RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza umuhimu wa kukuza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulkia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ili kuendeleza miradi kadhaa inayosimamiwa na Shirika hilo.
Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar
alipofanya mazungumzo na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tirso Dos Santos, wakati
Mwakilishi huyo alipofika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha na kumsalimia Rais.
Rais Dk. Shein alimueleza Mwakilishi huyo wa
(UNESCO) kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini sana uhusiano na
ushirikiano uliopo kati yake na Shirika hilo, hivyo ni vyema hatua hiyo
ikaendelezwa kwa azma ya kuimarisha miradi kadhaa iliyopo hapa nchini.
Alieleza kuwa Shirika hilo limeweza kushirikiana
na Zanzibar kwa muda mrefu hatua ambayo imepelekea kuimarika kwa miradi kadhaa
ambayo (UNESCO) inaiunga mkono ikiwemo miradi ya elimu, utamaduni, afya na
mengineyo ambayo imepata mafanikio makubwa hapa Zanzibar.
Hivyo, Dk. Shein alisisitiza kuwa kutokana na
uhusiano na ushirikiano huo wa muda mrefu ni vyema Shirika hilo likaendelea
kuipa kipaumbele miradi inayoimarishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
hasa katika Mji Mkongwe wake ambao ni urithi wa dunia.
Aidha, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo
kulipongeza Shirika hilo kwa kuendelea kushirikiana na Zanzibar na kuahaidi kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Shirika hilo ili kutekeleza
malengo yaliokusudiwa.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein amepongeza hatua za
Shirika hilo katika kusaidia uendelezaji wa miradi mbali mbali iliyopo Unguja
na Pemba ikiwa ni pamoja na mradi wa uimarishaji mawasiliano kwa jamii kwa
lengo la kutoa elimu kupitia redio Jamii iliyopo Micheweni Pemba.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliipongeza
Shirika hilo kwa kuendeleza juhudi zake za kuwaunga mkono vijana kupitia miradi
mbali mbali inayoendeshwa na Shirika hilo.
Mapema na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa
Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tirso Dos
Santos, alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Shirika hilo litaendelea kuiunga mkono
Zanzbar katika kuimarisha na kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo.
Mwakilishi huyo alimueleza Rais Dk. Shein kuwa
Shirika hilo linafarajika kwa kiasi kikubwa kwa kuona kwamba miradi mingi
inayoianzisha hapa Zanzibar inakwenda vizuri na imekuwa ikipata mafanikio.
Aidha, aliahidi kuwa (UNESCO) itaendelea kutoa
ushirikiano wake kwa Zanzibar sambamba na kuhakikisha miradi yote muhimu
iliyoanzishwa na inayotaka kuanzishwa inakwenda vizuri na kupata mafanikio
yaliokusudiwa.
Asema kuwa katika kuimarisha sekta ya elimu
(UNESCO) kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara
ya Elimu ina azma ya kuanzisha programu
ya “03” ambayo ina maana ya “ our right, our lives and our future” ambayo
itawasaidia vijana kutambua haki zao na kuwa na malengo juu ya maisha yao.
Kiongozi huyo alieleza kuwa mradi mwengine ni
mradi wa KOICA ambao una malengo ya kusaidia sekta ya elimu na kuwajengea uwezo
watoto wa kike na wanawake kwa jumla ambao utatekelezwa katika Wilaya nne za
Tanzania ambapo Zanzibar kwa upande wake Wilaya ya Mkoani Pemba itahusishwa.
Wilaya nyengine ni Sengerema, Kasulu na Ngorongore
kwa upande wa Tanzania Bara ambapo Mradi huu pia utayashirikisha mashirika ya
UNESCO, UN WOMEN na UNFPA.
Adha, Mwakilishi huyo aliitaja miradi mengine
ikiwemo ule utakaolenga Vyuo vya Serikali vya Amali pamoja na Skuli za Ufundi
hatua ambayo itakwenda sambamba na utoaji wa elimu na kujengea uwezo wa masoko
na wafanyakazi.
Mwakilishi huyo pia, alieleza azma ya Shirika lake
hilo katika kuiunga mkono Zanzibar kwa kupitia miradi yake ukiwemo mradi wa
uimarishaji wa Redio Jamii Unguja na Pemba ambapo redio hizo husaidia kutoa
elimu kwa jamii.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment