RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesisitiza haja kwa uongozi wa Wizara ya
Ardhi, Maji na Nishati kuvitumia vyombo vya habari kuyatangaza mafanikio iliyoyapata
ili wananchi wapate kuyajua.
Hayo aliyasema leo, Ikulu mjini Zanzibar
alipokutana na uongozi wa Wizara ya Ardhi, Maji na Nishati wakati ilipowasilisha
utekelezaji wa Mpango Kazi wa Julai 2018
hadi Juni 2019 sambamba na Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa mwaka 2019/2020.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa ni vyema wananchi
wakaambiwa mafanikio makubwa yaliopatikana kupitia Wizara hiyo kwa kuzungumza
na waaandishi wa Habari ama kwenda studio kuyaeleza kwani watakapokwenda huko
wananchi watapata kuyajua na watafurahi.
Amesema kuwa Serikali hii ni ya wananchi na ipo
kwa ajili ya kuwatumikia wananchi, hivyo ni vyema wakapewa taarifa zote
kuhusiana na shughuli mbali mbali zinazofanywa na serikali na hasa zile
zinazogusa maisha yao ya kila siku.
Aliwasisitiza viongozi hao kuvitumia vyombo vya
habari likiwemo Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) Redio na Televisheni kutoa
taarifa kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi na kuutaka uongozi huo kutoficha
habari kwani Serikali imefanya mambo mengi lakini wananchi hawayajui.
Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuupongeza
uongozi wa Wizara hiyo kwa kuwasilisha
vyema Mpango Kazi wao na kueleza kufarajika kwake kutokana na matumizi katika
Wizara za Serikali kwa kutambua kuwa tatizo hivi sasa sio fedha bali ni
matumizi.
Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
inazo fedha za kutosha kukidhi mahitaji ya Bajeti za Wizara zake kutokana na makusanyo
mazuri yanayofanywa na Taasisi husika zinazokusanya mapato zikiwemo ZRB na TRA.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali inajitahidi
kutekeleza wajibu wake katika kutafuta fedha kwa ajili ya kuendeleza mambo yake
ikiwemo miradi ya maendeleo jambo ambalo limeweza kuleta faraja katika kutekeleza
mipango ya nchi.
“Kuna mafanikio mengi yamepatikana katika miradi
mbali mbali ya maendeleo ndani ya Wizara hii ikiwa ni pamoja na mambo yote
manne na hivi karibuni limeingia la tano la mafuta na gesi asilia hivyo nina imani
kwamba mafanikio makubwa yatapatikana sasa ni vyema tukayatangaza, tukawaambiwa
wananchi wetu ili wayajue” alisema Dk. Shein.
Aliongeza kuwa katika Wizara hiyo kila Taasisi na
Idara zake zinaongozwa na Sheria hivyo ni rahisi kuiongoza na kuutaka uongozi
huo kufanya kazi kwa kuangalia sheria zilizopo hasa ikizingatiwa kwamba Zanzibar
ni mabingwa wa sheria.
Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuimarisha
mashirikiano yaliopo katika Wizara hiyo kwa lengo la kupata mafanikio makubwa zaidi
na kuupongeza uongozi wa Wizara hiyo kwa kuzidisha ushirikiano walionao.
Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza kazi nzuri ya uwasilishaji
iliyofanywa na Wizara hiyo huku akisisitiza haja kwa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA)
kutumia umeme wa jua ili kupunguza matumizi ya umeme uliopo ambao gharama yake
ni kubwa.
Mapema, Waziri wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati
na Mazingira Salama Aboud Talib alieleza kuwa Wizara hiyo inaendeleza juhudi na mikakati ya
Serikali ya kuhakikisha kuwa wananchi kwa ujumla wao wanapata huduma bora za
maji, nishati iliyo salama na endelevu, makaazi bora pamoja na matumizi mazuri ya
ardhi.
Waziri Salama alieleza kuwa Wizara yake kupitia
Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA),
imeendelea kusimamia shughuli za program za uhaulishaji na upanuzi wa
shughuli za maji Mijini na usambazaji maji vijijini.
Aidha, kwa maelezo ya Waziri Salama Mamlaka ya
Maji kupitia mradi huu imefanikiwa
kulaza mabomba kwa masafa ya kilomita 87.1 katika maeneo ya Bumbwisudi,
Kizimbani, Kianga, Welezo, Mikunguni, Mwembemakumbi, Makadara, Mwembeladu,
Rahaleo, Miembeni, Mkunazini na maeneo ya Mji Mkongwe.
Waziri huyo alieleza kuwa Wizara kupitia Mamlaka
ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (ZURA) imeendeleza juhudi za
kuimarisha mazingira bora ya utendaji wa kazi kwa kutekeleza shuguliza ujenzi
wa jengo la Ofisi Maisara ambapo ujenzi huo hadi kufikia Juni 2019 umekamilika kwa
asilimia 60.
Aliongeza kuwa Wizara hiyo pamoja na Wizara ya
Fedha na Mipango na Afisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar zilikamilisha majadiliano na Kampuni ya RAKGAS kwa kitalu cha
Pemba-Zanzibar na hatimaye Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia ilitia
saini Mkataba wa kwanza wa Mgawanyo wa uzalishaji wa mafuta na gesi asilia
Oktoba 28 mwaka jana 2018.
Mkataba huo kwa maelezo ya Waziri huyo unajumuisha
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Kampuni ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar na
Kampuni ya RAKGAS kutoka Ras al Khaimah.
Alieleza kuwa Serikali inaendelea na azma yake ya
kuhakikisha Zanzibar inazalisha umeme kwa kutumia nishati mbadala ya jua na
imeshatoa maamuzi ya uzalishaji wa nishati mbadala ya jua kwa kutumia mfumo wa
Mzalishaji wa kujitegemea ambapo bado Serikali inahusika kwa njia moja au
nyengine katika aina ya uwekezaji huo.
Aliongeza kuwa hivi sasa Wizara hiyo kwa
kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango inaendelea na matayarisho ya
kuangalia namna bora ya utekelezaji wa aina ya uwekezaji kwa kiwango cha
Megawati 30 MV.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Ali Khalil Mirza akieleza
Utekelezaji wa Malengo kwa kipindi cha Julai 2018 hadi Juni 2019 na alifafanua
juhudi zilizochukuliwa na Wizara kufanikisha miradi yake na kupongeza maelekezo
ya Dk. Shein katika utekelezaji wa zoezi hilo.
Nao uongozi wa Wizara hiyo ulieleza jitihada
zilizofanyika ikiwa ni pamoja na kutafuta mchanga na kufanikisha kuupata ambapo
umepelekea kuendelea vyema na ujenzi wa matangi ya Saateni kwa asilimia 80 na
Mnara wa Mbao asilimia 90 ambapo mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi
Septemba na mwezi Oktoba mwaka huu 2019 utafanyiwa majaribio na kuzinduliwa
katika sherehe za Mapinduzi zijazo
No comments:
Post a Comment