu kuwa baada ya
mafunzo haya mtawaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa SADC kwa maendeleo ya
kiuchumi ya nchi wanachama, fursa za kiuchumi, Namna nchi yetu inavyotekeleza
mikakati mbalimbali ya SADC, Fursa za masoko ndani ya SADC kutokana na bidhaa
na mazao ya kilimo yanayozalishwa katika nchi wanachama” Alisisitiza Mhe Shonza
Katika kusisistiza umuhimu wa amani
na utulivu Mhe. Shonza aliwaasa wanahabari kuwaelimisha wananchi umuhimu wa
amani kipindi choche cha mkutano huo wa wakuu wa nchi wanachama na hata
baada ili kuendelea kujenga taswira
nzuri ya Tanzania.
Baadhi ya fursa zinazotokana na
mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo utakaofanyika mwezi
ujao hapa nchini ni pamoja na usafiri na usafirishaji, malazi na utalii kwa
wageni hao zaidi ya 1000 wanaotarajiwa kuja hapa nchini kutokana na mkutano
huo.
Aidha, Mheshimiwa Shonza aliwataka
waandishi wote wa habari hapa nchini kutumia nafasi zao kuwaelimisha wananchi
kuhusu umuhimu wa amani iliyopo hapa nchini ambayo ni moja ya kivutio kikubwa
kwa wageni kutoka mataifa mbalimbali kuja na kuwekeza hapa nchini.
“Sitarajii mwandishi wa habari wa
Tanzania kutumia kalamu yake kuchafua taswira ya nchi yetu katika kipindi hiki
cha mkutano huu mkubwa na hata baada ya
mkutano, matarajio ya Serikali ni kuendelea kuona mnatangaza mafanikio
ya Jumuiya na fursa zilizopo ili ziweze kuwanufaisha wananchi” Alisisitiza Mhe.
Shonza
Katika kutekeleza jukumu hilo
amewaasa waandishi hao kuzingatia kuwa jukumu la kutangaza fursa zilizopo
katika Jumuiya hiyo ni la kila mwanahabari
ili kuwajengea uelewa wananchi
juu ya namna watakavyoweza kunufaika na idadi kubwa ya wananchi waliopo katika
jumiya hiyo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika
la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) linalodhamini mafunzo hayo kwa kushirikiana na
Sekretarieti ya SADC, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bw. Dagmore Tawonezvi amesema kuwa mafunzo hayo yanatokana na maombi ya Serikali
ya Tanzania na yatasaidia kujenga uelewa kuhusu fursa zilizopo na namna ya kuzitumia
ili kuchochea maendeleo hapa nchini na katika nchi wanachama wa SADC.
Aliongeza kuwa Shirika hilo
litaendelea kushirikiana na nchi wanachama kujenga uwezo kwa waandishi wa
habari ili waweze kutangaza na kuwaelimisha wananchi kuhusu jumuiya hiyo na
manufaa yake katika kukuza uchumi.
Kwa upande wake Kaimu mkurugenzi,
Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki Bi Agnes Kayola amesema kuwa mafunzo hayo yanafanyika kwa
awamu mbili zitakazoshirikisha waandishi wa habari 30 kwa kila awamu.
Mkutano huo utatanguliwa na maonesho
ya wiki ya viwanda yatakayotumika
kutangaza bidhaa zinazozalishwa hapa nchinina nchi za SADC kwa madhumuni ya
kuhamasisha ukuaji wa viwanda katika nchi za
SADC .
Mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa
Jumuiya hiyo unafanyika Tanzania mwezi Ujao ambapo Tanzania inatarajiwa kupokea
wageni zaidi ya 1000 kutoka nchi wanachama wa SADC, katika mkutano huo Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli anatarajia kuwa mwenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa kipindi cha
mwaka mmoja kuanzia Agosti 2019 hadi Agosti 2020.
Mkutano huo wa wakuu wa nchi wanachama utakuwa na
kauli mbiu ”Mazingira wezeshi ya Kibiashara kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu
ya Viwanda” utatanguliwa na vikao vya awali vya ngazi ya Makatibu Wakuu na
Mawaziri wa SADC, Unatarajiwa kuhudhuriwa na wakuu wa nchi 16 wanachama wa SADC .
No comments:
Post a Comment