Habari za Punde

Wachezaji Watano wa Klabu ya Malindi Waacha

Na.Mwanajuma Juma.
WACHEZAJI watano  wa klabu ya Malindi wameachwa kwa kile kilichodaiwa kuwa na majeruhi ya kudumu ndani ya timu hiyo.

Wachezaji hao ambao hawakutajwa majina yao wanamajeruhi ya magoti na nyama za mapaja (Misuli), wanadaiwa kwamba  hawajaisaidia timu kwa msimu mzima wa ligi uliopita kutokana na kuwa na majeruhi.

Hayo yalithibitishwa na kocha wa timu hiyo Saleh Ahmed Machupa alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko katika uwanja wa Amaan mjini hapa.

Machupa  alisema kuwa katika msimu huu wamepanga kuwacha wachezaji saba ambapo watano ni kutokana na sababu waliyoitaja hapo juu na wengine wawili wametoka na kuhamia timu nyengine.

Timu ya Malindi ambayo inashiriki ligi kuu ya Zanzibar  imesema kuwa mbali na kuacha wachezaji hao wanampango wa kusajili wachezaji 10 ambao wataweza kujaza nafasi za wachezaji walioacha.

Alieleza kuwa kati ya wachezaji hao 10 ambao watawasajili tayari wachezaji watano wameshamalizana nao na kuendelea na mazungumzo na wachezaji waliobakia.

Alisema kuwa wachezaji hao waliomalizana nao watatu wamechukuwa kutoka Kwerekwe City, Mlandege mchezaji mmoja na mmoja kutoka Tanzania Bara.

Hata hivyo alisema kuwa nafasi ambazo wamesajili kwa wachezaji hao watano ni nafasi za washambuliaji, kiungo na mlinzi wa Kati, ambapo alisema kuwa ni matarajio yao kuwa wataisaidia timu yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.