Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed kati kati akizungumza na Masheha hawapo pichani waliomo ndani ya Wilaya ya Magharibi “A” Kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Wilaya iliyopo Mwera.
Na.Kassim Abdi/Maryam Yunus.OMPR.
Viongozi wa Shehia pamoja na watendaji wao wametakiwa kuyatambua na kuyaripoti maeneo yanayotumiwa kufanywa vitendo vya uhalifu ikiwemo dawa za kulevya pamoja na udhalilishaji ili kuondosha kadhia hiyo katika Jamii.
Kufanya hivyo kutasaidia kupunguza majanga na maafa miongoni mwa Wananchi na kuwajenga Vijana kuwa tegemeo kubwa la nguvu kazi ya Taifa katika siku zijazo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed alieleza hayo wakati akizungumza na Masheha 31 kutoka Shehia zilizomo ndani ya Wilaya ya Magharibi “A” hapo Ukumbi wa Ofisi ya Wilaya hiyo iliyopo Mwera.
Nd. Shaaban alisema Viongozi hao wanalazimika kuzielewa na kuziwajibikia vyema dhamana zao za Uwenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama kwa kufanya vikao kwenye Shehia zao ili kujadili kwa kina matatizo yanayotendeka kwenye maeneo yao ikiwemo utumiaji wa dawa za kulevya na udhalilishaji kwa lengo la kuyapatia ufumbuzi wa kudumu.
Alisema kuna umuhimu mkubwa kwa Masheha kufanya Vikao vitakavyoandaa Ripoti zenye mapendekezo na hatimae kuzishauri Serikali za Mitaa kupitia Wakuu wa Wilaya ili kujenga Mustakabala mwema kuanzia ngazi ya Shehia hadi Wilaya.
“ ndugu Masheha niseme tu Serikali za Wilaya zinategemea sana ushauri wenu katika utendaji kazi wa kila siku”. Katibu Mkuu Shaaban alisisitiza.
Alieleza kuwa Sheha ni kiungo muhimu cha kuunganisha Serikali na Wananchi, hivyo ni vyema wakawajibika kwa karibu kuimarisha ushirikiano baina ya pande mbili hizo ili kuweza kutoa tija na kutatua changamoto zilizopo za vitendo vya udhalilishaji.
Akizungumza suala la Masheha kuyatambua maeneo ya uwajibikaji, Katibu Mkuu Shaaban alisema Sheha mzuri ni yule anayeyatambua maeneo yake katika Shehia wakati wote kwa kuzingatia uteuzi wao.
Alisema Serikali imeridhika na kuteuliwa kwao kutokana na uwezo mkubwa walionao wa kufanya kazi inayosaidia Serikali hasa katika masuala ya utatuzi wa changamoto zinazowakabili Wananchi kwenye maeneo yao.
“Kuteuliwa kwenu kumeonyesha imani kubwa kwa Serikali katika kutatua changamoto ikiwemo matatizo yanayoibuka hivi sasa ya vitendo vya udhalilishaji na tatizo la vijana kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya”. Alisema Nd. Shaaban.
Wakitoa michango yao Viongozi hao wa Shehia wamesema wamekuwa wakichukuwa jitihada kubwa za kuwabainisha wahalifu na kuwafikisha mbele ya vyombo vya Sheria lakini changamoto inayojitokeza hakuna hatua inayochukuliwa baada ya kuwakabidhi wahalifu hao ambapo muda mfupi baadae watu hao huendelea kuitamba mitaani.
Walisema jambo hilo kwa kiasi kikubwa hupelekea kuwashushia hadhi na hatimae kurejesha nyuma uwajibikaji wao wa kila siku.
Pamoja na mambo megine Masheha hao wamemuomba Katibu Mkuu kulifikisha Serikalini pendekezo lao la kupatiwa usafiri japo vyombo vya maringi mawili kama ilivyo kwa Masheha wa Pemba kutokana na maeneo yao kuwa makubwa wakati wa kutekeleza majukumu yao ili wapate unafuu.
Masheha wa Wilaya ya Magharibi “A” wakimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif hapo Ofisi ya Wilaya Mwera.
Masheha wa Wilaya ya Magharibi “A” wakimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif hapo Ofisi ya Wilaya Mwera.
Sheha wa Shehia ya Mtoni chemchem Bwana Rashid Rashid akitoa changamoto zinazowakabili katika utendaji wa majukumu yao ya kila siku za kupambana na dawa za kulevya na tatizo la udhalilishaji.
Picha na – OMPR – ZNZ.
No comments:
Post a Comment