Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Aendelea na Ziara Yake Mkoani Shinyanga.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif akisalimiana na Wananchi wa Kata ya Bibia baada ya kuwasili katika kata hiyo akiwa katika ziara yake Shinyanga Vijijini katika Jimbo la Msolwa.
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Tanzania inahitaji Viongozi waliojitolea kuwatumikia Wananchi wakati wote wakitokana na misingi ya Umoja, Mshikamano na huruma silaha ambazo ziko wazi katika utumishi mzuri uliotukuka.
Alisema Viongozi hao ambao ndio Watumishi wa Umma hupatikana kutokana na nguvu kubwa waliyonayo Wananchi katika kuwachagua wawaongoze baada ya kuwapima kwenye vigezo vinavyoashiria kuwa na sifa za kujitolea katika kuwasimiamia katika Miradi yao ya Maendeleo, Uchumi na Ustawi wa Jamii.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Kichama alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Wananchi na Wana CCM wa Majimbo ya Msolwa Shinyanga Vijijini na Jimbo la Shinyanga Mjini katika Mikutano Miwili Tofauti ya Wabunge wa Majimbo hayo kuwasilisha Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 0- 2020.
Alisema umakini wa Viongozi waliokubali kuwatumikia Kizalendo Wananchi katika maeneo yao mbali mbali Nchini hujidhihirisha kutokana na uchapa kazi wao unaowapa tiketi wa kuaminika kutoka kwa wale wanaowaongoza ikiwa ni njia sahihi ya kujipigia debe bila ya kutegemea wapambe ambao wakati mwengine ndio wanaoanzisha makundi katika Jamii na Chama kwa ujumla.
Balozi Seif  aliwaeleza Viongozi wa Majimbo ya Wilaya zilizomo ndani ya Mkoa huo wa Shinyanga kwamba wao ndio wanaobeba dhamana ya usimamizi wa Maendeleo kwa Wananchi wao kwa kushirikiana na Serikali Kuu, Uongozi  wa Wilaya pamoja na Halmashauri husika.
“ Wabunge wamebeba dhamana na kutoa ahadi ya kuwatumikia Wananchi, ahadi ambazo lazima zitekelezwe ili kutimiza ustaarabu wa Kiongozi aliyejizatiti kuwahudumia Wananchi”. Alisisitiza Balozi Seif ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi.
Mlezi huyo wa Mkoa wa Shinyanga Kichama aliendelea kuwashauri Wabunge waliochaguliwa na Wananchi Majimboni waishi kwenye Majimbo yao ili watakapohitajika isiwe usumbufu mkubwa  kuwapata.
Alisema katika kuwarahisishia utekelezaji wa majukumu yao ya kila Siku Wabunge,  Uongozi wa Ofisi ya Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania uliamua kuanzisha Ujenzi wa Ofisi za Wabunge katika Majimbo mbali mbali Tanzania Bara na Zanzibar.
Alifahamisha kwamba Uongozi wa juu wa Chama cha Mapinduzi ambao uko wazi katika utekelezaji wa majukumu yake kamwe hautakuwa tayari kumbeba Kiongozi aliyeteuliwa na Wananchi ambae amejenga tabia ya kiburi cha kutopita kwenye Jimbo lake mara baada ya kuchaguliwa.
Balozi Seif  aliwakumbusha Viongozi na Wanachama wa chama cha Mapinduzi kuendelea kuyatangaza Maendeleo makubwa yanayoendelea kufanywa na Serikali za Chama cha Mapinduzi Bara na Zanzibar.
Alisema si vyema kwa Viongozi na Wanachama hao kusubiri kazi hiyo kubwa na nzito ikafanywa na Wanachama wa Vyama vya Upinzani walioamua kurejea Chama cha Mapinduzi baada ya kuridhika na Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa mafanikio ya kupigiwa mfano.
Akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa Kipindi cha Miaka Minne Mbunge wa Jimbo la Solwa Mheshimiwa Ahmed Salum pamoja na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Aza Hilal Hamad walisema huduma za afya ni miongoni mwa Sekta zilizopewa kipaumbele zikifuatiwa na Elimu, Huduma za Maji safi na salama na Miundombinu ya Bara bara.
Walisema Vijiji vingi ndani ya Majimbo hayo tayari vimeanza kufaidika na huduma muhimu katika azma ya kustawisha Maisha yao sambamba na uwezeshwaji wa Vikundi vya ujasiri amali vitavyosaidia kupunguza utegemezi na kuendesha maisha yao kutokana na kile wanachokizalisha.
Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na msafara wake alikagua Maendeleo ya Ujenzi wa majengo ya Skuli ya Maandalizi na Msingi katika Kijiji cha Lyamidati.
Ujenzi wa Majengo hayo umefanywa kwa nguvu za Wananchi wenye baada ya usumbufu mkubwa waliokuwa wakiupata Watoto wao hasa wale wadogo wa kufuata Elimu katika masafa marefu ya zaidi ya Kilomita Tatu.
Akizungumza na Walimu, Wazazi na Wanafunzi wa Kijiji hicho Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif amewapongeza Wananchi hao wa Kijiji cha Lyamidati kwa kuanzisha Skuli baada ya kuelewa umuhimu wa Elimu kwa Kizazi chao katika maisha yao ya hapo baadae.
Balozi Seif  aliuagiza Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini kufanya juhudi zitakazosaidia kukamilisha kwa ujenzi wa Majengo hayo katika kuunga mkono nguvu za Wananchi katika Miradi yao waliyoianzisha kwenye maeneo yao.
Akiwahimiza Wanafunzi kuzingatia masomo yao Balozi Dseif aliwataka kuacha mchezo kwa vile Serikali Kuu katika miundombinu ya kuwafinyanga inawategemea kuwa Wataalamu Wazalendo  watakaobeba jukumu kubwa la kuendesha Taifa hapo baadae.
Balozi Seif aliwaasa Wazazi hasa wale wanaoishi Vijijini kuacha tabia ya kuwakatisha masomo  Watoto wao wa Kike  kwa kuwaingiza katika ndoa wakiwa na umri mdogo.
Alisema Watoto wana haki ya kupata Elimu ili ije kuwasaidia wao na familia zao katika maisha yao ya baadae hasa miaka ya sasa iliyobadilika katika mfumo wa Dunia wa Sayansi na Teknolojia.
Katika kuunga mkono jitihada za Wananchi hao wa Kijiji cha Lyamidati Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alijitolea kusaidia shilingi Milioni 1,000,000/- taslim ili kuongeza nguvu za muendelezo wa Ujenzi wa Majengo hayo ya Skuli.
Mapema Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Lyamidati Mwalimu Ali Matias Mlacha alisema Jamii ya Kijiji hicho iliamua kuanzisha Kituo cha maandalizi kwa Watoto wao mnamo Mwaka 2015  kikiwa chini ya muembe.
Kitendo hicho hakikuwapa furaha hali iliyopelekea kuanzisha Jengo la Madarasa Manne  yaliyobeba wanafunzi 41 na baadae 60 ongezeko lililoleta shauku ya kuiendeleza Skuli hiyo kwa mafunzo ya Msingi.
Mwalimu Mkuu huyo wa Skuli ya Lyamidati kwa niaba ya Walimu, Wazazi na Wanafunzi wa Kijiji hicho ameishukuru Serikali Kuu ya ushirikiano wa pamoja uliopelekea kufanikisha maendeleo ya ujenzi wa Majengo ya Skuli hiyo.
Balozi Seif alibahatika kusalimiana na Wananchi wa Kata ya Bibia baada ya msafara wake kusimama kwa muda na kuwapokea Wanachama 10 wa Chama cha Upinzani {Chadema} walioamua kurejea Chama cha Mapinduzi baada ya kuona upinzani kwa sasa umeishiwa na Agenda.
Aliwapongeza Wanachama hao kwa uamuzi wao wa kijasiri na kuwaomba wale wanaoendelea kung’ang’ani upande huo kuacha kudanganywa kwa vile yale malalamiko walikuwa wakiyadai ikiwemo mapambano dhidi ya Rushwa na ujenzi wa Tanzania Mpya hivi sasa yanatekelezwa na Chama cha Mapinduzi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akikagua Moja ya Vyumba vya Madarasa ya Skuli ya Lyamidati akielekea Shinyanga Vijijini na kuridhika na nguvu za Wananchi zilizomshawishi kusaidia Shilingi Milioni 1,000,000/- Taslim.
Balozi Seif akikagua Jengo jipya la itayokuwa skuli ya msingi ya Lyamidati ambalo linaendelea ujenzi wake aliouagiza uungwe mkono ya Hamlashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini.
Vijana wa Kikundi cha Utamaduni cha Nazeze cha Jimbo la Shinyanga Mjini kikitoa burdani ya nguvu wakati wa Mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini wa kutoa Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.
Balozi Seif Ali Iddi akiagana na Wananchi na Wana CCM wa Jimbo la Shinyanga Mjini baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Mbunge wa Jimbo hilo kutoa Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.

Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.